Mtoto mchanga mwenye umri wa miezi minne amezua kizaazaa cha aina
yake, baada ya kuwapo taarifa kwamba mara kadhaa umbo lake limekuwa
likigeuka na kuwa nyoka na mwili wake ukiendelea kudhoofu kutokana na
kukataa kunyonya maziwa ya mama yake.
Mtoto huyo (jina lake tunalihifadhi kwa sasa), wiki iliyopita alivuta
umati wa wakazi wa Kijiji cha Nkome mkoani Geita ambao walifurika ndani
na nje ya Kanisa la AICT Nkome, lililopo kijiji hapo,
kushuhudia maombi ambayo alikuwa akifanyiwa ili kumkomboa katika kile
kilichotafsiriwa kuwa ni mateso dhidi yake.
Ilikuwa saa 4.00 asubuhi Jumamosi, Novemba 8 mwaka huu wakati mtoto
huyo alipofikishwa katika kanisa hilo na kuanza kufanyiwa maombi na
sababu ya hatua hiyo ikielezwa kuwa ni kutokana na kuwa na umbo la nyoka
na kwamba matendo yake yanaashiria kwamba mwenye asili ya nyoka ndani
ya roho yake.
Mtoto huyo alifikishwa kanisani hapo na mama yake mzazi, Sarah Silasi
wakitokea Kijiji cha Ichile, Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, ambako
alikimbia matukio yanayohusishwa na ushirikina.
Mmoja wa wazee wa kanisa hilo la AIC Nkome, Mathew Misana anasema: “Alikuwa
anatoa ulimi mithili ya nyoka, mwendo wake anapolala alijizungusha kama
nyoka na hata alipojikunja mwili wake ulikuwa kama unavyoona nyoka.”
Misana anasema matukio hayo na mengine kadhaa yakiwamo ya ngozi ya
mtoto huyo kuwa nyeusi kama ya nyoka aina ya chatu, yaliwalazimisha
ndugu na jamaa zake wakiongozwa na mama mzazi kutaka aombewe.
“Ngozi yake kuonekana kama ya mzee huku macho yake
yakionekana kuwa makubwa na kichwa chake kuwa na umbo la nyoka pamoja na
miguu, baada ya kuona hali hii tukaihusisha na mambo ya kishirikina na
kuamua kuanza maombi,” alisisitiza.
Hata hivyo, muda mfupi baada ya maombi kuanza, taarifa za kuwapo kwa
aina hiyo ya mtoto zilisambaa haraka na kusababisha umati mkubwa wa watu
kujaa ndani ya kanisa hilo ambalo ni boma kwa maana kwamba ujenzi wake
bado unaendelea.
“Watu wengi walijaa na wengine wakawa wanapanda juu ya miti na juu ya
boma wakati mwingine matofali yalianguka. Hewa ikapungua na usalama
ukawa mdogo kwani watu walisukumana wakitaka kushuhudia,” anasema
Misana.
Baada ya watu kuwa wengi, uongozi wa kanisa uliomba msaada wa Polisi
wa Kituo cha Nkome ambao walifika kanisani hapo na kushauri mtoto huyo
aonyeshwe ili watu waweze kuridhika kwamba hakuwa amegeuka kuwa nyoka.
Uongozi wa kanisa ulifanya hivyo lakini mwonekano wa mtoto huyo
ulisababisha watu kuongezeka badala ya kupungua na hapo ndipo polisi
walipoelekeza mama wa mtoto huyo ambebe na kuondoka naye hadi kituoni.
Mwinjilisti wa kanisa hilo, Emmanuel Misungwi anasimulia: “Tumeshudia
vitu visivyo vya kawaida wakati tunafanya maombi na wakati tunaendelea
na huduma, mama wa mtoto Sarah alianguka akaanza kuongea juu ya mtoto
kwa nguvu ya mapepo.”
Anasema hali hiyo iliwavuta watu wengi kiasi cha usalama wa mtoto
kuwa mdogo, ndipo walipoamua kuomba msaada wa ulinzi kutoka polisi.
“Ilibidi polisi waingilie kati, walimchukua mtoto na kuondoka naye na
kuwaridhisha wananchi kwa kumwonyesha hadharani ili kila mtu aone kama
kweli ni nyoka kama uvumi ulivyokuwa umeena au la,” anasema Misungwi.
Kituo cha polisi
Baada ya mama huyo na mwanaye kufikishwa polisi, umati wa watu
ulihamia katika kituo hicho na kuwafanya askari kufanya kazi ya ziada
kuwaondoa watu waliokuwa wamekusanyika katika eneo hilo.
Licha ya wananchi kufukuzwa waliendelea kun’gang’ania kukaa katika
kituo hicho, hali ambayo ilisababisha polisi kumwondoa mwanamke huyo kwa
kificho na kumpeleka nyumbani kwa mchungaji wa kanisa hilo, Mchungaji
Mkuu wa Kanisa hilo Jonh Marko.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Nkome, Charles Belenge alithibitisha
kuwepo kwa tukio hilo na kusema kuwa hali hiyo imesababisha vurugu
wakati wa maombi.
“Nikweli tukio hilo lipo la kudai mtoto anabadilika kuwa nyoka, kwa
kweli limetupa shida kwani hali ya utulivu katika kijiji ilibadilika kwa
muda, lakini tumejitahidi kufanya udhibiti,” anasema Belenge.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Geita, Joseph Konyo alithibitisha kuwapo
kwa tukio hilo na kwamba walikuwa wakilifanyia uchunguzi wa kina.
“Haya mambo ndiyo yanasababisha mauaji ya mapanga, hivyo kama Jeshi
la Polisi tutafuatilia kujua kwa kina ili lisije kusababisha madhara ya
mauaji ya kukatana kwa mapanga,” alisema Konyo.
Alihusisha tukio hilo na uelewa mdogo wa wazazi na wachungaji
waliokuwa wakifanya maombi na kwamba mtoto huyo huenda alikuwa
anasumbuliwa na maradhi ya utapiamlo, tofauti na mawazo kwamba tatizo ni
nguvu za giza.
“Kazi tunayoifanya kama Jeshi la Polisi ni kuweka ulinzi kwa kuzuia
wasifanye maombezi eneo la kanisa hilo ambalo kiukweli liko wazi sana
kwani usalama utakuwa mdogo pia tuombe wanaohusika wampeleke mtoto
hospitali,” alisema Konyo.
Mashuhuda wa maombi
Misana anasema wakati wakifanya maombi mtoto huyo alikuwa hatoi sauti
isipokuwa alikuwa anatoa ulimi kama ufanyavyo nyoka na kwamba ulimi huo
ulikuwa mrefu mpaka shingoni pamoja na macho yake kuwa makubwa.
Mashuhuda wengine walisema kuwa waliona mtoto huyo akigeuka kimaajabu
na kuwa na maumbo mithili ya nyoka na baadaye kurudi katika umbo la
binadamu.
“Mimi nimeona wakati anaombewa alikuwa anatoa ulimi kama nyoka,
alikuwa anasimamisha kichwa na kutoa ulimi hadi unagusa shingo halafu
tumbo, miguu na kiuno vilizunguka,” anasimulia mkazi wa Nkone, Shaban
Masembe.
Naye Neema Masatu anasema: “Niliambiwa Kanisa la AIC kuna mtoto
anabadilika kuwa nyoka anafanyiwa maombi ikabidi nije nijionee, nimefika
hapa nikakuta kweli watu wamejigawa makundi mawili; wengine wanamuombea
mama wa mtoto na wengine mtoto.”
Masatu anafafanua kuwa alichokiona si nyoka isipokuwa ameona mtoto
huyo akiwa anatembea kama nyoka, anajikunja miguu inagusa shingo kisha
kichwa anakisimamisha kama nyoka na kutoa ulimi mrefu na mdomo na macho
yake yalikuwa yanakuwa makubwa.
Naye Pili Nyachimb’huga anasema: “Sijaona, watu walikuwa wengi
nimefika hapa hata sikuweza kumuona ila watu wanasema alikuwa mtu
anayefanana na nyoka, alikuwa anaachama kama nyoka na kwamba alikuwa
anatanuka mwili wake unakuwa mkubwa”.
Ni ipi historia ya mtoto huyu? Usikose toleo lijalo ambapo mama mzazi
atazungumzia kwa undani sababu za mtoto wake kuwa na matendo
yanayofanana na ya nyoka.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni