.

Alhamisi, 26 Septemba 2013

Mwanza washikana mashati kuhusu mipaka ya jiji hilo na manispaa ya Ilemela....Rais KIKWETE atishia kulifuta jiji la Mwanza.


AULI ya Rais Jakaya Kikwete katika ziara yake ya siku saba mkoani Mwanza hivi karibuni kuhusu uhalali wa mipaka inayounda Halmashauri ya Jiji la Mwanza imeibua mchanganyiko baina ya Jiji na Manispaa ya Ilemela. Hali imewalazimisha maofisa wa Halmashauri kwenda Dar es salaam kupata ufafanuzi wa kina.

Rais katika ziara hiyo alikaririwa akieleza kuwa Halmashauri ya Jiji la Mwanza haiwezi kukamilika bila kujumuisha eneo lote la mipaka ya Manispaa ya Ilemela.

“Wakati nakubali kuanzisha Manispaa ya Ilemela nilitoa maelekezo kuwa eneo la utawala la Jiji la Mwanza litakuwa likijumuisha Manispaa ya Ilemela.

“Leo hii kutenganisha Nyamagana ndiyo iwe jiji pekee na Ilemela iwe manispaa uhalali wa kuwepo kwa jiji la Mwanza haupo kwa sababu ili upate jiji la Mwanza kwa ujumla ni lazima uitamke na Ilemela.

“Nyamagana ukisema kwa mfano ndiyo iwe jiji haikidhi vigezo vya kuwa jiji…katika hili ninawaomba viongozi husika kuwasiliana na Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za mikoa na Serikali za mitaa(TAMISEMI) kupata tafsiri zaidi,” alisema.

Habari zinasema viongozi wa Jiji l Mwanza ambao kwa muda mrefu wamekuwa na mgogoro na Manispaa ya Ilemela kuhusiana na mipaka ya utawala wamefunga safari kwenda Dar es Salaam kuonana na Waziri wa TAMISEMI, Hawa Ghasia kwa kupata ufafanuzi zaidi.

Meya wa Manispaa ya Ilemela, Henry Matata alikiri kwa simu kuwa yuko Dar es Salaam kwa ajili ya kuonana na viongozi wa TAMISEMI kujua uhalali wa mipaka ya jiji kama unajumuisha pia mipaka ya manispaa yake.

Hapa ninapozungumza nawe tayari niko Dar es Salaam kuonana na viongozi wa TAMISEMI kuitikia wito wa Rais kwa sababu suala hilo limekuwa likituchanganya kwa muda mrefu,” alisema Matata.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza Francis Mkambenga alisema Halmashauri imewakilishwa na Meya wa Jiji hilo, Stanslaus Mabula na Mkurugenzi wa Jiji, Hassan Hidda.

-Mtanzania

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni