KIJANA "ANG'OLEWA" MENO 232
Madaktari nchini India wametoa meno 232 kutoka katika mdomo wa kijana
mwenye umri wa miaka 17, katika upasuaji uliochukua saa saba.
Kijana
huyo Ashik Gavai alifikishwa hospitali akiwa amevimba na maumivu kwenye
taya na shavu lake la upande wa kulia, amesema Dokta Sunada Dhiware,
mkuu wa idara ya meno katika hospitali ya JJ jijini Mumbai.
Kijana huyo amekuwa akisumbuliwa kwa miezi 18, na alilazimika kusafiri kwenda mjini, baada ya madaktari katika kijiji chake kushindwa kufahamu chanzo cha tatizo.
Madaktari wameelezea hali hiyo kuwa "ni haba sana" kutokea na ni jambo ambalo "limevunja rekodi ya dunia".
Upasuaji huo uliofanyika siku ya Jumatatu, ulihusisha madaktari wawili na wasaidizi wawili.
Ashik sasa ana meno 28.
"Ashik aligunduliwa kuwa na ugonjwa wa aina yake ambao ufizi mmoja
huunda meno mengi. Ni kama aina ya uvimbe wa saratani," amesema Dokta
Dhiware.
"Mwanzoni, hatukuweza kukata fizi, kwa hiyo tulilazimika kutumia nyundo na tindo kufanikisha.
"Tulivyopasua tu, meno madogo madogo yakaanza kutoka, moja baada ya
jingine, na tulipoyahesabu, yalifika meno 232." Amesema daktari huyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni