.

Jumatatu, 14 Oktoba 2013

"MWALIMU NYERERE ANGEKUWA HAI MPAKA SASA BASI ANGEHAMIA CHADEMA".....GAVANA

Aliyewahi kuwa Waziri wa Fedha na Gavana wa Tanzania (BoT) na baadaye mwasisi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edwin Mtei ameeleza jinsi alivyokuwa karibu na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere hadi kupata kazi hiyo ya juu.
Zaidi, kwenye mahojiano maalumu, nyumbani kwake Tengeru, Arusha, Mtei anabashiri kuwa iwapo kiongozi huyo angekuwa hai hadi leo, bila shaka angeachama na chama chake alichokiasisi na kujiunga na Chadema. Endelea…
Swali: Umepata kufanya kazi na Mwalimu Julius Nyerere, hivi huyu alikuwa ni mtu wa aina gani?
Jibu: Nilimfahamu Mwalimu mwaka 1959 mwishoni niliporudi nyumbani nikitokea masomoni Makerere nchini Uganda. Unajua Serikali ya Kikoloni haikunipa kazi, nikaamua kwenda Kenya kufanya kazi.


Siku moja nilikwenda kumtembelea Mwalimu nyumbani kwake nikiwa na rafiki yangu Mwanjisi, Mwanjisi ndiye aliyenipeleka.

Tulikaa tukaongea na tukafahamiana, ndipo alipotuambia kwamba ipo siku wakoloni wataondoka na sisi tutalitumikia taifa letu.
Mwalimu alikuwa ni mtu jasiri, ndiye aliyethubutu kuwaambia wakoloni waondoke, lakini hapo awali watu walikuwa wakiogopa kusema.
Yeye alisimama na kukemea ubaguzi wa aina yoyote.
Mwalimu pia alipenda haki na usawa. Hakupenda kabisa uonevu, lakini tatizo lake alikuwa haambiliki. Kile alichokisema alitaka hicho hicho kifuatwe, hakupenda mtu wa kumwambia hapana.
Swali: Mwalimu Nyerere alichukia nini enzi za uhai wake?
Jibu: Alichukia wezi wa mali ya umma na yeyote yule aliyekuwa mdokozi alimfukuza mara moja bila kumwonea haya. Unajua, Mwalimu alipobaini kwamba kuna mtu katika idara fulani hata wizara ni mzembe au mvivu, alimhamishia sehemu nyingine.
Mwalimu alikuwa tayari kuhakikisha wananchi wanamiliki rasilimali zao kama madini na wanazifaidi na siyo kuwapa wageni. Yeye alipenda Watanzania wafaidi rasilimali zao siyo chini ya asilimia hamsini.
Alisema wazi kabisa kwamba haya madini yaliletwa na Mungu hayakujileta yenyewe, hivyo alipenda wazawa wazifaidi rasilimali zao na siyo wageni.
Mimi nashangaa, baadhi ya viongozi wa CCM wa sasa tofauti na Nyerere, hawalioni hilo. Kuna tofauti kubwa kati yao na Mwalimu.  Yeye aliwapenda watu wake lakini viongozi wa CCM wanawachukia watu wao na kuwakumbatia wageni wanaowaita wawekezaji.
Swali: Ni tukio gani ambalo huwezi kulisahau wakati ukifanya kazi na Mwalimu Nyerere?
Jibu: Siwezi kusahau kipindi ambacho nilijiuzulu ugavana kwani tulitofautiana sana na Mwalimu hadi nikaamua kuuza nyumba yangu Dar es Salaam na kuhamia Arusha, na hapa nimekuwa mkulima hadi leo.
Unajua Mwalimu alikuwa mtu asiyependa demokrasia hata kidogo, alikuwa mtu ambaye haambiliki, yeye alipenda kile alichokisema tu kitekelezwe.
Mwaka 1977 Mwalimu Nyerere walitofautiana na Mzee Kenyata na alifunga mpaka wa Tanzania na Kenya, wakati huo Milton Obote (Rais wa Uganda enzi hizo) alikuwa ameporwa madaraka na Idd Amin na ndipo Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ikavurugika.
Mimi nikiwa ni Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo niliamua kurudi nyumbani.
Niliporudi nikapewa nafasi ya kuwa Waziri wa kwanza wa Fedha, wakati huo tukiwa katika vita ya Uganda na mimi ndiye nilikuwa nikisimamia masuala ya uchumi na fedha wakati wote wa vita. Vita  ilipoisha nchi yetu iliingia katika mtikisiko mkubwa wa kiuchumi, hatukuwa na fedha kabisa.
Ndipo nikaamua kumshauri Mwalimu, kwamba tukope fedha katika Benki ya Dunia ili kutatua suala hili. Baada ya kushauriana na watu wa Benki ya Dunia nilimwambia Mwalimu pia tupunguze bajeti ya matumizi yetu, nilimshauri vitu vingi kwa kweli.
Unajua, Mwalimu alinijibu kwamba mimi nimeshawishiwa na watu wa Shirika la Fedha Duniani (IMF), ndipo nikaamua kujiuzulu. Huwezi kuamini na siku najizulu Mwalimu alitoa hotuba ya kuridhia kujiuzulu kwangu na kusema kwamba ‘kamwe hawezi kuruhusu serikali yake iongozwe kutoka Washington.’
Hakika nilishtushwa na hotuba yake baada ya mimi kujiuzulu ukizingatia ya kwamba mimi nilikuwa nimelitumikia taifa langu kwa uadilifu mkubwa, ndipo nikaamua kuwa mkulima hadi leo. Niliuza nyumba yangu Dar es Salaam na kununua shamba kubwa hapa Tengeru mkoani Arusha.
Mwalimu alipenda watu wa kumwambia ‘ndiyo mzee’ na bahati mbaya mimi sikuwa mtu wa namna hiyo. Kila alichokisema alitaka kifuatwe na hata umma unajua kwamba mimi nilithubutu kumwambia Mwalimu ‘hapana’.
Swali: Ni jambo gani zuri ambalo unalikumbuka kwa Mwalimu Nyerere?
Jibu: Kwanza kabisa, yeye ndiye mwasisi wa taifa letu, alipenda sana nchi yake na hata pia alipenda uhuru wa nchi nyingine barani Afrika. Ndiyo maana wakati mwingine alikuwa tayari kuchelewesha uhuru wa Tanganyika ili nchi nyingine za Afrika zipate uhuru.
Hakika, Mwalimu aliipenda sana Afrika, alisaidia harakati za ukombozi wa nchi mbalimbali za Afrika, alikuwa mzalendo wa kweli ambaye hakuwahi kutokea kabisa kabla yake.
Hii nchi aliyoipigania Mwalimu ibaki moja, tusiigawe vipande vipande. Isiwe kundi la watu fulani linapokea mapesa na wengine wanyonge wanataabika, wanakufa na njaa. Leo tunasikia kuna vigogo wanaficha mapesa nje ya nchi hii ni ajabu sana”.
Swali: Iwapo Mwalimu Nyerere angelikuwa hai, je, unadhani angekemea mambo gani?
Jibu: Kwanza kabla ya kukujibu, Mwalimu angekuwa hai leo nakuambia kwanza tayari angekuwa ameshajiunga Chadema.
Na tuna imani huko aliko anatupigia makofi kwa kazi nzuri tunayoifanya ya kukemea ufisadi na rushwa kama sera yake ilivyokuwa.
Unajua Mwalimu enzi za uhai wake alishawahi kutuambia mbele yangu kwamba Chadema ndicho chama mbadala wa CCM.
Ndicho chama kitakachoweza kuongoza nchi hii baada ya CCM na leo tunaona utabiri wake. Lakini, niseme angekuwa hai angekemea vitendo vya kukithiri kwa rushwa na ufisadi, kwani sasa tunaona kundi la walionacho na wasionacho linavyokua hapa nchini.
Swali: Je, unadhani misingi aliyoiacha Mwalimu Nyerere inafuatwa leo hii?
Jibu: Kwanza kwa uhuru aliotupatia, hilo hakuna mtu wa kutupora. Kingine, misingi yake haifuatwi kabisa.
Mwalimu alipenda haki na usawa, maskini wapate na matajiri wapate, lakini kwa hali ya sasa hatuna viongozi wa kukemea rushwa wala ufisadi kwa kuwa hata wao wamechaguliwa kutokana na mkondo wa rushwa. hiyo hiyo.

-----MWANANCHI 
Mtete Focus Blog
    

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni