Alisema huo ni utaratibu wa kawaida unaotumiwa na ofisi yake kurejesha fedha za Bunge ambazo hazikutumika kama ilivyokusudiwa, isipokuwa kwa wabunge ambao hukubali kwa hiari yao kuzirejesha.
Dk. Kashilillah aliwataja wabunge ambao mishahara yao imeanza kukatwa kuwa ni Mbunge wa Mbinga, John Komba (CCM), Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi (CCM), Mbunge wa Tabora Mjini, Aden Rage (CCM) na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema).
Wengine ni Mbunge wa Hai ambaye pia ni kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe (Chadema), Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema), Mbunge wa Viti Maalumu, Zainabu Kawawa (CCM), Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Matiko (Chadema), Mbunge wa Viti Maalumu, Joyce Mukya (Chadema) na Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono (CCM).
Alipoulizwa kama uamuzi huo ni hatua za kuwaadhibu wabunge hao kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao ya kibunge, alisema hakuna mbunge anayeadhibiwa, bali ni utaratibu wa kawaida ambao umekuwa ukitumika kwa muda mrefu.
“Hakuna mbunge anayeadhibiwa hapa, huu ni utaratibu wa kawaida kabisa, kwa sababu Ofisi ya Bunge inazo taarifa zote za wabunge, hivyo hata wale ambao tuliwalipa lakini hakuwasafiri au walikatisha ziara, taarifa tulikuwa nazo mapema kabla hawajaanza kuumbuana bungeni.
“Hayo waliyoyasema bungeni ni mambo yao ya kisiasa, lakini ofisi yangu ina taarifa zote za wabunge 15 ambao hawakusafiri au walikatisha safari zao. Wapo waliokwisharejesha na ambao hawajarejesha, hawa ofisi ya uhasibu imekwishaanza kukata mishahara yao,” alisema Dk. Kashilillah.
Source: Mtanzania
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni