.

Alhamisi, 10 Oktoba 2013

GAZETI LA MWANANCHI LAMALIZA ADHABU YAKE YA KUTOCHAPISHWA KWA SIKU 14....


Tiddo
Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications limited (MCL)Tido Mhando (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari jijini kuhusu kuanza uchapishaji wa gazeti la Mwananchi


Kupitia mtandao wake MWANANCHI imeandika taarifa ya kutoka kifungoni, na jinsi ambavyo adhabu hiyo ilivyowapa hamasa kubwa imewaathiri watu mbalimbali wakiwemo waandishi, vijana wanaosambaza na wengine, pia wameeleza msimamo wao baada ya adhabu hiyo. Isome kama ilivyoandikwa.
“Hatua ya kulifungia gazeti hili kwa sababu za kufikirika imesababisha maumivu kwa watu wengi. Vijana (vendors) waliokuwa wakiuza na kusambaza gazeti hili pamoja na familia zinazowategemea wameumia. Waandishi wa kujitegemea wanaolipwa kutokana na habari wanazotuma gazetini wameumia pamoja na familia zao.
Tumetoka kifungoni tukiwa na somo muhimu. Kwamba sheria kandamizi kama Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 haisimamii masilahi ya taifa, bali kundi la watu wachache. Ni sheria kandamizi ambayo kwa umoja wetu tunaweza kuifuta. Tungependa kuwashukuru wasomaji wetu na wananchi kwa jumla kwa kuwa nasi katika kipindi kigumu tulichokuwa kifungoni. Vilevile, tunavishukuru kwa namna ya pekee vyombo vyote vya habari vya ndani na nje ambavyo vilisimama imara kupinga hatua ya Serikali kufungia magazeti.
Tutakuwa watu wasio na shukurani kama hatutatambua mshikamano mkubwa ulioonyeshwa na asasi za kiraia, mabalozi na watu mbalimbali kupinga matumizi ya sheria hii kandamizi. Hatujakata tamaa, bali tumetoka kifungoni tukiwa na hamasa kubwa kuendelea kuwapa habari wananchi pasipo woga wala upendeleo.
Hatupambani na Serikali, lakini tutaendelea kuikosoa pale inapofanya makosa na tutaipongeza pale inapotimiza wajibu wake. Tunawaomba wasomaji wetu mwendelee kutuunga mkono”.
SOURCE: MWANANCHI
 
Mtete Focus Blog 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni