.

Jumapili, 29 Desemba 2013

Watu watano wachomwa moto na wananchi wenye hasira kwa madai ya kuiba mchango wa rambirambi ya Sh. 65,000 msibani




Watu watano wamekufa kwa kuchomwa moto na wananchi wenye hasira kwa madai ya  kuiba mchango wa rambirambi Sh. 65,000.

Tukio hilo la kusikitisha lilitokea jana saa 7.30 mchana baada ya watuhumiwa kushambuliwa wakiwa mikononi mwa walinzi wa jadi (sungusungu).

Watu hao walidaiwa kuiba mchango huo juzi usiku nyumbani kwa  John Ibarabara. Chanzo cha tukio hilo kinadai kuwa  watuhumiwa hao walivamia nyumbani kwa mfiwa siku moja baada ya wanandugu na wanajamii kutawanyika wakiwemo watuhumiwa na ilipofika usiku walirudi nyumbani kwa mfiwa na kuvunja mlango na kutaka wapatiwe fedha ya rambirambi.

Habari zaidi zimedai kuwa watuhumiwa walimkuta mtoto na kumpiga makofi kisha wakamfuata baba mwenye nyumba wakampiga na kumwamuru awape fedha (Sh. 60,000) na kumfuata mke wake ambaye pia walimpiga na  kumpora Sh. 5,000.

Shuhuda wa tukio hilo alisema, baada taarifa hizo, sungusungu waliendesha msako na kufanikiwa kumkamata mmoja wa watuhumiwa akiwa na damu kwenye nguo zake na walipomhoji aliwataja watu wengine ambao walikamatwa wote.

Shuhuda huyo alisema, wakiwa chini ya uangalizi wa sungusungu ndipo wananchi waliofika kwenye eneo la tukio na kuwashambulia watuhumiwa hao ambapo wanne walikufa kwa kuchomwa moto huku  mmoja akikatwa panga kwenye mguu na kutumbukizwa kwenye kisima na kufia humo.

Mganga mfawidhi wa Hospitali ya wilaya Geita, Dk. Adam Sijaona, alithibitisha kupokea miili ya marehemu ambayo imehifadhiwa hospitalini hapo.

Akithibitisha kuwepo kwa tukio hilo, Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Geita Kamishna msaidizi mwandamizi, Leonard Paul, alisema watu hao walichomwa moto na kufariki dunia.

Aliwataja baadhi ya waliouawa kuwa ni Juma Patrick Kigara, Marwa, Chacha Kigara na wawili waliofahamika kwa jina moja moja la Eze na Shija huku watano akiwa hajafahamika jina lake.

Kamanda Paulo amedai kuwa tayari watu watatu akiwemo kiongozi wa walinzi wa jadi sungusungu wanashikiliwa na polisi kwa mahojiano huku jeshi likiendelea na upelelezi zaidi kuwabaini waliohusika na uchochezi huo.
SOURCE: NIPASHE

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni