Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amesema Wazanzibar
wanaisubiri kwa hamu Rasimu ya Katiba ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba
ili kuona kama imezingatia masilahi na matakwa yao katika kupata mamlaka
kamili ya Zanzibar.
Msimamo huo ameutoa kwenye mkutano wa hadhara wa
CUF uliofanyika Kinyasini, Mkoa wa Kalazini Unguja na kuhudhuriwa na
wajumbe wa Kamati ya Maridhiano inayoongozwa na Mwenyekiti wake, Mzee
Hassan Nassor Moyo.
Aidha, katika mkutano huo, kwa mara ya kwanza
Waziri wa zamani wa SMZ na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC),
Mansoor Yussuf Himid alihutubia tangu avuliwe uanachama wa CCM kutokana
na madai ya kwenda kinyume na sera, maadili na nidhamu ya chama hicho.
Katika maelezo yake, Maalim Seif alisema
wanachodai Wazanzibar ni mamlaka kamili ni kuifanya Zanzibar ijitegemee
kiuchumi, kujipangia na kujiamulia mambo yake ya ndani na nje bila ya
kutegemea upande wowote.
Alisema Zanzibar ilikuwa taifa huru lililoungana
na Tanganyika kwa ridhaa na siyo mateka wa Tanganyika, hivyo wanayo
sababu ya kujitegemea.
“Madai yetu yako wazi, hayana kificho na siyo
mageni, tunaisubiri kwa hamu rasimu ya Jaji Warioba, kama ni supu
isiyolika, hatutaila tutamrudishia mwenyewe na kuendeleza madai yetu,”
alisema Maalim Seif.
Maalim Seif, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa
Rais Zanzibar, alisema Zanzibar itasimama wenyewe na kujiendeleza kwa
kufuata misingi iliyowekwa na Rais wa Kwanza wa Zanzibar hayati Mzee
Abeid Amani Karume.
“Madai yetu ni kama meli iliyobeba watu wengi,
ikizama tunazama wote, lengo letu ni kufika salama katika bandari ya
matumaini na kila mmoja aweze kunufaika na matunda ya nchi yake,”
alisema Maalim Seif.
Alisema ikiwa Wazanzibari watapata Serikali,
anaamini mengine yatakuja yenyewe na kuinufaisha Zanzibar kiuchumi na
kusisitiza kuwa muundo wa Serikali mbili umepitwa na wakati.
>>Mwananchi
>>Mwananchi
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni