Akitoa taarifa ya Mkutano Mkuu wa chama hicho
uliofanyika jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa
Chadema, John Mnyika aliwataja waliopendekezwa kuwa ni Profesa Abdallah
Safari, Mabere Marando, Nasra Juma Burhan na Method Kimomogoro.
Miongoni mwa hayo yatateuliwa majina ya watakaokuwa Wabunge wa Bunge Maalumu la Katiba linalotarajiwa kuanza mapema mwezi ujao.
Desemba 13 mwaka jana Rais Kikwete alivitaka vyama
vya siasa na wadau wengine kupeleka ofisini kwake majina yasiyopungua
manne au kuzidi tisa kwa ajili ya kupata majina 201 yanayohitajika
kuteuliwa kuingia kwenye Bunge Maalumu la Katiba.
Akitoa ufafanuzi kuhusu majina yaliyopelekwa na
Chadema, Mnyika alisema kuwa walioteuliwa wana sifa zilizopendekezwa
kuangaliwa wakati uteuzi huo.
“Marando huyu ni msomi mwenye Digrii ya Sheria na
ni wakili wa Mahakama Kuu, Kimomogoro ni msomi wa sheria na ni Wakili wa
Mahakama Kuu, Profesa Safari ni msomi mwenye Shahada ya Uzamivu
aliyebobea kwenye mambo ya sheria, vilevile ni Wakili wa Mahakama Kuu na
mama Burhani ni mwalimu kwa taaluma,” alisema Mnyika.
Alibainisha kuwa Kamati Kuu ya Chadema imeazimia
kupita nchi nzima kuchukua saini na majina ya wananchi wote walio na
sifa za kupiga kura, lakini majina yao hayamo kwenye Daftari la Kudumu
la Wapigakura.
Aliongeza kuwa uamuzi huo umefikiwa baada ya Tume
ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), kutangaza kuwa haitalifanyia marekebisho
Daftari la Wapigakura kabla ya upigaji kura ya maoni.
“Chama kimekusudia kukusanya orodha na saini za
wananchi ambao wataathirika na hatua hii ya tume na Serikali kuacha
kuboresha Daftari la Kudumu la Wapigakura,” alisema na kuongeza:
“Tutakusanya saini za wananchi ambao ama ndiyo
wamefikia umri wa kujiandikisha au walipoteza kadi na hawana utambulisho
mwingine na walitaka kujiandikisha kwenye daftari hilo au walihama
makazi na walioathirika na suala la ukazi hasa kwa Zanzibar. Tutaanza
kazi hiyo ili kuishinikiza Nec na Serikali kuboresha daftari hilo kabla
ya kura ya maoni.”
Mnyika alisema kwamba taarifa hizo za wananchi
zitapatikana kupitia maandamano, programu ya Chadema ni msingi,
Operesheni za M4C kwa mujibu wa utaratibu ambao chama kitaeleza baadaye.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni