Mwigulu anadaiwa kuwashawishi madiwani hao wakubali sh milioni 45 ili wajivue uanachama wa CHADEMA.
Tanzania Daima imedokezwa kuwa baada ya mpango huo kukamilika, wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo walipousikia waliugomea kwa madai utasababisha machafuko zaidi katika maeneo yao.
Katika Wilaya ya Igunga, CHADEMA wana madiwani watatu kati yao mmoja ni wa viti maalumu ambapo Mwigulu anadaiwa katika mkakati wake huo, aliwashirikisha wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ambao walivujisha siri hiyo kwa uongozi wa CHADEMA.
“Tulimueleza wazi kuwa tutakuwa tunaiingiza serikali katika gharama za matumizi ya fedha kwa sababu zisizo na msingi wowote kwa ajili ya kutaka sifa za kisiasa, tulikataa na tukawaambia madiwani kama watathubutu kuwasaliti wananchi tutawafikisha mahakamani kwa kuwa mkakati huo tunauelewa,” alisema mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama mjini Igunga.
Kwa mujibu wa sheria, kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya inaundwa na mkuu wa wilaya na wawakilishi wa vyombo vyote vya usalama katika wilaya husika.
Mkakati huo unaelezwa kupata upinzani kutoka kwa wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wilayani Igunga, kwa kile walichoeleza kuwa wamechoka kushuhudia vifo na matukio ya uvunjifu wa amani yanayoweza kujitokeza.
Wapinzani wa mpango huo walieleza kuwa sababu ya kumkatalia Mwigulu ni pamoja na kurejea matukio yaliyojitokeza wakati wa uchaguzi mdogo wa ubunge uliomuingiza Dk. Dalaly Kafumu madarakani baada ya Rostam Aziz kujiuzulu nafasi hiyo akihusishwa na tuhuma za ufisadi.
Katika uchaguzi mdogo wa Igunga uliofanyika mwaka 2011, baadhi ya watu waliuawa na wengine kujeruhiwa katika mchakato mzima wa kuhitimisha uchaguzi huo.
Ofisa habari wa CHADEMA, Tumaini Makene, alipoulizwa juu ya kuufahamu mpango huo wa Mwigulu, alikiri kupata taarifa hiyo, lakini haukufanikiwa kwakuwa walidhibiti kila mwanya wa hujuma hiyo.
Akijibu tuhuma hizo, Mwigulu alisema hazina ukweli na hajui kama katika Wilaya ya Igunga kuna madiwani wa CHADEMA.
“Havina ukweli na sijui kama Igunga ina madiwani wa CHADEMA, kwani wana msaada gani kwa chama changu na wana tatizo gani wakiwa CHADEMA?” alisema.
Source: Tanzania Daima
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni