Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe, amesema anatarajia Katiba Mpya itabainisha umri wa msichana kuolewa ni miaka 18 na kuondoa utata wa kisheria na kukomesha ndoa za utotoni.
Aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam
katika kikao cha wadau mbalimbali kujadili namna ya kukomesha ndoa za
utotoni ikiwa sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa
Kike Duniani.
Waziri Chikawe alisema kwa sasa kuna
mkanganyiko wa Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 inayobainisha kuwa mwanamke
na mwanaume wawe wametimiza umri wa miaka 18 ili wafunge ndoa, hata
hivyo mwanamke anaweza kuolewa akiwa na umri wa chini ya miaka18 lakini
siyo chini ya miaka 15 kama atapata idhini ya wazazi au kama wote
wamefariki idhini itatolewa na mlezi wa binti huyo.
“Kisheria mtoto mwenye umri chini ya miaka
18 hawezi kuingia kwenye mkataba. Na Sheria ya Makosa ya Kujamiiana ya
mwaka 1998 (SOSPA) inatamka wazi kuwa mwanamume atajayejamiiana na
msichana mwenye umri chini ya miaka 18 hata kama ameridhia ni mbakaji na
atahukumiwa kwa mujibu wa sheria.Huu ni mgongano wa kisheria,”alisema.
Alisema hatua hiyo itasaidia kujenga
mazingira mazuri ya kukomesha ndoa za utotoni na kuwapa fursa wasichana
kukua vyema na kupata elimu ambayo ni haki yao ya msingi.
Mkurugenzi wa Chama cha Wanahabari
Wanawake Tanzania (Tamwa),Valerie Msoka alisema anatiwa moyo na hatua
hiyo ya serikali, lakini akatoa angalizo kwamba kuwa na sheria nzuri ni
jambo na utekelezaji ni jambo jingine “tunataka kuona utekelezaji wa
vitendo ili kuwanusuru wasichana na ndoa za utotoni,” alisema.
Mke wa Rais wa Afrika Kusini, Graca
Machel, katika ujumbe wake kwa nijia ya video alisema ni muhimu
kukaimarisha usajili wa ndoa na vifo vya wasichana wadogo ili ukubwa wa
tatizo lifahamike na kuhakikisha kuwa watoto wanapata fursa ya elimu,
kuondoa umaskini na haja ya kukomesha ndoa za utotoni.
Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye kiwang
cha juu cha ndoa za utotoni duniani na inakadiriwa kuwa wasichana
wawili wa Tanzania kati ya watano watakuwa wameolewa kabla ya
kufikisha umri wa miaka 18.Kiwango hiki cha juu kinachangia kukwamisha
wasichana kupata elimu, kupata mimba na kuhatarisha maisha yao kutokana
na matatizo ya afya ya uzazi.
Mtete Focus Blog
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni