Ziara hiyo inaanzia katika mikoa ya Tanga, Mwanza na Ruvuma, huku
viongozi wa chama hicho wakijigawa katika makundi sita; matatu yakitumia
helkopta na matatu yatawafikia wananchi kwa kutumia usafiri wa magari.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema jana jijini Dar es
Salaam kuwa, lengo la operesheni hiyo ni kukiimarisha chama hicho na
kuwafumbua macho wananchi kuhusu mchakato wa Katiba Mpya.
“Tumejigawa katika makundi sita na makundi matatu kati ya hayo yatatumia helikopta kila moja, makundi mengine yatawafikia wananchi kwa misafara ya ardhini,” alisema Mbowe na kuongeza;
“Viongozi wakuu wa chama, wabunge, wenyeviti wa mikoa, wilaya, majimbo na kanda kila mmoja atashiriki kwa nafasi yake katika operesheni hii. Tutafanya mikutano kwa wiki mbili, ila tunaweza kuongeza wiki nyingine moja.”
Alisema chama hicho kimejipanga kuwafikia wananchi wengi kadri
itakavyowezekana, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya uchaguzi wake wa
ndani kuanzia ngazi ya mashina, uchaguzi mdogo wa madiwani katika Kata
27 nchini utakaofanyika Februari 9, mwaka huu pamoja na Uchaguzi wa
Serikali za Mitaa.
“Naomba tueleweke, katika hili hatufanyi kampeni hata kidogo, huu ni
mwendelezo wa maandalizi ya chaguzi mbalimbali. Kama mnakumbuka tulianza
kujiandaa na uchaguzi wa mwaka 2015 baada ya kumalizika kwa Uchaguzi
Mkuu wa 2010,” alisema Mbowe na kuongeza;
“Kwa sasa tunachokifanya ni kuongeza nguvu na umakini zaidi. Makundi yataanzia katika mikoa ya Tanga, Mwanza na Ruvuma, tutapita kila Kata ambazo utafanyika uchaguzi wa madiwani.”
Mbowe alisema operesheni hiyo itapiga kambi katika Jimbo la Kalenga
ambalo kwa sasa lipo wazi baada ya mbunge wake ambaye pia alikuwa Waziri
wa Fedha na Uchumi, Dk William Mgimwa kufariki dunia Januari 1, mwaka
huu nchini Afrika Kusini.
“Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) haijatangaza kufanyika uchaguzi katika jimbo hilo, Chadema tutafika Kalenga na tutafanya mkutano maalumu na kutoa pole kwa wakazi wa jimbo hilo kutokana na msiba mkubwa wa mbunge wao,” alisema Mbowe.
Operesheni hiyo inafanyika siku chache tangu chama hicho kikuu cha
upinzani nchini kipite katika mgogoro ambao ulisababisha aliyekuwa Naibu
Katibu Mkuu wake, Zitto Kabwe kukimbilia mahakamani ili kunusuru
uanachama wake.
Wakati Zitto akinusurika kufukuzwa kutokana na zuio la mahakama,
aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoani Arusha, Samson Mwigamba na Mjumbe
wa Kamati Kuu, Dk Kitila Mkumbo walifukuzwa uanachama, likiwa ni
hitimisho la mchakato ulioanza kwa kuwavua nyadhifa zao pamoja na Zitto.
SOURCE: Mwananchi
SOURCE: Mwananchi
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni