Mwanasiasa na kada mkongwe wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM), Peter Kisumo ameonya kuwa chama hicho kinaweza
kuondolewa madarakani kutokana na kunyamazia vitendo vya ufisadi na
matumizi mabaya ya rasilimali za umma vinavyotokea nchini.
Mzee Kisumo alitoa onyo hilo wiki
iliyopita katika mazungumzo maalumu aliyofanya na Mwananchi nyumbani
kwake Dar es Salaam kuhusu kumbukumbu ya miaka 14 ya kifo cha Mwalimu
Julius Nyerere inayoadhimishwa leo.
Alisema tatizo kubwa la chama hicho
ni kwamba kimemeendelea kuwa chama dola kikikaa mbali na wananchi, huku
kikishindwa kuidhibiti rushwa na kuwajibisha wahusika wa vitendo hivyo.
“Chama kimebaki kuwa cha
walalamikaji, kila mtu amekuwa mlalamikaji. Hata Waziri Mkuu amegeuka
mlalamikaji. Sijaona watu wanaowajibishwa kwa ufisadi,” alisema Kisumo
na kuongeza:
“CCM haiwezi kujivunia ufisadi
unaoonekana nchini. Siwezi kusema imeukumbatia, lakini nasema imekuwa
CCM bubu, hata kuukemea ufisadi haiwezi. Utamaduni huu enzi za Mwalimu
Nyerere haukuwapo.”
Alisema kutokana na udhaifu huo wa
CCM, kuna uwezekano mkubwa wa chama cha upinzani, na hasa Chadema
kutumia mwanya huo kuwashawishi wananchi na kushinda uchaguzi.
Kisumo ambaye alikuwa Mwenyekiti wa
Bodi ya Wadhamini wa CCM, alisema ingawa Chadema haijaonyesha wazi mambo
kinayoyapigania, kinaweza kutumia agenda ya ufisadi na matumizi mabaya
ya rasilimali za umma kuwavutia wananchi na kuchaguliwa.
Alitoa mfano wa tuhuma za baadhi ya
viongozi wa Serikali kuficha mabilioni ya shilingi kwenye benki za
Uswisi, kuwa zinaweza kuwa kete muhimu ya kuwaingiza Chadema madarakani,
iwapo Serikali ya sasa haitawashughulikia wahusika.
“Wakijitokeza na kuwataja majina
wahusika, wakasema fulani na fulani ndiyo wenye mabilioni haya Uswisi,
na Serikali ikasita kuwachukilia hatua, wakasema tukiingia madarakani
tutawakamata, wananchi wanaweza kuwaamini na kuwachagua,” alisema na
kuongeza: “Wakishinda uchaguzi hata kwa viti vichache tu, watakosa nguvu
bungeni, lakini kwa wananchi watakuwa na nguvu sana.
Hii inaweza kuwasaidia kwa miaka
mitano ya kwanza. Wanaweza kupata ushindi mkubwa zaidi kwa mara ya pili
na wakiingia madarakani watawafunga viongozi wa zamani kweli.”
Mzee Kisumo anasistiza, “Hili
linawezekana. Anayesema uwezekano wa CCM kushindwa haupo, anajikana
mwenyewe. CCM inabidi ijihami na majibu ya jinsi inavyotumia rasilimali
za nchi.”
Alionya kuwa si vizuri kuishia
kujinadi kwa mambo mengi mazuri iliyofanya huko nyuma, akitolea mfano
kuwa hiyo ni sawa na nguo nyeupe ambao ikiingia doa moja tu inakuwa
haitamaniki tena.
_Mwananchi
Mtete Focus Blog
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni