.

Jumatano, 20 Novemba 2013

NADHARIA HII, ITAWASHANGAZA HATA WANAWAKE WENYEWE........

 Nadharia hii itawashangaza hata wanawake wenyewe…..!

Mnamo Agost 23, 1973, majambazi wawili wenye silaha aina ya machine gun, walivamia benki moja jijini Stockholm, Sweden. Mmoja kati yao ambaye Alikuwa ametoroka jela siku chache nyuma, Jan-Erik Olsson alitangaza kwamba, “Shughuli imeanza.”

Majambazi hao waliwashikilia mateka watu wanne, wanawake watatu na mwanaume mmoja. Mateka hao walifungwa mabomu miilini na kushikiliwa ndani ya benki hiyo kwa muda wa saa 131, ikiwa na maana kwamba, walishikiliwa kwa siku tano. Mateka hao waliokolewa Agosti 28 na majambazi hao kukamatwa.



Baada ya kuokolewa, mateka wawili walionyesha jambo la kuchangaza na pengine kutisha, kama siyo kuudhi kwa baadhi. Walifanyaje?


Pamoja na kufungiwa mabomu na watekaji wale, kutishwa, kudhalilishwa na kuishi kwa hofu kuu mikononi mwao, lakini walipookolewa wanawake wawili kati ya hao watatu waliwakumbatia na kuwabusu wale majambazi kwa bashasha. Lakini pia waliamua kuwapenda na kuwasaidia majambazi wale.


Walipohojiwa na vyombo vya habari vya nchi hiyo, walisema, hata watu wa usalama walipofika kuwaokoa, walishajenga upendo kwa watekaji, wakiamini kwamba, ni kweli watekaji walikuwa wakiwalinda kutoka kwa polisi.


Baadaye mwanamke mmoja kati yao alifunga uchumba na jambazi mmoja. Mwanamke wa pili alianzisha mfuko kuwachangia wale majambazi fedha za kuwawezesha kupata huduma bora za kisheria ili wasifungwe au kupata adhabu nafuu. Kumbuka hawa wanawake ndiyo waliokuwa wamefungiwa mabomu wakati wa utekeji…!


Hali hii ambayo baadaye ilikuja kupewa jina la Stockholm syndrome, imekuwa ikitambuliwa katika Saikolojia kwa miaka mingi kabla ya tukio lile la Stockholm. Kilichotokea kwenye tukio hili, ni wale waliotekwa kujifunga kihisia na watekaji.


Hali hii imewahi kujitokeza huko nyuma kwa watekwaji wengine, wafungwa na kwenye ufujaji wa aina mbalimbali ukiwemo ule wa watoto, wanawake, na wafungwa wa kivita. Imebainika na inafahamika vizuri sana kwamba, uamuzi wa mateka kujibainisha na kujifunga kihisia na watekaji huwa ni mkakati wa mateka kujiwezesha kuendelea kuishi. Kwenye uhusiano wa kifujaji, mwanamke anayefujwa anaweza kuamua kumtetea na kumpenda zaidi mumewe ikiwa ni mkakati wake wa kujiweka katika mazingira ya kumudu kuendelea kuishi.


Kwa hiyo, mwanamke kufujwa na mumewe na bado mwanamke huyo akamtetea mumewe, akawa tayari kufa kwa ajili yake akimlinda asichukuliwe hatua za kisheria kwa kumpiga kwa mfano, ni jambo ambalo kwa wanasaikolojia halishangazi tena. Lakini halishangazi kwa polisi ambao wamekutana sana na kesi za wanawake wanaofujwa.


Kuna wanawake wengi ambao hufujwa na waume zao, lakini wao ndiyo wako mstari wa mbele kuwatetea waume hao wasiadhibiwe. Kuna wakati wanawake wanaofujwa huenda kuwawekea dhamana waume zao ambao wamekamatwa kwa kuwapiga wao (wake) kuna wakati wanawake hao wako tayari kuwatukana au hata kuwageuka na kuwashambulia watu wanaokuja kuwasaidia wakati wakipigwa na waume zao……………!

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni