.

Jumapili, 29 Desemba 2013

Chadema kuamua hatma ya Uanachama wa Zitto mwakani...atakiwa kujieleza kwanini asifukuzwe Uanachama..!!


KAMATI Kuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), inayotarajiwa kuketi mwishoni mwa mwezi Februari mwakani, ndiyo itakayoamua hatma ya kisiasa ndani ya chama hicho kwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe.

Zitto alivuliwa wadhifa wake wa Unaibu Katibu Mkuu wa chama hicho na kamati hiyo iliyoketi kwa siku mbili kuanzia Novemba 20-21, na kumpa siku 14 za kujieleza kwanini asifukuzwe uanachama kwa tuhuma za kukihujumu, kukisaliti chama chake na viongozi wenzake.

Desemba 10, mwaka huu, Mbunge huyo wa Chadema aliwasilisha utetezi wake Makao Makuu ya Chama hicho.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili lililotaka kufahamu hatua ya chama ilipofikia hasa baada ya Zitto kuwasilisha utetezi wake, Katibu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa alisema maamuzi dhidi ya rufaa hiyo yataamuliwa na Kamati Kuu itakayoketi kulingana na Kalenda yake.

“Iko Kamati Kuu na huko kuna taratibu zake kwani kamati hiyo haikai kwa ajili ya mtu mmoja, huko itasikilizwa na kutolewa maamuzi kulingana na kalenda yake” alisema Dk. Slaa.

Hata alipotakiwa kufafanua kuwa Kamati Kuu itakutana lini Dk Slaa hakuwa tayari kwa madai kuwa suala hilo ni kwa mujibu wa kalenda ya chama hicho.

Gazeti hili lilimtafuta msemaji wa Chadema, Tumaini Makene ambaye alisema kamati hiyo itakaa kwa mujibu wa ratiba yake iliyopo ndani ya Katiba ya Chama hicho pasipo kutaja tarehe wala mwezi.

“Kamati itakaa kwa mujibu wa Katiba, angalia ndani ya Katiba utagundua inakaa baada ya muda gani,” alisema Makene.

Kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho, kamati kuu huwa inaketi kila baada ya miezi mitatu ndani ya mwaka.

Katika Katiba hiyo sura ya saba imeandikwa kuwa “7.7.15 Kamati Kuu itakutana mara nne (4) kwa mwaka. Vikao maalum/dharura vinaweza kuitishwa kadri itakavyolazimu kwa mujibu wa kanuni za Chama,” ilieleza.

Hivyo mkutano ujao unatarajia kuwa mwezi Februari mwishoni mwaka 2014.

Mbali na Zitto, kamati kuu hiyo ya Chadema iliyoketi katika ukumbi wa wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam ilifikia uamuzi wa kuwavua uongozi viongozi wake wengine wawili wakihusishwa na tuhuma za usaliti wa kuandaa mpango wa kufanya mabadiliko ya uongozi ndani ya chama hicho.

Viongozi waliovuliwa uongozi kwa kuhusika na Waraka huo ni mjumbe wa Kamati Kuu pamoja na Dk Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Arusha.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni