HUU ni msimu wa sikukuu! Juzi, tumesherehekea Sikukuu ya Krismasi na
sasa tunaelekea Mwaka Mpya 2014. Kwa nguvu za Mungu tutafika salama.
Ndugu zangu, hebu tutafakari vizuri kuhusu mwaka uliopita na kuangalia
cha maana tulichofanya kwa wenzi wetu.
Tuliwaumiza au tuliwapa furaha? Je, kupitia kona hii matatizo
yameondoka, yamepungua au yameongezeka? Nimeandika mada nyingi ambazo
zimewagusa watu wengi. Ujumbe wenu na simu mlizopiga zinaonyesha jinsi
kona hii inavyosomwa na watu wengi, tena makini.
Kwa vile tunakaribia kumaliza mwaka na kuanza mwingine mpya, basi
napenda kuwapa kazi ya kufanya utafiti kuhusiana na mwenendo mzima wa
maisha yenu ya kimapenzi. Huu ndiyo muda muafaka wa kujichambua
mwenyewe ulibeba vipi uhusiano ndani ya penzi lako.
Katika muda wote kulikuwa na migongano, je, chanzo chake nini? Kama
ni wewe ni muda wako wa kujirekebisha ili usiwe chanzo cha matatizo ya
kila siku.
Ni makosa mtu kurudia kosa moja kila mara, mwanadamu
anayejitambua hujifunza kupitia lile linalokemewa sana na mwenzake,
japokuwa unapenda kulifanya.
Sifa kubwa ya mwanadamu ni kufikiri kabla ya kutenda, siku zote
mapenzi ni kusikilizana, kufarijiana na kubembelezana. Bila shaka mwaka
huu unaomalizika kuna mambo yalitokea hadi kufikia hatua ya kutishia
kuvunja ndoa au uhusiano wenu.
Mwaka unaisha, umekaa na kujiuliza tatizo nini? Umejichunguza na kujua labda wewe ndiye chanzo?
Mmeukaribisha mwaka, mmekaa kama wanandoa au wapenzi kumaliza tofauti zenu?
Kama hamjakaa kujadili mwenendo mzima wa uhusiano wenu kwa mwaka
mzima hamjachelewa. Hebu kupitia makala haya kaeni chini na kuchambua
matatizo yote yaliyowakwaza sana. Tafuteni sehemu tulivu ili kupata
nafasi ya kuzungumza kwa kujiamini. Sehemu hii haitakiwi mmoja kujiona
yupo juu ya mwenzake au ubishi kwa kile ambacho kimemgusa.
Mazungumzo yenu yawe ya kirafiki, kosoaneni kwa sauti za kawaida,
ondoeni jazba kwani muda huo hauna nafasi. Uwe mwepesi kukubali kosa na
kuomba msamaha. Kwa vile nia yenu ni kujenga, hakikisheni yote
yaliyowakwaza mwaka uliopita hamyapi tena nafasi.
Jiepusheni kuwa chanzo cha maumivu ya wenzenu, umeamua huyo awe wako
wa kufa na kuzikana kwa nini muumizane? Sawa, mwanadamu ana upungufu,
basi makosa yako yasiwe mazoea kwa vile tu upo juu ya mwenzako.
Mapenzi hayaangalii cheo, fedha wala uzuri wa sura na umbile, bali kujitoa kwa ajili ya mwenzako. Jutia makosa uliyofanya mwaka huu na uanze upya mwaka ujao.
Anza mwaka ukiwa makini sana na kumfanya mpenzi wako asahau maumivu
ya mwaka jana. Muahidi mpenzi wako kuwa mwaka huu utakuwa sehemu ya
furaha yake ya kila siku, kama utakwenda tofauti basi utakuwa msaliti.
Kiapo hiki si cha mtu mmoja bali kiwe cha wote. Kama kweli unayosema
yanatoka moyoni na kuwa tayari kutorudia yaliyomkwaza mwenzako mwaka huu
unaoishia, basi mwaka ujao utakuwa wa furaha na amani. Nakutakieni
mwaka mpya wenye mapenzi ya dhati, kila mmoja awe sehemu ya furaha ya
mwenzake. |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni