.

Alhamisi, 9 Oktoba 2014

CUF Yakiri Kuwa Ni Vigumu Kuiondoa CCM katika madaraka.

Chama cha Wananchi (CUF) kimekiri kwamba ni vigumu kuondoa Chama Cha Mapinduzi (CCM) maradakani bila kuwa na umoja na mshikamano baina ya wanachama na viongozi.
Aidha chama hicho kimesema CCM ni chama kilichokaa madarakani kwa muda mrefu hivyo kama kweli wanataka kukiondoa, ni lazima kuwe na mipango madhubuti ya kisiasa ikiwa ni pamoja na wanachama kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi mbalimbali.
Akihutubia juzi wanachama pamoja na wananchi wilayani Masasi waliojitokeza kumsikiliza kwenye mkutano wa ndani, mjini hapa, Mwenyekiti Taifa wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema wakati umefika kwa wanachama kuacha maneno badala yake wajitokeze kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura wawe na sifa za kupiga kura.
Alisema bila umoja na mshikamano ni sawa na kuota ndoto za alinacha kuiondoa CCM madarakani.
Alisema ni vyema wanachama wakajenga mtandao imara mikoa yote nchini ili katika uchaguzi mbalimbali, waishinde CCM.
Kwa mujibu wa Profesa Lipumba, vijana ni nguvu kazi ya taifa ambao wengi wao huwa hawajihusishi moja kwa moja na masuala ya siasa, badala yake wanaishia kulaumu Serikali kuwa haiwaletei maendeleo.
Alisema kama wote wangeipigia Cuf kura ilikuwa ni rahisi kuiondoa CCM.
“Ndugu zangu, wanachama wenzangu kazi ya kuiondoa CCM madarakani si lelemama kama mnavyodhani…hivyo kama hamtajitokeza kujiandikisha pamoja na kupiga kura kwenye chaguzi mbalimbali itakuwa kazi bure,” alisema.
Alisema CUF ina nia ya dhati kuiondoa CCM lakini changamoto kubwa iliyo mbele yao ni ushiriki mdogo wa vijana ambalo ni kundi kubwa.
Alisema Desemba mwaka huu ni Uchaguzi wa Serikali za Mitaa hivyo aliwataka wanachama kujitokeza kwa wingi kupiga kura huku akisema hiyo ndiyo silaha pekee ya kukiondoa Chama Cha Mapinduzi (CCM) madarakani.
Katika hatua nyingine, Profesa Lipumba aliongoza harambee ya kuchangia ununuzi wa uwanja kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya chama hicho Wilaya ya Masasi ambapo jumla ya Sh 430,000 taslimu zilipatikana huku ahadi ikiwa ni Sh 270,000.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni