Taarifa zilizoenea mitandao mbali mbali
ya Nigeria saa chache zilizopita zinazungumzia tukio kutoka Kenya
linalohusiana na kukamatwa kwa msanii wa Nigeria Wizkid ambaye
alishikiliwa na na jeshi la Polisi nchini humo saa chache kabla ya
kupanda ndege kurejea Nigeria.
Taarifa iliyoandikwa na Standard Digital
Kenya imesema, Wizkid alikamatwa hotelini Nairobi Crown Plaza ambapo
amekaa kwa takribani wiki moja baada ya kufanya onesho lake.
Kwa mujibu wa habari kutoka chanzo
hicho, Wizkid alikamatwa kwa kosa la kuvuta bangi hotelini hapo na baada
ya mzozo wa muda mrefu baina yake na mhudumu wa hoteli hiyo, mhudumu wa
hoteli alitoa taarifa polisi ambao walimkamata na kumfikisha kituo cha
Capital Hill ambapo alipigwa faini ya sh. 50,000 za Kenya kwa kosa hilo
na baadaye kuachiwa huru.
Wizkid alikamatwa hotelini hapo siku ya
jumamosi kwa kosa hilo, ambapo Victoria Kimani, msanii wa Kenya ambaye
wamefanya kolabo hivi karibuni ametajwa kuhusika kumtoa Wizkid kutoka
kituo cha Polisi.