Wakati
jamii ikiwa bado haijasahau mateso aliyoyapata mtoto Nasra Mvungi na
kusababisha kifo chake, tukio lingine la aina hiyo limetokea katika
Kijiji cha Matongola, Tarafa ya Magole Wilaya ya Kilosa, baada ya
kubainika mtoto wa miaka sita akiwa amefichwa uvunguni mwa kitanda na
kufanyiwa vitendo vya kikatili na mama yake mzazi.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonald Paulo alikiri kutokea kwa tukio
hilo na kusema kuwa taarifa za mateso ya mtoto huyo zilifikishwa Kituo
cha Polisi wilayani Kilosa saa za mchana jana, baada ya uongozi wa
kijiji na kata kutoa taarifa na tayari mwanamke huyo amekamatwa kwa
ajili ya mahojiano zaidi.
Mama
aliyefanya ukatili huo anafahamika kwa jina la Sala Mazengo ambaye
alimficha ndani mtoto wake aliyefahamika kwa jina la Devota Malole na
kumfanyia vitendo vya kikatili ikiwa pamoja na kutompa chakula, wala
kumfanyia usafi.
Baada
ya kufichuliwa kutoka alipofichwa, mtoto huyo alionekana kuwa dhaifu
kiafya kutokana na kukosa lishe pamoja na mazingira aliyokuwa akiishi
kutoridhisha, jambo ambalo ni kosa kisheria, pia ukiukwaji wa haki za
watoto.
Inadaiwa
kuwa tangu mwaka 2009 Sala amekuwa akimficha mtoto wake huyo ambaye
sasa amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kilosa kwa ajili ya kupatiwa
vipimo na matibabu.
Hata
hivyo, mwanamke huyo alipoulizwa alidai kuwa afya ya mtoto wake ilikuwa
mbaya tangu alipozaliwa kutokana na magonjwa ya mara kwa mara, pia hali
ngumu ya maisha ilichangia kudhoofisha afya ya mtoto huyo.
Alidai
kuwa ana watoto sita, pia alikiri kumlaza chini mtoto huyo kutokana na
kuwa na kitanda kimoja, ambacho hakiwatoshi watoto hao.
Aliongeza kuwa hata chakula amekuwa akikipata kwa shida kutokana na kushindwa kufanya kazi kwa kuwa ana mtoto mwingine mdogo.
Kamanda
Paulo alisema kuwa mwili wa mtoto huyo umedhoofu kutokana na kufichwa
ndani kwa muda mrefu na bado mwanamke huyo hajaeleza sababu za kufanya
vitendo vya ukatili dhidi ya mtoto huyo.
“Siwezi
kutoa taarifa ya kidaktari, lakini kutokana na afya ya mtoto yule na
mazingira tuliyomkuta ni dhahiri alikuwa akipata mateso na kufanyiwa
vitendo vya ukatili. Hata hivyo, uchunguzi zaidi tunaufanya na kwamba
taratibu za kumfikisha mtuhumiwa huyo Kituo Kikuu cha Polisi mkoani hapa
zinaendelea,” alisema Kamanda Paulo.
Alisema
kuwa mpaka sasa bado haijafahamika kama mtoto Davota ni mlemavu au la
na kwamba taarifa za afya ya mtoto huyo zitatolewa baada ya madaktari
kumfanyia uchunguzi wa kina.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni