Akizungumza katika mkutano wa hadhara kwenye viwanja vya Kwa Noti Ujiji Mjini Kigoma, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Kirumbe Ng’enda alisema kuwa Zitto alikuwa sahihi katika kusimamia mambo hayo makubwa mawili.
Alisema kuwa CHADEMA kama chama ambacho kinajinasibu kusimamia demokrasia nchini kilipaswa kuonesha kwa vitendo utekelezaji wa jambo hilo, lakini badala yake baadhi ya viongozi wa chama hicho wameonesha kuwa chama hicho hakitekelezi demokrasia.
Ng’enda aliongeza kuwa kitendo cha kutangaza kuwa na nia ya kuwania uenyekiti kwa Zitto imekuwa tatizo kubwa kwa mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini, hali ambayo uongozi wa CHADEMA umeona ni uhaini na kuamua kumvua madaraka.
Aidha akizungumzia matumizi na usimamizi wa fedha za ruzuku ambazo vyama vya siasa vinapewa Mjumbe huyo wa Halmashauri Kuu ya CCM alisema kuwa hilo ni suala la kisheria na ni lazima kila chama kioneshe matumizi sahihi ya fedha hizo kwa kuwa na taarifa ya mahesabu iliyokaguliwa ambapo Zitto kama Mwenyekiti wa kamati ya bunge ya hesabu za serikali analo jukumu la kusimamia na kuwasilisha bungeni taarifa hizo.
“CHADEMA wanashangaza sana badala ya kuonesha taarifa iliyokaguliwa wanaanza kumsulubu Zitto kwamba anawasaliti, mara anatumiwa na CCM kuwahujumu, yote hiyo inaonesha hakuna demokrasia wala utawala bora kwa viongozi wa chama hicho,” alisema Kirumbe Ng’enda.
Awali akizungumza katika mkutano huo Katibu Mwenezi wa CCM wilaya ya Kigoma Mjini, Zuberi Mabie alisema kuwa CHADEMA imeonesha haina ukomavu wa kisiasa wala utawala wa pamoja na ndiyo maana baadhi ya viongozi kwa kuona kama chama ni mali yao hawataki kukosolewa.
Mabie alisema kuwa kukosolewa kwa viongozi ni jambo la kawaida na kwamba CHADEMA inakosea kwa kiasi kikubwa kumsulubu Zitto ambaye ameonyesha msimamo na uzalendo wake kwa Taifa badala ya chama kwa kusimamia utekelezaji wa sheria na katiba ya nchi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni