Nchimbi ambaye ni mbunge wa Songea Mjini kwa tiketi ya CCM, alisema hayo juzi kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa facebook, wakati akisherehekea kutimiza miaka 42 ya kuzaliwa.
“Kama Mwenyezi Mungu angeniuliza ni kitu gani anipatie kwa muda huu, ningemuomba anipatie moyo wa upendo na kusamehe,” aliandika.
Mawaziri wengine waliovuliwa nyadhifa zao pamoja na Nchimbi, ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Mathayo David Mathayo na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha.
“Sasa nina miaka 42, namshukuru Mungu kwa kunibariki na kunisaidia kwa kipindi cha mwaka mzima, nawashukuru wazazi wangu, kaka, dada na marafiki zangu, pia ninawashukuru waajiri wangu watu wa Jimbo la Songea na Watanzania wote.
“Ninaukubali upendo wenu na kuniunga mkono…Kama Mungu ataniuliza leo kitu gani anipatie jibu langu litakuwa rahisi, nitamwambia Mungu wangu naomba moyo wa upendo kwa kila mmoja, moyo wa kumsamehe kila mmoja pasipo kujali nini nitarudishiwa, anipe moyo wa kuwatumikia watu kwa saa 24 kwa siku,” alisema Dk. Nchimbi.
Dk. Nchimbi na wenzake wanne walienguliwa madarakani baada ya Rais Jakaya Kikwete kutengua uteuzi wao mara baada ya kupewa taarifa za wabunge kuwashinikiza mawaziri hao wajiuzulu kwa sababu ya yaliyojitokeza katika Operesheni Tokomeza Ujangili.
Kuondolewa kwa mawaziri hao kulitokana na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli, kuwasilisha taarifa ya kamati yake iliyobainisha unyama mkubwa waliotendewa wananchi katika operesheni hiyo.
Operesheni hiyo ilikuwa ikizihusisha wizara za mawaziri hao waliong’olewa ambapo inadaiwa watendaji waliokuwa wakiiendesha waliua watu, kujeruhi na kuharibu mali mbalimbali ikiwemo mifugo.
Matukio mengine yaliyobainika kwenye operesheni hiyo ni wanawake kubakwa na wengine wakilazimishwa kufanya mapenzi na mama, wakwe au watoto wao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni