MAHAKAMA ya Rufani leo inatarajia kutoa uamuzi wa ama kulikubali au kulikataa ombi la marejeo lililowasilishwa na mwanamuziki wa dansi nchini, Nguza Vicking ‘Babu Seya’ na mwanae, Papi Kocha ‘Mtoto wa Mfalme’, ambao waliomba mahakama hiyo ifanyie marejeo hukumu ya kifungo cha maisha iliyoitoa Februari 2010, kwa kuwa ina dosari za kisheria na kuwaachia huru.
Kwa mujibu wa hati ya wito wa mahakama iliyotolewa kwa mawakili wa pande zote mbili, mahakama imemtaka Babu Seya na mwanae pamoja na mawakili wa pande zote kufika leo mahakamani ili wapokee uamuzi wa maombi hayo.
Oktoba 30 mwaka huu, jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Nataria Kimaro, Salum Massati na Mbarouk Mbarouk, walisikiliza ombi hilo lililowasilishwa mahakamani hapo na wakili wa waomba rufani, Mabere Marando.
Wakili Marando alidai kwa mujibu wa kanuni ya 66 ya Mahakama ya Rufaa ya mwaka 2009 inatoa mamlaka kwa Mahakama ya Rufaa kufanya mapitio ya hukumu inazozitoa, hivyo wateja wake wamewasilisha ombi hilo kwa sababu wanaamini mahakama ilikosea kisheria katika hukumu yake Februari 2010.
“Waheshimiwa majaji, kwa sababu jopo lenu katika hukumu yake lilikiri wazi wazi kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilikosea kurekodi ushahidi wa watoto waliodai walitendewa vibaya na waomba rufaa (Babu Seya na Papii) na sheria za nchi zinasema endapo mahakama itabaini kuwa mahakama ya chini ilikiuka taratibu za kurekodi ushahidi wa watoto wadogo, basi ushahidi ule wa watoto wadogo uliotumika katika mahakama ya chini kuwatia hatiani washitakiwa unafutwa na waomba rufaa au washitakiwa wanaachiwa.
“Nafahamu ni kazi ngumu kuwashawishi nyie majaji kubadili uamuzi wenu mlioutoa katika hukumu ya Februari 2010, ambapo uliwatia hatiani wateja wangu, ila kwa utetezi huo wa kisheria niliouainisha unaonyesha katika hukumu yenu mlikubaliana na hoja yangu kuwa Mahakama ya Kisutu ilikosea kurekodi ushahidi wa watoto wadogo, naamini mtatumia busara zenu na kufuata sheria na leo naiomba mahakama iwaachie huru wateja wangu,” alidai Marando.
Mawakili wa upande wa mjibu maombi (DPP), Angaza Mwipopo, Jackson Mlati, Imaculata Banzi na Joseph Pande, waliomba mahakama itupilie mbali ombi hilo, kwa kuwa sababu zote alizozitoa alizieleza wakati wa usikilizwaji wa rufaa na ziliamuliwa katika hukumu iliyotolewa na mahakama hiyo Februari mwaka 2010.
Jackson alidai kama Marando anaona hukumu ya mwaka 2010 ilikuwa na dosari, angeomba mahakama hiyo impangie jopo la majaji watano wa kusikiliza ombi na si ombi lake kusikilizwa na jopo la maji watatu wale wale waliotoa hukumu hiyo ambayo anadai ina dosari.
CHANZO: TANZANIA DAIMA
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni