Balozi Msuya alitoa kauli hiyo jana katika misa ya maombi iliyofanyika nyumbani kwa marehemu, Mikocheni jijini Dar es Salaam, muda mfupi baada ya mwili wake kupokelewa kutoka nchini Afrika Kusini.
Alisema kifo cha Dk. Mgimwa ni cha kawaida na hakina utata na kwamba uvumi unaoenezwa kuwa amelishwa sumu si wa kweli.
“Hakuna utata amekufa kwa ‘Natural Causes’ ni kutokana na viungo vya mwili kufikia mwisho,” alisema Balozi Msuya ambaye aliongoza msafara ulioleta mwili wa marehemu Mgimwa kutoka Afrika Kusini.
Kuwasili mwili
Awali ndege iliyobeba mwili wa Dk. Mgimwa iliwasili saa 7:48 mchana kutoka Afrika Kusini na kuingizwa ndani ya Uwanja wa Julius Nyerere (VIP) na kubebwa kwa gari namba T 183 BMV mali ya Kampuni ya mizigo ya Swiss port.
Mara baada ya kuwasili mwili huo sambamba na mke wa marehemu, Jonisia Mgimwa akiambatana na kaka wa marehemu, Joachim Mgimwa, walilakiwa na baadhi ya Mawaziri wakiongozwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba.
Baadaye mwili ulipelekwa lango kuu la wanaowasili ambako ulipokelewa na askari wa Bunge pamoja na mawaziri mbalimbali.
Viongozi walioupokea mwili
Waziri asiyekuwa na Wizara maalumu, Mark Mwandosya, Waziri wa Ujenzi John Magufuli, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge, Willium Lukuvi ambaye pia ndiye kiongozi wa Kamati ya maandalizi ya msiba huo, Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta aliyeambatana na mkewe Magreth, Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe na Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk. Makongoro Mahanga.
Wengine waliofika uwanjani hapo ni Manaibu waziri wake wawili, Janeth Mbene na Saada Mkuya Salum, ambao muda wote walionekana kububujikwa na machozi.
Wengine ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe na Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba.
Wakizungumza mara baada ya kuupokea mwili wa marehemu, Waziri Magufuli alisema aliongea na Dk. Mgimwa wiki moja kabla ya kukumbwa na mauti akiwa hospitalini alikolazwa.
Magufuli alisema nchi imepoteza kiongozi mwenye heshima na upendo na kwamba akiwa huko walizungumza mengi na kuahidi kuja kushughulikia madeni ya wakandarasi lakini Mungu alimpenda zaidi.
Naye, Waziri Chikawe alisema, Dk. Mgimwa atamkumbuka kwa mengi kutokana na kwamba alikuwa akikaa kiti cha upande wa kulia kwake katika safu ya Mawaziri bungeni.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dk. Mahadhi Juma Maalim alimwelezea marehemu kuwa alikuwa mtu makini ambaye aliweza kuongoza sekta ngumu ya fedha kutokana na kuwa mkweli, hata kama jambo likishindikana alitoa sababu ya kwanini limekwama.
Naye, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe alisema amejifunza unyenyekevu kwani marehemu alimsikiliza kila mtu na ndicho kilisababisha kufanya kazi pamoja kwa ukaribu wakati akiwa Waziri wa Fedha na yeye akiwa Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi ndani ya chama hicho.
Jeneza lenye mwili wa marehemu lilipakiwa kwenye gari ndogo ya kubebea maiti, kwa ajili ya kuelekea nyumbani kwake Mikocheni B.
Nyumbani kwa marehemu
Mara baada ya kuwasili mwili wa marehemu, vilio vilitawala kwa ndugu na jamaa waliokuwa nyumbani hapo, ambao walionekana kushikwa na huzuni kubwa.
Misa ya maombi kwa ajili ya marehemu iliongozwa na mapadri wawili wa Kanisa Katoliki, ambao ni Luciano Mpona na Leonard Maliva.
Katika maombi hayo, Padre Maliva alisoma Zaburi ya 112:6 inayosema mwenye haki atakumbukwa milele.
Pia alisema thamani ya mwanadanu ni kubwa na kwamba katika ukimya wa Dk. Mgimwa, unaelezea kutenda haki kwa wengine pamoja na kuishi kwa kumtegemea Mungu.
Mdogo wa marehemu, Joachim Mgimwa aliyekuwa akimuuguza nchini Afrika Kusini, alisema kaka yake kabla hajaaga dunia alimshukuru Rais Jakaya Kikwete kwa kufika kumjulia hali mara mbili hospitalini hapo.
Marehemu Dk. Mgimwa ambaye anatarajia kuagwa rasmi leo kabla ya kusafirishwa mkoani Iringa, ameacha mjane na watoto watano.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni