Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ambaye anakabiliwa na shinikizo la
kujiuzulu amesema atazungumzia hatima yake baada ya sikukuu za Krismasi
na Mwaka Mpya.
Gazeti la The Citizen, lilimkariri Pinda jana
akisema kwa sasa anahitaji amani na utulivu katika kipindi hiki cha
sikukuu baada ya shughuli za kikao kilichopita cha Bunge.
Katika kikao hicho, mawaziri wanne walitimuliwa baada ya ripoti ya
kamati ndogo ya Bunge kufichua madhara yaliyojitokeza wakati wa
utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili.
Wabunge kadhaa walishinikiza kujiuzulu kwa Pinda na mawaziri wengine,
ambao wizara zao zilihusika katika utekelezaji wa operesheni hiyo.
“Baada ya kikao cha Bunge Dodoma nilikwenda likizo kuwasalimia wazazi
wangu. Wasiliana na mimi baada ya likizo halafu niulize maswali yako
yote nitakujibu,” alisema Pinda, ambaye yuko katika Kijiji cha Kibaoni,
Mkoa wa Katavi.
Rais Jakaya Kikwete alitengua uteuzi wa mawaziri Khamis Kagasheki
(Maliasili na Utalii), Dk Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani), Shamsi Vuai
Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa) na Dk David Mathayo(Uvuvi na
Maendeleo ya Mifugo), baada ya malalamiko ya wabunge.
Pinda alikiri bungeni kuwa operesheni hiyo ilikuwa na matatizo na
wale wote waliokuwa na dhamana walikiuka taratibu za utekelezaji wa
Operesheni Tokomeza Ujangili.
Pamoja na kujiuzulu kwa mawaziri hao, pia Serikali itaunda tume, ambayo itaongozwa na Jaji ili kuchunguza sakata hilo undani.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni