.

Jumamosi, 5 Oktoba 2013

HAYA HUWAFANYA WANAWAKE KUSITA KUINGIA KATIKA NDOA (KUOLEWA)


Pamoja na kuwa kuna wanawake husita kuolewa, lakini jambo hili si kubwa sana kwa wanawake kama ilivyo kwa wanaume. Kwa kiasi kikubwa katika suala la kutaka kuingia ndani ya ndoa, wanawake ni wengi ambao hutaka kufunga ndoa kuliko ilivyo kwa wanaume. Hilo tunaliona wazi tokana na shamra shamra awazo nazo mwanamke wakati wa maandalizi ya shughuli za Ndoa na Harusi.

Hata hivyo, kwa wale wanawake wachache ambao husuasua kuolewa hizi ni baadhi ya sababu zinazopelekea kusuasua huko. (Izingatiwe hii ni kwa wanawake ambao hawajawahi kuolewa kabisa)
 

Vigezo vilivyopitiliza viwango (hasa kwa muonekano)
 
Wanawake wengi hasa wa umri mdogo (lakini unatosha kuolewa) hutumia muda mwingi katika kuchagua aina ya mwanaume ambaye angependa awe mume wake. Wanawake hawa hujiamini zaidi na kusimamia sifa zile ambazo huamini ni muhimu mwanaume wa kumuoa awe nazo.  Vigezo hivyo huwa hata kwa misingi ya muonekano wa mwanaume huyo – kuna wale ambao hutaka mwanaume huyo wa kumuoa awe na sifa kama vile, mrefu, aliyejazia kifua, mtanashati, sauti nzuri n.k. Inaweza kuwa kama mzaha na ikaonekana ni kipengele kidogo sana lakini bado kuna wale ambao anaweza kuwa tayari kuolewa ila hataki sababu tu huyo mwanaume hafananii vile ambavyo yeye anataka mumewe awe.
 

Kutaka mwanaume tajiri
 
Kuna wanawake ambao tayari wameshajiwekea akilini kuwa hatakubali kuolewa na mwanaume yeyote yule ambaye hana pesa nyingi. Yupo tayari kuolewa ila si kwa mwanaume mwenye uwezo wa kawaida – hata ikitokea mwanaume ana uwezo kidogo wa kuweza kujitosheleza, yeye bado huona huyo mwanaume hamfai hadi pale tu atakapo pata yule ambaye anahisi ataishi maisha ya kifahari. Hivyo hukazana kusubiri na kujitahidi kuwinda aina ya mwanaume ambaye atakuwa na uwezo mkubwa, bila kujalisha kama huyo mwanaume kampita sana umri.
 

Kutompata Mwanaume Ampendae
 
Hili ni kama tu vile ilivyo kwa wanaume ambao huamini ndoa haiwezekani na haifai bali tu hadi pale umpatapo yule ambaye unampenda na unaamini anakupenda pia.  Wengi katika kundi hili huamini kuwa mafanikio ya ndoa kigezo kikubwa ni kupendana tu na mengine hufuata kwenye sababu ya upendo. Kuna wanawake vigezo vya mwanamme awe vipi havina umuhimu kabisa katika kutaka kuamua kuolewa. Yeye kikubwa anataka ampate mume ambaye atampenda kwa dhati na huku akiwa na matumaini kuwa huyo mume atampenda na yeye pia kwa dhati.  Huyu mwanamke anaamini msingi bora wa ndoa ni mapenzi ya dhati kati ya yeye na mmewe basi! Hana haraka hadi pale atakapompata mwanaume akampenda ndipo atakapokuwa tayari kuolewa.  
 

Kuchagua mno Wanaume wa Kumuoa
 
Kuna wale wachache ambao akili hubadilika kama kinyonga; wasioridhika wala kujitambua ni nini wanataka ama mwanaume wa aina ipi wanataka. Akija wa mwenye uwezo atasema nataka wa kuchuma nae, akija asiye na uwezo atatoa sababu tu hata kama kumlaumu kuwa inaonyesha hajitumi kutafuta maendeleo. Akija wa kabila hii, atasema hapana hao wana tabia hii mimi siitaki! Yaani kwa ufupi ni mtu asiyeisha kutoa kasoro za wale ambao wanajitokeza kutaka kumuoa. Hatimaye inaweza tokea muda wa kuolewa ukapita na akaishia kupunguza uchunguzaji lakini ikiwa hata wanaume wa umri wa kufaa kumuoa kutokuwepo tena katika soko.
 

Kujiona ni mzuri sana
 
Kuna wanawake ambao ni kweli Mwenyezi Mungu kawajaalia uzuri hasa (uzuri wa muonekano), anakuwa ni mzuri kiasi kwamba wake kwa waume wote wanamkubali kwa uzuri huo na hata wote kumtamani. Hata hivyo hapo hapo kuna wale ambao huwa ni wazuri kawaida – ila kwa mtazamo wake hujiona ni mzuri mno hakuna mfano kama yeye; kitendo ambacho kwa wachache kwenye kundi hili hufanya kujiona yeye ni yeye na kuwa kwa yeyote kuwa na yeye huyo mtu anatakiwa atambue kuwa ana bahati sana. Kitendo hiki hukuza nyodo za hali ya juu ya mwanamke mwenye mtazamo huu, kiasi kwamba wanapojitokeza wanaume kutaka kuoa – anaweza onyesha tabia kama maringo, dharau na kiburi.
 

Kujiona ana Umri mdogo
 
Binti yeyote wa miaka 18 na kuendelea anaruhusiwa kuolewa endapo tu karidhia kuolewa. Wanawake wametofautiana mipangilio yao ya kimaisha, kuna wale akiwa katika umri wa kuolewa hutamani sana kuolewa na kuna wale ambao hupenda kuolewa wakiwa wakubwa zaidi. Katika kundi hili umri kuwa mdogo hutegemeana, kuna mwingine anakuwa na umri wa miaka 25 na bado akajiona mdogo na hali kuna mwingine anakuwa na miaka 20 na akajiona ni mkubwa na anafaa kuolewa. Hii pia ni kwa wanawake wale ambao huwa na malengo ya kutotaka kuharakisha katika ndoa. Anapokuwa na umri ambao anaweza kuolewa lakini yeye hayupo tayari kwa muda huo, huwa ni kikwazo kwake kuingia katika ndoa.
 

Maradhi hasa UKIMWI
 
Hili kama lilivyo kwa wanaume -  Pamoja na kuhamasishwa kwingi na wataalamu wa maradhi ya HIV/AIDS kuwa mtu hata ukiwa umeathirika unaweza kuwa na mahusiano na hata kuoa na kuwa na watoto; bado haisaidii sana kwa vijana wanaojitambua kuwa ni waathirika wakiwa bado ni wadogo, hawajaoa/olewa ama kuwahi kuwa na mtoto.  Wengi sana hukata tamaa na huona ni kheri kubaki walivyo kuliko kuingia katika ndoa, hasa tokana na imani kuwa wanawake wakizaa wakati ni waathirika; afya hudhoofika zaidi.
 

Kutaka maisha ya Tamthilia (Ndoa za kuishi kwa furaha milele)
 
Kutokana na kukua kwa idadi ya tamthilia nyingi ambazo huonyesha maisha ya kimagharibi zaidi; kumekuwa na dhana kwa baadhi ya wanawake kutaka hayo maisha ya tamthilia yawe na kwao pia. Hilo linafanya vigezo ambavyo mwanamke huyo anatumia kuchagua ama kukubali mwanaume kumuoa kutotimiza yale ambayo yeye binafsi anatarajia.  Wengi hushindwa kutambua kuwa hakuna maisha ya furaha milele, na hasa kuwa maisha ya maigizo yapaswa kuchanganya na zako kuweza kufanya maamuzi ya kipi kiigwe na kipi kiachwe kama kilivyo.
 

Kuona taasisi ya Ndoa kama Utumwa
 
Mtazamo huu kwa wanawake wenye msimamo huu, huchangiwa na baadhi kama haya:
 
- Usomi: Aina ya usomi ambao hupelekea kwa baadhi kuwa na tafsiri tofauti juu ya ndoa, haki, majukumu na mengine mengi.
 
- Kushuhudia ndoa mbovu: Hii inaweza kuwa ya wazazi/walezi wake wenyewe (pengine mama aliteswa sana), na hata ndugu wa karibu kama vile kushuhudia kila ndoa ya ndugu yake anayoijua mwanamke huishi kwa mateso, manyanyaso na maisha ya taabu na kuonewa.
 
- Kuwa na uwezo sana wa kujitosheleza ambao unaweza kumtimizia na kufanya lolote lile ambalo anataka katika maisha. Kwake kuwa na mwanaume kama mume kwake anaona kama ni utumwa.
 

Kutokuwa kabisa na mshipa wa hisia za kufanya mapenzi
 
Kuna wanawake wale wachache waliozaliwa hivyo. Hawana hisia yoyote ile ya kimwili ya kuweza kupata hisia za kuweza kujisikia ama kutamani kufanya mapenzi. Wengi wa aina hii ya wanawake huwa ni waoga sana wa kuwa karibu na mwanaume, na kwa wale ambao wamewahi hata jaribu baadhi huona kama kitendo cha ndoa ni kero, unyanyasaji na uchafu.  Hivyo wazo la kuwa akiolewa anatarajia kufanya kitendo cha ndoa mara kwa mara kinamvunja kabisa hamu ya kutaka kuolewa.
 


Source:Fikrapevu.com

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni