.

Alhamisi, 26 Desemba 2013

"Nitaongea kila kitu baada ya Sikukuu"....Pinda


Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ambaye anakabiliwa na shinikizo la kujiuzulu amesema atazungumzia hatima yake baada ya sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.
Gazeti  la The Citizen, lilimkariri Pinda jana akisema kwa sasa anahitaji amani na utulivu katika kipindi hiki cha sikukuu baada ya shughuli za kikao kilichopita cha Bunge.
Katika kikao hicho, mawaziri wanne walitimuliwa baada ya ripoti ya kamati ndogo ya Bunge kufichua madhara yaliyojitokeza wakati wa utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili.

Wabunge kadhaa walishinikiza kujiuzulu kwa Pinda na mawaziri wengine, ambao wizara zao zilihusika katika utekelezaji wa operesheni hiyo.
“Baada ya kikao cha Bunge Dodoma nilikwenda likizo kuwasalimia wazazi wangu. Wasiliana na mimi baada ya likizo halafu niulize maswali yako yote nitakujibu,” alisema Pinda, ambaye yuko katika Kijiji cha Kibaoni, Mkoa wa Katavi.
Rais Jakaya Kikwete alitengua uteuzi wa mawaziri Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii), Dk Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani), Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa) na Dk David Mathayo(Uvuvi na Maendeleo ya Mifugo), baada ya malalamiko ya wabunge.
Pinda alikiri bungeni kuwa operesheni hiyo ilikuwa na matatizo na wale wote waliokuwa na dhamana walikiuka taratibu za utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili.
Pamoja na kujiuzulu kwa mawaziri hao, pia Serikali itaunda tume, ambayo itaongozwa na Jaji ili kuchunguza sakata hilo undani.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni