Gazeti la Mwananchi leo November 24 2013 limeandika >>> Siku moja baada ya Kamati Kuu ya Chadema kumvua uongozi aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Taifa wa chama hicho, Zitto Kabwe, mama yake mzazi, Shida Salum ametoa ya moyoni akieleza kuwa kilichomkuta mwanaye kimefunika mabaya mengi yaliyopangwa afanyiwe.
“Kwa upande wangu naona kama ni ushindi kwa Zitto kutokana na jinsi
ninavyojua hali ilivyo, mambo yalikuwa ni mengi mno na nikwambie tu,
Zitto kuvuliwa uongozi kumefunika hayo yaliyokuwa yamekusudiwa kufanywa
dhidi yake, nilikuwa naomba Mungu kila siku ili afukuzwe Chadema,”
alisema mama huyo wakati akizungumza na gazeti hili nyumbani kwake
Tabata, Dar es Salaam.
Shida Salum alisema kuwa Mungu amemnusuru mwanaye na kusisitiza,
“Watu walikaa na kutengeneza ripoti ya siri kuhusu Zitto na kuiweka
kwenye mtandao kisha kuituma kwa wanachama wa Chadema wanaowafahamu.
Mpaka wanafikia hatua hiyo maana yake ni kwamba wamejaribu njia zote za
kummaliza, lakini wameshindwa.”
Alisema kutokana na hali ilivyo hivi sasa amemnyang’anya mwanaye kwa
muda simu zake zote za mkononi, kompyuta mpakato (Laptop) pamoja na iPad
ili asiwasiliane na watu, kwa maelezo kuwa wapo wenye nia mbaya
wanaomsaka kumpa pole za kinafiki. “Kwa sasa nataka mwanangu atulize
akili.”
Shida Salum, mbali na kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, pia ni
mwasisi wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu (Shivyawata) na
Mwenyekiti wa Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Viungo (Chawata).
Zitto pamoja na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Dk Kitila Mkumbo
juzi walivuliwa uongozi kutokana na uamuzi wa kikao cha Kamati Kuu
kilichokutana kwa siku mbili, kuanzia Novemba 20 mwaka huu katika Ukumbi
wa Blue Pearl jijini Dar es Salaam, wakituhumiwa kukisaliti chama.
Mbali ya kuwavua uongozi Zitto, Dk Mkumbo pamoja na aliyekuwa
Mwenyekiti wa chama hicho mkoani Arusha, Samson Mwigamba, pia Kamati Kuu
imewapa siku 14 wajieleze kwa nini wasifukuzwe uanachama.
Kwa uamuzi huo Zitto amebaki na wadhifa wa ubunge wake wa Jimbo la
Kigoma Kaskazini na Uenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali
(PAC).
Katika ufafanuzi wake wa jana, Shida aliwataka wanachama wa Chadema
kuwa watulivu kwa maelezo kuwa Zitto hajafukuzwa uanachama, “Siku nyingi
walikuwa wanamwinda na hata hilo jambo ambalo Chadema wanasema
amefanya, hawana uhakika nalo.”
Juzi wakati akisoma uamuzi wa Kamati Kuu, mwanasheria wa Chadema,
Tundu Lissu alisema wamebaini kuwapo kwa mkakati mkubwa wa watu hao
kutimiza malengo hayo ambao umeandikwa katika waraka unaoitwa ‘Mkakati
wa Mabadiliko 2013’, ambao umeandaliwa na kikundi kinachojiita ‘Mtandao
wa Ushindi’.
Alisema kikundi hicho vinara wake wapo wanne, Zitto anajulikana kama
Mhusika Mkuu (MM), Mkumbo (M1), Mwigamba (M3) na mtu mwingine wa nne
ambaye alieleza kuwa hajatambulika na anatumia jina la M2.
Stori imetoka mwananchi.co.tz
Stori imetoka mwananchi.co.tz
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni