Kampuni
ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL),
imemfungulia kesi Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi)
katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ikimtaka aombe radhi na
kulipa fidia ya Sh bilioni 310.
Katika kesi hiyo ya madai, Kafulila anadaiwa kuidhalilisha kampuni hiyo, kutokana na kauli alizotoa dhidi yake (IPTL).
IPTL
na walalamikaji wengine Pan Africa Power Solution (PAP) na Mkurugenzi
wa PAP, Harbinger Seth wanamlalamikia Kafulila kuwatuhumu kuchukua fedha
kinyume cha sheria katika akaunti ya Escrow iliyopo Benki Kuu ya
Tanzania (BoT).
Walalamikaji
hao kupitia kwa Wakili wao, Augustine Kusalika wamefungua kesi hiyo,
wakitaka Kafulila awalipe Sh bilioni 210 kama fidia ya kutoa kauli za
udhalilishaji, kuwasababishia hasara katika biashara na kuharibu
mtazamo wa biashara zao.
Aidha,
wanaiomba Mahakama iamuru Kafulila, awaombe radhi, pia awalipe Sh
bilioni 100 kama hasara ya jumla pamoja na usumbufu walioupata, kutokana
na kauli za udhalilishaji.
Kwa
mujibu wa hati ya madai, iliyopatikana mwishoni mwa wiki, Juni mwaka
huu Kafulila alitangaza kuwa IPTL na Seth, walijipatia fedha kutoka
akaunti ya Escrow kinyume cha sheria na kumuita Seth ni ‘Singasinga’,
jambo lililomdhalilisha na kumharibia muonekano wake na biashara yake.
Walalamikaji
hao wanadai kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, bila
kuwa na haki, Kafulila alitoa taarifa hizo, kuwa IPTL inajihusisha na
biashara zisizo halali na za uongo, jambo lililosababisha jamii kuamini
na kuwaharibia mtazamo wa kibiashara.
Aidha,
wanadai Kafulila akiwa mbunge alipoteza kinga ya wabunge inayowalinda
wakizungumza bungeni, kwa kuwa alitoa taarifa hizo nje ya shughuli za
Bunge.
Walidai
Kafulila anaendelea kutoka taarifa hizo, licha ya kumpa taarifa kwa
maneno na maandishi, wakimtaka kuacha kufanya hivyo, kwa kuwa
anawaharibia biashara kitaifa na kimataifa.
Kwa
mujibu wa hati ya madai, IPTL iliingia mkataba na Shirika la Umeme
Tanzania (Tanesco) kwa ajili ya kusambaza umeme kwenye shirika hilo,
lakini kulitokea mgogoro kati ya IPTL, Kampuni ya VIP Engineering and
Marketing na Tanesco, jambo lililosababisha wafike Mahakama Kuu.
Kutokana
na mgogoro huo, Mahakama iliamuru Sh bilioni 200 zilizokuwa kwenye
akaunti ya Escrow, zisitolewe hadi kesi hiyo itakapokwisha na baada ya
kesi kuisha, Mahakama iliamuru IPTL ichukue fedha hizo.
Walalamikaji
hao wanadai licha ya Kafulila, kujua kuwepo kwa mgogoro huo, aliendelea
kutoa tuhuma hizo, huku akijua kuwa IPTL imechukua fedha hizo kwa amri
halali ya Mahakama.
Wakili
huyo alisema wateja wake, wanaiomba Mahakama iamuru Kafulila awalipe Sh
bilioni 310 kama fidia, aombe radhi, alipe gharama za uendeshaji wa
kesi hiyo na amri nyingine, ambazo Mahakama itaona zinafaa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni