KATI
ya vitu vilivyoonesha kushangaza wengi wakati wa kilele cha wiki ya
usalama barabarani kilichofanyika hivi karibuni mkoani Dodoma ni baadhi
ya wakazi za eneo la Chaduru kutaka Kikosi cha Usalama Barabarani cha
Jeshi la Polisi kuweka askari wa kuvusha walevi ili wasiendelee kufa kwa
kugongwa na magari hasa nyakati za usiku katika eneo hilo.
Eneo
hilo pamoja na lile la Kizota limekuwa na ajali nyingi kutokana na kuwa
na vilabu vya pombe za kienyeji karibu na barabara kuu.
Si
binadamu pekee wamekuwa wakigongwa katika eneo la Kizota bali hata mbwa
na paka ambao wamekuwa wakifika vilabuni kwa ajili ya kutafuta makombo
ya nyama kutokana na eneo hilo kuwa maarufu kwa uchomaji wa nyama na
utumbo.
“Eneo
hili watu wengi wanaogongwa ni walevi wanaotoka vilabuni wakiwa
wamelewa. Kutokana na ulevi, mtu anaingia barabarani akiwa hatambui kama
anavuka barabara na gari kama liko kwenye mwendo kasi,” anasema mkazi
wa Chaduru, Juma Shabani Shabani anasema ni bora kungekuwa na alama za
madereva kupunguza mwendo wanapofika kwenye maeneo hayo kwani kukosekana
kwa vibao vya tahadhari imekuwa ikisababisha ajali hata nyakati za
mchana.
Wakazi
hao ambao walikuwa wakizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ambaye
alitembelea eneo la Chaduru na Kizota manispaa ya Dodoma akiwa na Mkuu
wa Kikosi cha Usalama barabarani Mkoa wa Dodoma, Mrakibu Mwandamizi wa
Polisi, Peter Sima na wadau wengine, walisema Jeshi la Polisi linatakiwa
kutoa elimu za mara kwa mara ili kupunguza tatizo la ajali ambazo
zinaweza kuzuilika.
Naye
Athumani Abdalah anasema ajali nyingi zinazotokea katika eneo la
Chaduru lenye vilabu vingi vya pombe za kienyeji zinaweza kuepukwa
endapo hatua zitachukuliwa kwa kugundua nini kinaendelea mahala hapo,
hususan nyakati za usiku.
“Tunaomba
Serikali kuweka askari ili kuvusha walevi katika eneo hili ili
wasiendelee kupoteza maisha kutokana na kugongwa na magari...
Wakishautwika mtindi wanavuka bila tahadhari,” anasema mkazi huyo.
Anasema
hakuna ubishi kwamba ulevi umekuwa chanzo kikubwa cha ajali eneo hilo
na kwamba jambo hilo linatakiwa kuangaliwa kwa makini kama kweli mkoa wa
Dodoma umedhamiria kupunguza ajali za barabarani zinazosababisha vifo.
Anasema
askari wa usalama barabarani wakiwekwa kwenye maeneo hatarishi kama
hilo la Chaduru itapunguza tatizo laajali. Kutokana na kauli hiyo, Mkuu
wa Mkoa wa Dodoma, Dk Rehema Nchimbi anasema hilo ni jambo
lisilowezekana kwani hakuna utaratibu wowote duniani unaoruhusu kuvusha
walevi barabara.
Anasema
serikali haiwezi kufanya kitu kama hicho na hakuna Serikali yoyote
duniani yenye utaratibu wa kuvusha walevi bali kinachotakiwa ni walevi
kuwa makini wanapovuka barabarani. Mkuu wa mkoa aliwataka wananchi wa
eneo hilo kuachana ama kupunguza ulevi kwani mbali na kugongwa, pombe
zina madhara ya kiafya kwa wale wanaoendekeza sana pamoja na kupunguza
kipato kwa ajili ya ustawi wa familia.
“Muwe
mnakunywa kwa kiasi si kwa kupitiliza. Mtu analewa hadi anakosa
kumbukumbu na kufahamu kuwa hii ni barabara na anatakiwa kupita kwa
uangalifu,” anasema.
Aliwataka
wananchi hao kuheshimu michoro ya usalama barabarani na hata kulinda
alama hizo badala ya kuzitoa hali inayofanya magari kukosa ishara ya
kutambua kama kuna alama au michoro katika eneo hilo.
Anasema askari wa usalama barabarani wanatakiwa kuvusha watoto, wenye ulemavu, wenye mahitaji maalumu lakini si walevi.
Dk
Nchimbi anasema jambo lingine linalochangia ajali ni pamoja na wananchi
kufanya biashara kwenye maeneo ya hifadhi ya barabara. Anasema katika
eneo la Kizota wengi wamepanga bidhaa zao za vyuakula, nguo na hata
nyama kando ya barabara na kusababisha njia ya waenda kwa miguu
kukosekana, kitu ambacho ni hatari.
Mkuu
wa Mkoa anataka ugumu wa maisha na hata umasikini usiwe sababu ya watu
kuvunja sheria kwa kufanya biashara katika maeneo hatarishi.
Anasema
ni muhimu kwa viongozi wa Serikali za Mtaa kukaa na wananchi na
kutafuta maeneo mengine ya kufanyia biashara na kuepusha idadi kubwa ya
watu wanaopoteza maisha katika eneo hilo.
Katika
eneo la Kizota, takwimu zinaonesha kuwa katika kipindi cha miaka mitatu
jumla ya watu 49 walipoteza maisha kutokana na kugongwa na magari.
“Hapa
Kizota tatizo ni kilabu kuwa karibu na barabara, mtu akilewa anatimka
haangalii kama kuna gari linakuja au vipi anajitosa barabarani na
kujikuta akigongwa na kufa,” anasema mkazi wa eneo hilo, John Mapiga
Anasema ajali nyingi zimekuwa zikitokea nyakati za usiku na kwamba mtu
akiwa amelewa, tena peke yake anakosa maamuzi sahihi na kujikuta
akigongwa.
“Ukilewa
hata gari ikiwa karibu unaliona kama liko mbali si kwa vile ni usiku na
taa inamulika. Ulevi ni mbaya lakini huwezi kumzuia mtu kunywa pombe
kwa vile atagongwa na gari dawa ni kunywa kwa kiasi unatoka kilabuni na
unafika nyumbani salama,” anasema. Anasema hakuna anayeweza
kumzuia mtu kunywa pombe lakini inawezekana kumfundisha mtu kuchukua
tahadhari pindi anapovuka barabara akiwa amelewa.
Kwa
upande mwingine, Mkuu wa Mkoa anataka kuwe na mikakati ya kuweka rekodi
za madereva wa magari na waendesha pikipiki ambao mara kwa mara
wamekuwa wakisababisha ajali ili ikibidi sheria zilizopo zitumike kuzuia
leseni zao.
Kwa
mujibu wa takwimu, jumla ya watu 727 wamepoteza maisha mkoani Dodoma
kutokana na ajali za barabarani katika kipindi cha mwaka 2010 hadi
Septemba mwaka huu.
Mkuu
wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani Dodoma, Peter Sima anasema watu
hao walipoteza maisha katika ajali 585 zilizotokea zikahusisha vifo
hivyo katika maeneo mbalimbali mkoani Dodoma.
Anasema
mbali na ajali hizo za barabarani pia jumla ya ajali 784 zilizotokea
katika kipindi hicho zilizosababisha watu 1919 kujeruhiwa.
Pamoja
na hayo, Sima anasema Kikosi cha usalama barabarani kimekusanya jumla
ya Sh milioni 670.6 kutokana na faini mbalimbali walizotozwa madereva
waliokiuka sheria za usalama barabarani katika kipindi cha Januari hadi
Septemba mwaka huu.
Aidha
katika kipindi hicho jumla ya madereva 21,680 walikamatwa kutokana na
makosa mbalimbali ya kuvunja sheria za usalama barabarani ambapo
walilipa faini jumla ya Sh milioni 670.6. Sanjari na madereva wa magari
waliokamatwa madereva wa pikipiki maarufu kama bodaboda walikuwa 3,036.
Anabainisha
kuwa jeshi hilo kwa kushirikiana na Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) na
shule ya Udereva ya Dodoma katika kipindi cha Januari hadi Septemba
waendesha pikipiki wapatao 2292 walipata mafunzo na kati ya hao 1,140
walipata leseni za kuendesha pikipiki.
Sima
anasema katika kupambana na ajali za barabarani katika mkoa wa Dodoma,
Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali limejipanga katika
mpango mkakati ikiwemo kurusha kipindi maalumu cha usalama barabarani
katika vituo mbalimbali vya redio vya mkoani Dodoma.
Anasema
mpango mwingine ni kuendelea kutoa elimu katika mikusanyiko ya watu
kama vituo vya mabasi na vituo vya waendesha pikipiki pamoja na kutoa
vipeperushi vya safari salama kwenye shule za msingi na sekondari.
Anasema
katika kipindi cha Januari hadi Septemba mwaka huu jumla ya wanafunzi
3,055 wamepewa elimu ya usalama barabarani na kati yao wanafunzi wa
shule za msingi ni 1,764 na za sekondari ni 1,309. Sima anasema mikakati
mingine ni kufanya ukaguzi wa magari hususani mabasi yanayosafiri
mikoani na Wilayani kuhakikisha yako salama kabla ya kuanza safari.
Aidha
kuwapima madereva ulevi kabla ya kuanza safari na kufanya ukaguzi wa
kushtukiza katika barabara kuu za mkoa na barabara nyingine kwa kutumia
vipima mwendo kasi kwa lengo la kuwabaini madereva wanaokwenda mwendo
kasi na kuwachukulia hatua za kisheria.
Anasema
licha ya wanaofanya makosa kutozwa faini, hatua hiyo imeonekana
haitoshi bali kinachohitajika ni kupiga hatua zaidi ya hiyo ikiwa ni
pamoja na elimu. Pia watumiaji wote wa barabara wana wajibu kuzingatia
sheria ikiwemo utunzaji wa hifadhi za barabara kwani kuna tatizo la watu
kuvamia hifadhi za barabara na kuzitumia kwa matumizi binafsi kama
gereji ama kufanya biashara mbalimbali.
“Uvamizi
huo ni kosa kwa mujibu wa sheria za usalama barabarani pia ni kikwazo
inapotokea barabara inayotumika imefungwa kwa namna moja au nyingine,”
anasema. Hifadhi za barabara eneo la Dodoma Inn, barabara ya mzunguko ya
barabara za Arusha hadi ya Bahi ni baadhi ya sehemu ambazo hifadhi za
barabara zimevamiwa.
Anasema
kamati ya usalama barabarani inatoa ushauri kwa Mamlaka ya Ustawishaji
Makao Makuu (CDA) na Manispaa kuona uwezekano wa kujenga stendi ya
mabasi ya masafa marefu nje ya mji ili kuondoa msongamano wa magari
mjini ambao tayari umeshaonekana kutokana na kuongezeka kwa magari.
Aidha wadau wanashauri ziwekwe alama za barabarani, ikiwa ni pamoja na
alama za vituo vya daladala katika barabara za manispaa na barabara kuu.
Wanadi
wanataka pia wakala wa barabara waone uwezekano wa kuweka taa za
kuongoza magari katika makutano ya barabara eneo la Ndasha, Chuo cha
Biashara na Kilimo/Relini.
Kadhalika
halmashauri ya manispaa ya Dodoma inashauriwa kujenga stendi muafaka za
daladala kwani stendi ya Jamatini ni ndogo na isitoshe haiko kwenye
mazingira rafiki ya mahitaji.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni