WABUNGE wawili wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rosesweeter Kasikila na Profesa Juma Kapuya, wameingia katika kashfa mbaya ya kimapenzi inayoweka hatma yao kisiasa shakani.
Kashfa za wabunge hao wa CCM zinatokana na hatua yao ya kujiingiza kwenye mahusiano ya kimapenzi kwa nguvu na vijana wadogo.
Rosesweeter ambaye ana umri wa miaka 60, yuko katika kashfa ya
kufunga ndoa na kinda wa miaka 26, Michael Christian, wakati Profesa
Kapuya anahaha kujinasua na kashfa inayomzingira ya kumbaka binti wa
miaka 16, ambaye sasa anatishia kumuua baada ya kumwaga mtama hadharani.
Ukija kwenye kashfa ya Rosesweeter kufunga ndoa na kijana wa miaka 26
sio kosa kisheria, lakini wadadisi wa mambo wanasema kimaadili ndoa
hiyo haikupaswa kufungwa kutokana na umri wa bibi harusi kuwa mkubwa
kiasi kwamba hana uwezo tena wa kuzaa wakati bwana harusi ndiyo kwanza
kijana wa miaka 26 tu.
Wakati Profesa Kapuya anadaiwa kumbaka msichana huyo mwaka 2011,
Rosesweeter naye alifunga ndoa na kijana huyo mwaka huo huo, Septemba
Mosi.
Kabla ya wawili hao kuamua kufunga ndoa, mbunge huyo kutoka mkoani
Rukwa, mwenye makazi yake Bagamoyo mkoani Pwani, alikuwa akimtumia
Michael kwenye shughuli mbalimbali na muda wote alikuwa akiishi nyumbani
kwake.
Inaelezwa kuwa mbunge huyo ambaye ana familia ya watoto wawili ambao
kiumri wanalingana na Michael, alianza uhusiano wa kimapenzi na kijana
huyo kwa siri kubwa na baadaye alifanikiwa kumshawishi wafunge ndoa huku
akimuahidi kumpa huduma mbalimbali anazotaka.
Hata hivyo, kashfa ya Rosesweeter kwa sasa imeongezeka baada ya
kuamua kuzuia vyeti vya shule vya kijana huyo baada ya kufunguka macho
na kuamua kuachana na ndoa hiyo ambayo kwa vigezo vyote ni batili.
Wakati kijana huyo ameamua kuvunja ndoa hiyo kwa kile alichoeleza
kukosa uhuru, manyanyaso na mambo mengine, mbunge huyo anasisitiza kuwa
ndoa hiyo bado halali kwani haijavunjwa kisheria na kuongeza kuwa kinda
huyo bado ni mume wake.
Mbunge huyo bila kumung’unya maneno anakiri kufunga ndoa na kinda
huyo na kuitangazia jamii kuwa kijana ndiye aliyemdanganya na kumtaka
wafunge ndoa hiyo ambayo hadi leo imebaki kuwa gumzo nchini.
Hata hivyo, ndoa anayosisitiza mbunge huyo kuwa ni halali, inaelezwa
kuwa ni batili kutokana na ukweli kwamba imefungwa bila kuzingatia
vigezo kwani haijatangazwa mara tatu kama sheria ilivyotaka, imefungwa
kwa siri bila wasimamizi wala mashuhuda katika Kanisa la Mikocheni B
Assemblies Of God Mlima wa Moto linaloongozwa na Mchungaji Getruda
Rwakatare.
Tayari wanaharakati na baadhi ya viongozi wa dini wameandika barua
kwa Waziri wa Mambo ya Ndani kutaka aingilie kati kumsaidia Michael
apate vyeti vyake vya shule, vinavyoendelea kushikiliwa na mbunge huyo
na kusisitiza kwamba hawezi kuvitoa kwani bado kijana huyo ni mumewe.
Kashfa ya Kapuya
Kashfa ya Profesa Kapuya ya kudaiwa kumbaka msichana wa miaka 16, ni aibu kwa mbunge huyo ambaye amepata kuwa waziri.
Mbunge huyo maarufu nchini, anadaiwa kumbaka binti hiyo kwenye hoteli
moja ya kitalii iliyoko jijini Dar es Salaam mwaka 2011, na kurudia
tena kitendo hicho ndani ya ofisi yake katika jengo la Biashara Complex
lililoko Mwananyamala Juni 3, 2012 alipoitwa kwenda kuchukua ada kwa
mara ya pili.
Wakati Serikali inakusudia kufungua mashitaka mawili ya kubaka na
kutishia kuua dhidi ya Profesa Kapuya, waziri huyo wa zamani bila woga
ameendelea kutuma ujumbe mfupi kupitia simu yake ya mkononi kwa binti
huyo na kusisitiza kuwa lazima amuue.
Profesa Kapuya amekuwa akitumia simu yake kuhamisha fedha kwenda kwa
binti huyo ambaye hivi karibuni katika baadhi ya vyombo vya habari
alikana kumfahamu na hajawahi kukutana naye.
Amekuwa akihamisha fedha kutoka kwenye simu yake namba 0784993930
iliyosajiliwa kwa jina lake kwenda kwa namba inayomilikiwa na binti
huyo.
Tayari serikali kupitia Jeshi la Polisi, imesema inakusudia kufungua mashitaka mawili dhidi ya mbunge huyo.
Mashitaka yanayotajwa kumkabili Kapuya ni ya ubakaji na kutishia kuua.
Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova,
aliliambia gazeti hili juzi kuwa jeshi lake halitakuwa na sababu ya
kumuacha mbunge huyo aendelee kutamba mitaani huku akituma ujumbe wa
vitisho kwa binti wa miaka 16 anayedaiwa kumbaka.
Kutokana na mfululizo wa habari hiyo ambayo imekuwa ikichapishwa na
gazeti hili, Profesa Kapuya kupitia kwa wakili wake Yasin Memba,
ametishia kuliburuza mahakamani endapo halitamwomba msamaha ndani ya
siku saba.
Mbali na kutishia kulipeleka gazeti hili na baadhi ya mitandao ya
kijamii mahakamani, pia Profesa Kapuya alikana kumfahamu binti anayedai
alibakwa huku akikanusha kumiliki simu namba 0784993930 ambayo imekuwa
ikitumiwa kuwasiliana naye ikiwemo kumtumia ujumbe mfupi wa maneno (sms)
wa vitisho.
Source: Tanzania Daima
Source: Tanzania Daima
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni