Rais Jakaya Kikwete amesema maadui
wote ambao walitaka kupandikiza chuki miongoni mwa Watanzania kwa lengo
la kuvuruga amani ya nchi wamedhibitiwa .
Rais Kikwete alisema kuwa Serikali
yake itaendelea kulinda amani ya nchi na maadui wote wanaohusika na
kutaka kuvuruga nchi watachukuliwa hatua kali za kisheria. “Kulikuwapo
na upepo mbaya, lakini kwa sasa Tanzania ni shwari na tumemshinda adui,”
alisema Rais Kikwete jana kwenye Maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya
Kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere yaliyoandamana na sherehe
za kuzima Mwenge wa Uhuru, mkoani Iringa.
Alisema katika siku za hivi karibuni,
maadui wasioitakia mema Tanzania walikuwa na mkakati wa kuvuruga amani
ya nchi, lakini Serikali kwa kushirikiana na vyombo vya dola
vimewadhibiti na nchi iko salama.
Rais Kikwete alisema kuwa Serikali
haiwezi kuvumilia vitendo vya uvunjifu wa amani kwa sababu inajua wazi
kwamba nchi ikiingia kwenye mgawanyiko, mshikamano utavurugika na
shughuli za maendeleo zitasimama.
Katiba Mpya
Rais Kikwete alisema mwaka 2014 ni mwaka wa kipekee kwa nchi kwa kuwa utakuwa na mambo makubwa matatu yatakayofanywa.
Rais Kikwete alisisitiza kwamba Katiba Mpya ni lazima ikamilike mwakani kama mambo yatakwenda kama ilivyopangwa.
Vilevile, alisema mwakani Tanzania
itasherehekea miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyoondoa udhalimu na
kuwarudishia Wazanzibari heshima ya mwanadamu na utu wake.
“Pia tutasherehekea miaka 50 ya
Muungano wetu. Nawaomba Watanzania wajiandae kuyafanikisha vizuri mambo
hayo ili historia mpya ifunguliwe nchini.
“Wazanzibari waanze miaka mingine
baada ya miaka hamsini ya uhuru wao, muungano uanze miaka mingine baada
ya miaka hamsini na Katiba Mpya itupeleke miaka mingine tukiwa wamoja,”
alisema Kikwete.
Rais Kikwete alionya kuwa asingependa
mchakato wa kupata Katiba Mpya uligawe taifa na kuleta mfarakano
utakaovunja umoja wa kitaifa badala ya kuuimarisha.
“Tunataka tuwe na Katiba itakayojenga, siyo kubomoa, kutugawa kwa misingi ya kiitikadi,” alionya Rais Kikwete.
-Mwananchi
Mtete Focus Blog
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni