CHUO
Kikuu cha Dodoma (UDOM), kimeshindwa kudahili wanafunzi wa kutosha
kutokana na wahitimu kutokuwa na vigezo. Malengo ya kuanzishwa kwa chuo
hicho ni kudahili wanafunzi 40,000 ifikapo mwaka 2015 lakini hadi sasa
idadi ya wanafunzi waliopo hawazidi 15,000.
Taarifa
hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Chuo
hicho, Profesa Idris Kikula wakati wa uzinduzi wa baraza la pili la
wafanyakazi la chuo hicho.
Profesa Kikula alisema idadi ya
wanafunzi wanaodahiliwa chuoni hapo inaendelea kushuka siku hadi siku
ikilinganishwa na nafasi zilizopo.
"Changamoto zinazotukabili ni
nyingi lakini za msingi ni idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa imendeelea
kushuka mwaka hadi mwaka kutokana na ukosefu wa wahitimu wa kutosha
wenye vigezo vya kudahiliwa katika kozi zetu.
"Changamoto
nyingine ni ufinyu wa bajeti unaotokana na vyanzo vichache vya mapato ya
chuo na pia ufinyu wa ruzuku ya Serikali ndiyo vinakwamisha chuo
kufikia malengo yake kama ilivyotarajiwa awali," alisema.
Alisema
katika kukabiliana na changamoto ya kuongeza udahili, chuo kimeanzisha
programu za cheti na stashahada kuanzia mwaka huu wa masomo.
Alisema
kwa sasa Chuo hicho kina wanafunzi 13,376 wa shahada za awali,
wanafunzi 1,403 wa shahada ya uzamili, wafanyakazi 1,181 na wataalamu 66
kutoka nje. |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni