NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA), Zitto Kabwe, amesema Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ni mzigo
katika serikali.
Amesema kuwa hii ni kutokana na kushindwa kufanya uamuzi mgumu katika
masuala yanayolihusu taifa licha ya baadhi ya mambo kuwa katika mamlaka
yake.
Zitto alisema kuwa hivi karibuni Pinda alishindwa kusimamia muswada wa
sheria ya marekebisho ya mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2013, hali
iliyosababisha kutokea vurugu bungeni.
Zitto ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Kaskazini, alitoa kauli hiyo juzi
wakati akihutubia mikutano ya hadhara katika kata ya Inyonga na
Songambele wilayani Mlele, mkoa wa Katavi, ikiwa ni siku ya kwanza ya
ziara ya kuimarisha chama Kanda ya Magharibi.
Alisema ni jambo la kusikitisha kuona Waziri Mkuu akishindwa kukutana
na kiongozi wa upinzani bungeni na kujadili masuala muhimu ya kitaifa
kabla ya Bunge kuanza kwa ajili ya mustakabali wa taifa.
Akitolea mfano masuala kadhaa ambayo Pinda ameshindwa kuyasimamia na
kumsubiri Rais Jakaya Mrisho Kikwete kuyafanyia uamuzi, Zitto alitaja
sakata la aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David
Jairo, na Yule wa Wizara ya Afya na sasa suala la kuhakikisha muafaka
unapatikana katika suala muhimu la Kikatiba.
“Kama tunaye Waziri Mkuu anayekaa bungeni na kushika tama wakati nchi
ikiwa katika hali ngumu ni tatizo. Huyu kila jambo anasubiri Rais atoke
UN kuja kufanya uamuzi ambao yeye angeweza kuusimamia. Basi tuna kazi ya
ziada katika kupata maendeleo,” alisema.
Zitto alifafanua kuwa mwanzoni alidhani Pinda anashindwa kusimamia
majukumu ya serikali kutokana na kukabiliwa na jitihada za kuboresha
miundombinu na maisha ya wakazi wa jimbo lake hali aliyoelezea kuwa ni
tofauti na aliyoikuta.
Alisema kutokana na hali hiyo ya Pinda kutokuwa na mamlaka, wakulima
wa Katavi wameendelea kununua mbolea kwa gharama ya juu licha ya
serikali kutenga kiasi cha bilioni 60 kwa mwaka kwa ajili ya ruzuku ya
mbolea kote nchini.
Alisema fedha hizo zinaliwa na wajanja huku serikali ikiendelea kuwa katika hali ya usingizi wa pono.
Tofauti ya CCM, CHADEMA
Akizungumzia sababu ya ziara yake katika kanda hiyo, Zitto alisema ni
kwa ajili ya kuhimiza mbegu ya ukombozi wa fikra na maendeleo kutoka
katika mikono ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
Alisema wakati CHADEMA inapambana katika kila kona kuhakikisha
udhalimu unaofanywa na serikali unaondoka, CCM inatumia kila njia
kuhakikisha inawanyonya wananchi.
“Tofauti kubwa kati ya vyama hivi ni kwamba CCM inaishi kwa kuwanyonya
wananchi na CHADEMA imesimama kidete kutaka udhalimu huo uondoke; na
kwa ajili hiyo chama hicho tawala kinatumia kila propaganda kuhakikisha
wananchi hawatuungi mkono,” alisema.
Kwa mujibu wa Zitto, kazi ya CHADEMA siku zote imekuwa ni kuwafumbua
macho wananchi juu ya unyonyaji unaofanywa na serikali ya CCM na
kuwataka waepukane na propaganda za kwamba kuiunga mkono CHADEMA ni
kukaribisha vita nchini.
Alisisitiza kuwa kwa sasa CHADEMA inajiandaa kushika dola mwaka 2015
na kwamba wanasimamia upatikanaji wa Katiba bora itakayowafanya
wanasiasa kuwa watumishi wa wananachi badala ya kuwa watawala.
“Mmetuona kwa uchache wetu bungeni tumeweza kufanya mambo makubwa kwa
nchi kila kashfa ya ufisadi mnayoisikia leo ni wabunge wa upinzani
wameibua na si wa chama tawala,” alisema.
-Tanzania daima
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni