.

Jumapili, 21 Septemba 2014

CHADEMA Wasisitiza kuwa Maandamano Bila Kikomo


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesisitiza kuwapo kwa maandamano yasiyo na kikomo yatakayoanza leo katika baadhi ya mikoa licha ya jeshi la polisi kuzuia.
 
Chama hicho kimesema maandamano hayo  yana lengo la kushinikiza kuahirishwa kwa Bunge la Katiba linaloendelea mjini Dodoma.
 
Malengo mengine ni kuitaka Sheria ya Mabadiliko ya Katiba itekelezwe katika upatikanaji wa Katiba mpya na kupinga uchakachuaji dhidi ya maoni yaliyotolewa na wananchi kupitia Tume ya Jaji Mstaafu Joseph Warioba.
 
Akizungumza na NIPASHE , Mkuu wa Idara ya Mawasiliano  wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tumaini Makene, alisema tayari mikoa kadhaa na wenyeviti wa mikoa wa chama hicho, wameshapeleka barua polisi ili kutekeleza hilo.
 
Alisema barua hizo lengo lake ni kupata ushirikiano wa kiulinzi kwa jeshi hilo na siyo kuomba kibali kama ilivyozoeleka. Alisema mikoa ambayo leo itaandamana ni Iringa, Arusha na Morogoro huku Tanga, Manyara, Kilimanjaro, Mbeya, Mwanza na Musoma wanatarajia kuyafanya Jumatatu.
Mbowe (1)
ARUSHA WAJIANDAA NA MAANDAMANO
Chadema mkoa wa  Arusha, kimesema  maandamano yatakayoanza leo waandamanaji watavaa vitambaa vyeupe kusisitiza amani.
 
Akizungumza jana kwa njia ya simu, Mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Arusha, Amani Golugwa , alisema wamepokea barua ya  Polisi ambayo imezuia maandamano na mkutano wa hadhara waliopanga kufanya leo. Alisema katika barua hiyo hakuna sababu za msingi zilizotolewa hivyo Chadema na Ukawa wataandamana kwa lazima na hakuna mtu yeyote atakayeguswa.
 
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatusi Sabasi, alisema hakuna maandamano yaliyoruhusiwa na atakayeandamana  atakabiliana na mkono wa sheria.
 
Wakati hali hiyo ya sintofahamu ikiendelea baadhi ya makada wa chama hicho wameonekana wakiwa katika harakati za kupamba magari yao kwa maandishi ya kulaani Bunge la katiba kama maandalizi ya maandamano ya leo.
 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni