.

Alhamisi, 26 Desemba 2013

Madawa ya Kulevya yanaswa yakiwa yamefichwa ndani ya Maiti huko Morogoro..!!


JESHI la Polisi mkoani Morogoro limekamata dawa za kulenya zilizokuwa zimefichwa ndani ya maiti pamoja watu watatu waliokuwa wakiusafirisha mwili huo. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile alimtaja marehemu huyo kuwa ni Khalid Abdul Kitara (47) mfanyabiashara na mkazi wa Kariakoo jijini Dar es salaam.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni madereva wawili waliokuwa wakipokezana kuendesha gari hilo ambao ni Teddy Sichilima (27), mkazi wa Tunduma Mbeya, Lucas Atubonekisye (32) mkazi wa Mtaa wa Songea Tunduma na aliyekuwa na mwili wa Marehemu Jumbe Mbano (36) mfanyabiashara na mkazi wa Kariakoo.

Alisema marehemu huyo baada ya kufanyiwa uchunguzi alikutwa na kete 17 zikiwa tumboni, na saba zilikutwa kwenye begi dogo la watuhumiwa hivyo kufanya idadi ya kete hizo kuwa 24.

Kamanda Shilogile alisema walipata taarifa kutoka kwa msamaria mwema kuwa kuna gari lilikuwa likitokea Mbeya likiwa na mwili wa marehemu ambao unadhaniwa kuwa na dawa ya kulevya.

Alisema baada ya kupata taarifa hizo polisi waliweka kizuizi katika kituo cha polisi Mikumi, na ilipofika saa 3:30 usiku gari hilo lilisimamishwa na kupekuliwa huku maiti ikiwa imelazwa ndani ya gari hilo likiwa na madereva wawili na abiria mmoja na marehemu.

Alisema watu hao walikamatwa na kupelekwa kituo kikuu cha polisi kisha kuhojiwa, ambapo walisema marehemu huyo alifariki Desemba 23 mwaka huu katika Hospitali ya Vwawa iliyopo Wilaya ya Mbozi Mkoani Mbeya.

Shilogile alisema watuhumiwa hao wakiwa na marehemu alianza kuumwa, hivyo kumpeleka hospitalini hapo na kudanganya kuwa marehemu anasumbuliwa na ugonjwa wa kisukari na baadaye kufariki wakati akipatiwa matibabu na watuhumiwa kupewa mwili wao.

Hata hivyo alisema, kete hizo zitapelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ili kubaini uzito wake pamoja na thamani na kwamba baada ya majibu kutolewa watuhumiwa watafikishwa mahakamani.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni