.

Jumatano, 22 Januari 2014

Kampeni Mpya za CHADEMA kutikisa Nchi Nzima….Helikopta tatu kurushwa Angani Siku 14 Mfululizo.


MBOWE
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuanzia leo, kinarusha helkopta tatu kwa siku 14 mfululizo, katika  kutekeleza kampeni iliyopewa jina la Operesheni Pamoja Daima (ODB) itakayoendeshwa katika mikoa yote nchini.
Ziara hiyo inaanzia katika mikoa ya Tanga, Mwanza na Ruvuma, huku viongozi wa chama hicho wakijigawa katika makundi sita; matatu yakitumia helkopta na matatu yatawafikia wananchi kwa kutumia usafiri wa magari.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa, lengo la operesheni hiyo ni kukiimarisha chama hicho na kuwafumbua macho wananchi kuhusu mchakato wa Katiba Mpya.
“Tumejigawa katika makundi sita na makundi matatu kati ya hayo yatatumia helikopta kila moja, makundi mengine yatawafikia wananchi kwa misafara ya ardhini,” alisema Mbowe na kuongeza;
“Viongozi wakuu wa chama, wabunge, wenyeviti wa mikoa, wilaya, majimbo na kanda kila mmoja atashiriki kwa nafasi yake katika operesheni hii. Tutafanya mikutano kwa wiki mbili, ila tunaweza kuongeza wiki nyingine moja.”
Alisema chama hicho kimejipanga kuwafikia wananchi wengi kadri itakavyowezekana, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya uchaguzi wake wa ndani kuanzia ngazi ya mashina, uchaguzi mdogo wa madiwani katika Kata 27 nchini utakaofanyika Februari 9, mwaka huu pamoja na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
chadema
“Naomba tueleweke, katika hili hatufanyi kampeni hata kidogo, huu ni mwendelezo wa maandalizi ya chaguzi mbalimbali. Kama mnakumbuka tulianza kujiandaa na uchaguzi wa mwaka 2015 baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa 2010,” alisema Mbowe na kuongeza;
“Kwa sasa tunachokifanya ni kuongeza nguvu na umakini zaidi. Makundi yataanzia katika mikoa ya Tanga, Mwanza na Ruvuma, tutapita kila Kata ambazo utafanyika uchaguzi wa madiwani.”
Mbowe alisema operesheni hiyo itapiga kambi katika Jimbo la Kalenga ambalo kwa sasa lipo wazi baada ya mbunge wake ambaye pia alikuwa Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk William Mgimwa kufariki dunia Januari 1, mwaka huu nchini Afrika Kusini.
“Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) haijatangaza kufanyika uchaguzi katika jimbo hilo, Chadema tutafika Kalenga na tutafanya mkutano maalumu na kutoa pole kwa wakazi wa jimbo hilo kutokana na msiba mkubwa wa mbunge wao,” alisema Mbowe.
Operesheni hiyo inafanyika siku chache tangu chama hicho kikuu cha upinzani nchini kipite katika mgogoro ambao ulisababisha aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wake, Zitto Kabwe kukimbilia mahakamani ili kunusuru uanachama wake.
Wakati Zitto akinusurika kufukuzwa kutokana na zuio la mahakama, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoani Arusha, Samson Mwigamba na Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitila Mkumbo walifukuzwa uanachama, likiwa ni hitimisho la mchakato ulioanza kwa kuwavua nyadhifa zao pamoja na Zitto.

SOURCE: Mwananchi

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni