.

Jumapili, 5 Januari 2014

GIZA NENE LATANDA NDANI YA CHAMA CHA CHADEMA


Giza nene limeendelea kutanda ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), baada ya juzi kulazimika kuongeza muda wa kikao cha Kamati Kuu kusubiri uamuzi wa Mahakama Kuu kuhusu aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wake Zitto Kabwe.

Kikao hicho kiliendelea jana kikimhoji aliyekuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho, Dk Kitila Mkumbo, huku taarifa nyingine zikieleza kuwa Zitto Kabwe ameendelea na msimamo wake akituhumu chama hicho kuongozwa kwa ubabe.

Habari kutoka ndani ya kikao hicho kinachofanyika Hoteli ya Mbezi Garden jijini Dar es Salaam zinaeleza kuwa mkutano huo ulianza saa 4:00 asubuhi kwa kujadili ajenda zilizoshindwa kujadiliwa juzi, ambapo Dk Kitila alianza kuhojiwa saa 7:00 mchana.

Hata hivyo, taarifa hizo zinaeleza kuwa baada ya Dk Kitila kuingia kuhojiwa, aliwaomba  wajumbe amwite mwanasheria wake, ambaye anazifahamu vyema taratibu na sheria za chama ili amsaidie kujibu hoja.

Kazi hiyo ya Dk Kitila kutafuta mwanasheria ilichukua muda mrefu na akapatikana saa 11;00 jioni ndipo kikao kilipoanza.

Hata hivyo, kabla ya kuingia katika ukumbi huo wa mkutano, Dk Kitila aliliambia gazeti hili kuwa atatoa ufafanuzi wa msimamo wake baada ya kutoka ndani ya kikao hicho.

Hata hivyo, hadi saa 1:00 jioni jana alikuwa bado ndani ya chumba cha mkutano akihojiwa, huku taarifa zaidi zikieleza kuwa wajumbe wengi walikuwa wakimsihi Dk Kitila aombe radhi ili asamehewe, yaishe.

Baada ya kumaliza kuhojiwa saa 1:40 usiku, Dk Kitila alimwambia mwandishi  amemaliza kazi yake na anauachia uongozi kutoa uamuzi wake.

Mnyika

Awali akitoa taarifa ya kikao hicho, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa chama hicho, John Mnyika alisema kuwa Kamati Kuu ilishindwa kuwahoji Dk Kitila na aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba baada ya kuondoka mapema eneo la mkutano bila ya kuaga na kuzima simu zao. Alisema kwa sababu Chadema ni chama kinachoamini katika demokrasia, waliamua kuwatafuta kwa namna nyingine na kufanikiwa kuwapata jana asubuhi.

Mnyika alisema kuwa kama mmoja wa watu hao hatafika kuhojiwa mbele ya Kamati Kuu, basi chama kitachukua uamuzi kitakachoona unafaa dhidi yake.

Mjumbe wa Kamati Kuu apigwa

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Shaaban Mwamba, juzi usiku alipata kipigo kutoka kwa maofisa wa  kikundi cha ulinzi cha chama hicho waliokuwa katika eneo ambalo mkutano wa Kamati Kuu ulifanyika, baada ya kutuhumiwa alikuwa akiwasiliana na wafuasi wa Zitto.

Taarifa kutoka kwa mjumbe mmoja ambaye hakupenda jina lake litajwe gazetini, ilisema kuwa mtu huyo alikuwa akichunguzwa na maofisa wa ulinzi wa chama hicho muda mrefu, kutokana na nyendo alizokuwa akizionyesha zilizotia shaka.

Mwandishi wa habari hizi ambaye alikuwa katika eneo hilo, alishuhudia kiongozi huyo akibebwa juu juu na maofisa hao, huku akiulizwa aliyekuwa akiwasiliana naye ni nani, kabla ya vijana wengine wa chama kumkamata na kumweka chini ya ulinzi, wakimtaka atoe ufafanuzi wa alichokuwa anakifanya.

Baada ya mahojiano ya muda mfupi, kiongozi huyo alionekana akiinuka na kwenda  kunawa kwenye bomba la maji, huku akitokwa damu mdomoni.

Taarifa zilizopatikana baadaye zilidai kuwa kiongozi huyo alikuwa akiwasiliana na mama yake Zitto na Katibu wa Zitto, Dk Alex na kwamba pia simu yake ilikutwa na ujumbe mfupi aliokuwa amewaandikia watu hao.

Gazeti hili lilijaribu kumtafuta kiongozi huyo ili kueleza sababu ya kupigwa kwake, lakini hakupatikana eneo la mkutano kwa madai kuwa alikwenda hospitali kupata huduma ya kwanza, lakini hakurudi.

Wakati suala la Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe na uongozi wa chama chake likiendelea kuwasumbua vichwa wapenzi wa chama hicho, inadaiwa kuwa baadhi wa wabunge, viongozi na wazee wa Chadema, wanataka suala hilo liishe mapema.

Habari ambazo gazeti hili lilizipata jana, zilisema kuwa baadhi ya viongozi hao walitaka Zitto aende Halmashauri Kuu ya Chadema na kuomba msamaha ili mambo yaishe.

“Walimfuata Kitila (Dk Kitila Mkumbo) wakamwambia amshawishi Zitto ili mambo yaishe nje ya mahakama, wanataka aende kwenye Halmashauri Kuu kuomba radhi. Kitila akawaambia kuomba radhi kwa kosa gani?” kiilisema chanzo hicho.

Zitto azungumza

Hata hivyo, Zitto aliliambia gazeti hili jana kuwa kumekuwa na jitihada  mbalimbali za wazee kutaka kukiepusha chama hicho na migogoro na kuwa amekuwa tayari kwa suala hilo. “Wazee walikuwa na wajibu wa kuhakikisha hatufiki hapa tulipofika. Sijui kama fursa hiyo bado ipo,” alisema Zitto.

Kuhusu uamuzi wake wa kwenda mahakamani alisema: “Nimekwenda mahakamani kutaka haki itendeke. Chama cha kidemokrasia kinanyima vipi mwanachama fursa ya kukata rufaa?

“Nisingekwenda mahakamani kama ningeona haki ikitendeka. Tatizo kubwa la chama chetu sasa kinaongozwa na mawazo ya kihuni na yeyote mwenye mawazo ya kujenga anaonekana msaliti.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni