MKAKATI WA MABADILIKO 2013
UTANGULIZI:
Taasisi
tunayoizungumzia ilisajiliwa rasmi mwezi January 1993 na tokea wakati
huo imeongozwa na wakuu wa taasisi wapatao wawili na aliyepo kwa sasa ni
wa tatu. Wa kwanza aliongoza kwa miaka mitano tangu wakati huo 1993
hadi 1998 na kumwachia aliyefuata ambaye naye aliongoza kwa miaka mitano
hadi mwanzoni mwa 2004 na kumwachia aliyepo sasa. Huyu aliyepo
aliongoza kwa miaka mitano tangu mwaka 2004 hadi 2009 na kisha
akachaguliwa tena mwaka 2009 kwa kipindi cha pili.
Tunapenda kwa hatua ya mwanzo kabisa kutambua juhudi za wakuu wetu wote
waliopita walizozifanya katika kuhakikisha taasisi yetu inakua kwa
kutumia uwezo wote waliokuwa nao na katika mazingira yaliyowakabili.
Mwaka 1995 chini ya mkuu wa kwanza tulipata wawakilishi watatu kwenye
chombo chetu kikuu cha uwakilishi. Mwaka 2000 chini ya mkuu wa pili
tukapata wawakilishi wanne pamoja na wa nyongeza mmoja na kufanya idadi
kuwa watano. Mwaka 2005 chini ya mkuu wa tatu ambaye ndiye aliyepo hivi
sasa, tulipata wawakilishi watano na wa nyongeza sita jumla wakawa 11.
2010 chini ya mkuu huyu huyu wawakilishi wakaongezeka na kuwa 23 na wa
nyongeza 25 na kufanya idadi kuwa 48 kabla ya kupata mwingine mwaka jana
na kufanya sasa wawe 49.
Dk. Kitila Mkumbo.
Tunapopongeza juhudi zao hizi tunahitaji pia kuwapongeza wakuu wetu
wawili wa kwanza ambao kimsingi waliweka msingi mzuri sana wa
kutong’ang’ania madaraka na badala yake kuachia mapema na kumwachia
mwingine kidemokrasia bila vurugu. Hawakuwa madikteta na tunawapongeza
sana. Walijitahidi sana kutokuwa wapenda madaraka na kimsingi
walituwekea utamaduni ambao walitaka wote tuufuate na kujenga taasisi
imara inayojali demokrasia na haki ya kila mwana taasisi. Ni kwa msingi
huo waliamua kuandika kabisa katika mwongozo wetu kwamba kiongozi yeyote
katika ngazi yoyote ya kuchaguliwa atakapogombea na kushinda ataongoza
kwa kipindi kimoja cha miaka mitano na kisha ataweza kugombea na
kuongoza kwa kipindi cha pili cha miaka mitano baada yapo hawezi
kugombea tena katika nafasi ile ile aliyoitumikia kwa vipindi viwili.
Ili kuonyesha kwamba walimaanisha kile walichokisema, wote wawili
hawakuwahi kukaa madarakani kwa vipindi viwili vilivyoruhusiwa katika
mwongozo bali wote wawili walikaa kipindi kimoja kimoja tu.
Samson Mwigamba.
Lakini kuna matatizo yameanza kujitokeza na tusipochukua hatua haraka
huko mbele tunaweza kupata shida kubwa. Tunapenda kuainisha matatizo
hayo kwa uchache kama ifuatavyo:
Wakati tukiufanyia mwongozo wetu
mabadiliko mwaka 2006 hatukugusa kipengele kinachomzuia kiongozi
kuongoza kwenye nafasi moja kwa zaidi ya vipindi viwili vya miaka mitano
mitano. Lakini wakati mwongozo unachapwa chini ya uongozi uliopo,
kipengele hicho kiliondolewa kinyemela. Mambo yanayotokea hivi leo
yanaonyesha dhahiri kipengele hicho kiliondolewa kwa makusudi kwa
maslahi na kwa faida ya viongozi waliopo madarakani kwa sasa. Hiki
kinaweza kuchukuliwa kama kitendo kidogo lakini kama viongozi wetu
wanaweza kutokuwa waaminifu katika jambo kama hili, ni dhahiri hawawezi
kuaminika na wanaweza kufanya mambo mengine makubwa na yenye athari
zisizomithirika kwa taasisi yetu.
Ni dhahiri kwamba uongozi
uliopo umeishiwa mbinu na kuakisi jambo la msingi sana ambalo waasisi
wetu waliliona tangu mwanzo na kuamua kuweka kipengele cha ukomo wa
uongozi kwenye mwongozo wetu. Kuchoka kwa uongozi wetu kunaonekana
dhahiri katika mipango na mikakati ya taasisi ya miaka kadhaa. Mfano
mwaka 2008 uongozi ulianzisha mkakati wa operesheni samaki mkubwa
(maarufu kama Oparesheni Sangara). Huo ulifanyiwa kazi katika mikoa
kadhaa na hatimaye ikafa kimya kimya. Baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka
2010 kulianzishwa matembezi ya maandamano ambayo nayo yalikuwa
yakipeleka ujumbe kwa watu na yalipangwa kufanyika mikoa yote na wilaya
zote.
Kumbukumbu zetu zinaonyesha kwamba yalikuwa yakianzia makao
makuu ya mkoa na kwenda kwenye wilaya zote. Lakini kumbukumbu hizo
zinaonyesha kwamba yalifanyika Mwanza, Musoma, Shinyanga, Kagera na
mikoa ya Nyanda za Juu kusini (Mbeya, Iringa, Njombe na Rukwa) kisha
nayo yakafa kifo cha mende. Kisha mwaka 2012 ikaanzishwa operation ya
mabadiliko maarufu kama Movement for Change (M4C). Hiyo ilikuwa
inakwenda kwenye mikoa na timu kama nne hivi ambazo kwa ujumla
zilitathmini hali ya mtandao na uongozi wa taasisi, kuhamasisha umma kwa
njia ya mikutano ya hadhara, kuingiza wanachama na kusimika uongozi na
hatimaye kufanya mafunzo kwa viongozi. Hiyo ikafanyika Mtwara na Lindi,
Morogoro na kisha ikaenda kufia Iringa. Mwaka huu viongozi wetu wamekuja
na ugatuaji madaraka kutoka makao makuu ya taasisi na kupeleka madaraka
kwenye kanda mbalimbali. Mkakati huu ulikufa kabla ya kuanza pale
viongozi wakuu walipobadilisha maazimio ya kikao kikuu na kutekeleza
matakwa yao ikiwa ni pamoja na kuleta suala la viongozi wa muda kwa muda
mrefu badala ya kuajiri maofisa na wakahakikisha wanaweka watu wao
kwenye uongozi wa muda. Kitendo hiki kwa peke yake, cha kufeli kwa kila
mkakati unaoletwa na viongozi wetu katika hatua za utekelezaji
unaofanywa na wao wenyewe waleta mkakati, ni kiashiria tosha kwamba
uongozi uliopo umechoka.
Performance yetu kwenye chaguzi ndogo
nayo ni ishara kwamba mabadiliko yanahitajika. Tangu uongozi huu uingie
madarakani, kumefanyika chaguzi ndogo 8 za wawakilishi kwenye chombo
kikuu, kati ya hizo tumeshinda 2 tu sawa na asilimia 25. Aidha baada ya
mwaka 2010 kumefanyika chaguzi kadhaa za wawakilishi kwenye halmashauri.
Mwezi Oktoba 2011, mwezi wa4 2012, mwezi Septemba 2012 na mwezi Juni
2013. Kote performance yetu imekuwa poor kupindukia. Mfano mwezi wa Juni
2013 tumepata viti 6 kati ya 22 (27%) na mwezi Septemba 2012 tulipata
viti 7 kati ya 29 (24%). Ni dhahiri mabadiliko yanahitajika kwa kuwa
wakuu waliopo wanatumia mbinu zile zile na kupata matokeo yale yale.
Tunahitaji mbinu mpya. Kwa kifupi, ushindi ambao tumekuwa tukiupata
katika chaguzi ndogo haulingani na ukubwa wa hamasa kwa taasisi yetu
iliyopo mitaani. Hii ni kwa sababu tumekuwa tukitumia mbinu hizohizo
katika kila chaguzi. Aidha, tu wepesi mno wa kuridhika na kujisifu kwa
mafanikio madogo badala ya kukaa chini na kutafakari kwa kina mahala
tunapojikwaa.
Matumizi ya fedha za taasisi. Hakuna mtu anayejua
hivi sasa fedha za chama zinatumikaje zaidi ya kakikundi ka watu watatu
yaani mkuu kabisa, mtendaji mkuu na mkuu wa fedha kwenye taasisi yetu.
Maamuzi ya vikao hayaheshimiki tena na mabwana hawa. Baada ya uchaguzi
wa 2010 vikao halali vilielekeza kiasi na aina ya fedha ambazo
hazitaguswa bali zitunzwe kwenye akaunti maalum kwa ajili ya uchaguzi wa
2015. Lakini leo si tu akaunti hiyo haina fedha bali hakuna akaunti
yoyote yenye fedha. Watu watatu ndo wanaamua fedha zitumikeje. Mfano
mwingine ni maamuzi ya kikao cha juu mno cha hivi karibuni kilichoamua
kwamba kiasi cha fedha inayotoka serikalini kipelekwe kwenye mikoa na
wilaya na kiasi kingine kipelekwe kwenye kanda. Leo ni mwezi wa tano
maamuzi hayo hayajatekelezwa. Lakini kuna michango ya watu binafsi kama
yule mtanzania mwenye asili ya kihindi, hizo nazo hazijulikani
zimechukuliwa lini kwa mfumo gani, zikatunzwa wapi na hatimaye
zimetumikaje. Hapo hatujataja fedha zinazopatikana kutoka kwenye
fundraising events mbalimbali kama ile ya Dar es salaam na Mwanza. Hizo
nazo hazijawahi kuonekana na walioendesha hizo fundraising, uaminifu wao
kwenye masuala ya fedha ni questionable.
Taarifa za fedha. Tokea
baada ya uchaguzi wa 2010 mpaka leo, hakuna kikao chochote kilichowahi
kupokea na kujadili hadi mwisho ripoti ya mapato na matumizi ya fedha za
taasisi. Kila kikao agenda hiyo inarushwa kiaina. Wanaojua mchezo huo
ni watu watatu tu tuliowataja hapo juu na malengo ya kurusha hiyo agenda
kila wakati na kukwepesha isijadiliwe pia wanayajua wao. Ni dhahiri
tukiendelea na hawa watu tutafika 2015 tukiwa hatuna pesa hata ya kuweka
mawakala kwenye vituo na tutapigwa tukiwa tumesimama. Kwa kiasi kikubwa
mkuu aliyepo anatengeneza mazingira yaleyale ya mwaka 2005 na 2010 ya
kutaka chama kiwe hakina hela ili ikifika wakati wa uchaguzi kimpigie
magoti. Kisha atatoa pesa bila kumbukumbu zozote na mara baada ya
uchaguzi anapeleka lundo la deni na kudai alipwe hela aliyekikopesha
chama wakati wa uchaguzi. Alifanya hivyo katika chaguzi za 2005 na 2010.
Wakati wote wa kampeni za mwaka 2010, kwa mfano, taasisi yetu
ilihangaika sana kwa kukosa hata hela ya kununua maji kwa wajumbe wa
ngome. Lakini ajabu ni kwamba baada ya uchaguzi mkuu wa taasisi na
baadhi wa wapambe wake walilete deni kubwa la takribani shililingi
milioni mia tano akiadi kuwa walikikopesha chama. Taasisi imewalipa pesa
zote hizi kwa muda mwaka mmoja. Sasa anatengeneza mazingira hayohayo
kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka 2015.
Mipango ya kukipatia chama
mapato ya ziada kutoka nje ya chama. Wakuu waliopo hawana hata ndoto ya
namna ya kupata fedha za ziada. Wanachokijua ni kukusanya ‘sadaka’
kwenye mikutano ya hadhara na kuwapatia kazi watu wanaoonekana kuwa
matapeli eti waendeshe harambee za kuchangisha fedha kwa njia ya
matukio. Mawazo mazuri kama lile la kuanzisha kampuni la uwekezaji la
taasisi yetu litakalowekeza kwenye miradi mbalimbali, halijawahi
kufanyiwa kazi, na hivyo uanzishaji wa miradi mbalimbali ya kuiingizia
taasisi fedha imebaki ndoto ya mchana. Hatuwezi kufika hata siku moja
bila fedha. Hata uchaguzi wa wenzetu wa hapa jirani juzi juzi wakuu wetu
ingawa walishiriki lakini hawaonekani kama wamejifunza chochote.
Njia
haramu za kubaki madarakani. Ili kuhakikisha wakuu wanabaki madarakani,
wameanzisha vikundi vikundi ndani ya taasisi yetu. Siku hizi ni rahisi
sana kuambiwa kwenye taasisi yetu eti huyu ni wa boss na huyu ni wa
dogo. Na wale walio wa boss kwa kuwa boss ndo anashikilia raslimali za
taasisi anatumia mfumo haramu kuwaneemesha watu wake kwa kutumia
raslimali za taasisi na kuwakandamiza wote wanaoonekana wanapishana naye
kimtazamo. Jambo hili limewaibua wachumia tumbo, wapenda madaraka, na
vibaraka lukuki wanaokwenda kujipendekeza kwa wakuu wa taasisi kwa
malengo ya kujinufaisha binafsi. Katika kufanya hivyo vibaraka hao
wamekuwa wakiwaendea wakuu wa taasisi na kuwajaza maneno mabaya dhidi ya
viongozi wenzao na kuzidi kuwafarakanisha viongozi wa juu.
Kuna
mchezo umeanzishwa na wakuu wa taasisi unaitwa ulinzi wa chama
uliogawanyika katika makundi mawili yaani visible na invisible. Visible
ni ule unaoonekana ambao uko chini ya kikosi chetu chekundu ambacho
kinajulikana kwa kila mtu lakini invisible wanajulikana kwa mkuu wa
taasisi na mtendaji mkuu peke yake. Wanafanya kazi kwa maelekezo ya
wakubwa hao wawili na hawajulikani kwa viongozi wengine wa juu. Ni hawa
hawa ambao wanatumika vibaya pale wanapoleta taarifa za kiintelijensia
ambazo zinawahusisha viongozi wasiopendwa na wakuu na usaliti dhidi ya
taasisi. Hakuna kamati maalum inayowathibitisha maaintelijensia hao bali
wakuu wenyewe wanawachukua wanaowataka. Ni katika mfumo huu wa kipuuzi
mida eight amekuwa akitumika vibaya kwa kumshambulia mtendaji mkuu
msaidizi hadharani kwa kutumia mitandao ya kijamii na wakuu wanafurahia
na kumlipa pesa.
Udhaifu wa utendaji wa mtendaji mkuu. Mtendaji
mkuu ni dhaifu mno na ni mara nyingi sana tumeshuhudia mkuu wa taasisi
akifanya mambo ya kiutendaji kinyume na utaratibu kama vile yeye
mwenyewe kuja kwenye kamati ya makatibu na wakurugenzi na kupangua
mipango yao na ku-inject ya kwake na mtendaji mkuu kuadopt tu kana
kwamba yeye hawezi kupanga mambo ya kiutendaji, hata tunapokuwa kwenye
operesheni maalum tumeshuhudia mkuu wa taasisi ndo akipanga watendaji,
posho zao na hata kusimamia matumizi ya pesa na shughuli mbalimbali za
kiutendaji. Udhaifu wa mtendaji mkuu ni udhaifu wa mkuu wa taasisi kwa
kuwa amemteua yeye mara mbili tena mara ya pili alileta jina moja mbele
ya Baraza la juu kuonyesha kwamba aliridhika na utendaji wake kiasi cha
kutotaka kumpambanisha na mwingine. Lakini baada ya kumpendekeza mara ya
pili ndipo tumeshuhudia yeye kuingilia kati mara nyingi sana mambo ya
kiutendaji kana kwamba anamfichia aibu mtendaji wake. Swali kwa nini
alimteua tena? Jibu lake litakuwa rahisi tu kwamba ni kwa sababu
mtendaji huyu ni passivekwa kila takwa la mkuu wake.
Matumizi
mabaya ya madaraka yanayoweza kuhusishwa na ufisadi. Taasisi yetu inayo
kamati ya tenda ambayo iko chini ya kamati ya makatibu na wakurugenzi.
Lakini uzoefu unaonyesha kwamba kamati hii haifanyi kazi imezimwa kimya
kimya na wajumbe wote wa kamati ya tenda kwa kuwa ni wachumia tumbo
wanaojigonga kwa wakuu, wamekubali kuzimwa. Leo ikidaiwa kamati hiyo
ilete nyaraka za mchakato wa manunuzi ya magari, pikipiki, vifaa vya
kueneza taasisi, set ya televisheni iliyofungwa ofisini kwa mtendaji
mkuu, hawana. Manunuzi haya yote yote yanafanywa na wakuu hasa hasa mkuu
wa taasisi bila utaratibu wowote jambo ambalo ni hatari na
linarahisisha matendo ya kifisadi. Bila aibu, mkuu wa taasisi ndio
amekuwa mnunuzi wa vifaa vyote vya chama nje ya nchi kwa bei anayoijua
mwenyewe na ambaye haihojiwi popote. Huu ni mfano wa wazi wa mgongano wa
kimaslahi jambo ambalo ni hatari kwa kiongozi mkubwa wa taasisi kama
yetu inayojitambulisha katika kupinga vitendo vya ufisadi na uvunjifu wa
maadili ya uongozi kwa ujumla.
Makubaliano ya kifisadi na mtu
binafsi anayeuza vifaa vya kueneza taasisi. Hakuna kikao chochote cha
juu kilichojadili ama kilichowahi hata kupewa taarifa tu kwamba sasa
kuna mtu binafsi kapewa tenda ya kuuza vifaa vya taasisi na taasisi
inanufaika vipi na mauzo hayo na kwa nini vifaa muhimu vya taasisi
vinauzwa. Jambo hili linajulikana kwa wakuu tu.
Mifumo ya uteuzi
wa maofisa wa makao makuu ya taasisi imevurugwa na siku hizi wakuu wa
taasisi hasa mtendaji mkuu anateua na kutimua ofisa anavyotaka na mara
nyingi bila hata kamati ya makatibu na wakurugenzi kujua. Mambo haya
yanafanyika mbele ya macho na masikio ya mkuu wa taasisi jambo ambalo
linazidi kuthibitisha kwamba mkuu na mtendaji mkuu wanajuana na
wanafanya kwa kulindana.
NANI TUMUUNGE MKONO KUCHUKUA NAFASI YA MKUU:
Baada
ya utangulizi huo unaoonyesha kinagaubaga kwamba tunahitaji mabadiliko,
hatua iliyofuata ilikuwa ni kuangalia nani anaweza kuleta mabadiliko
tunayohitaji. Ni vema ikazingatiwa kwamba mtu ambaye tungemuunga mkono
lazima awe ni mtu mwenye uwezo mkubwa kuliko tunayetaka kumtoa. Awe ana
qualities za kiuongozi na zaidi sana awe na uwezo wa kupambana na mkuu
aliyeko. Tukileta mtu asiyefahamika sana kwenye mifumo ya taasisi yetu
hata kama angekuwa mzuri kiasi gani hatachagulika na mkuu aliyeko
atarudi kwa urahisi na kuendelea kuididimiza taasisi.
Katika
kuchunguza ndani ya taasisi tuliridhika kwamba mtendaji mkuu msaidizi
ana sifa zote tulizozitaja hapo juu ingawa kila mwanadamu ana udhaifu
wake. Ni dhahiri pia kwamba udhaifu wa mtendaji mkuu msaidizi
unarekebika kuliko wa mkuu aliyepo. Kwa ujumla mtendaji mkuu:
Ni kiongozi anayeweza kuongoza taasisi bila kujenga makundi akijali zaidi kazi ya taasisi kuliko maslahi binafsi.
Ameonyesha
kwa vitendo kwamba hana maslahi binafsi kwa kuwa tumeshuhudia akifanya
kazi nyingi za taasisi bila kudai malipo kwa njia ya posho ama
vinginevyo.
Anaheshimika na viongozi wa ndani na nje ya taasisi
jambo ambalo ni la muhimu sana kwa ustawi wa taasisi na kwa yeye kuwa
mkuu wa taasisi tunatarajia wakubwa wengi sana kutoka nje ya taasisi
yetu kuiamini na hata kujiunga nasi katika kuhakikisha tunafanikisha
lengo la taasisi.
Ni msomi wa kiwango cha juu na mwenye uwezo
mkubwa katika kuchanganua mambo ya kiuchumi, kisiasa, kijamii,
kimichezo, nk jambo ambalo ni muhimu sana kwa kuwa ni hatari kuwa na
kiongozi asiye na ujuzi wa kutosha kwenye masuala kama hayo.
Ndani ya taasisi anakubalika kwa makundi yote ya vijana, wazee na akina mama.
Uongozi
wa sasa wa taasisi yetu umefanya tuonekana kwamba taasisi yetu ipo kwa
ajili ya kuvuruga amani ya nchi. Yote hii ni kwa sababu tumekuwa hatuna
mbinu mpya za mapambano zinabadilikabadilika zaidi ya maandamano ya kila
mara. Kwa kuzingatia utamaduni wa watanzania wa kupenda amani, kuna
haja ya kufuta hii taswira na njia rahisi ni kubadilisha uongozi wa
taasisi haraka iwezekanavyo.
Uelewa wake wa mambo ya kiuchumi ni
muhimu sana kwa taasisi kwa sasa. Tunahitaji kuja na vyanzo vipya vya
mapato ikiwa tunahitaji kufanikiwa. Mkuu aliyepo si kwamba ameishiwa
bali hana mbinu za maana za kuiimarisha taasisi kimapato kwa ajili ya
malengo yake ya mbele.
Exposure kubwa na kukubalika katika siasa
za kimataifa. Tunahitaji kiongozi ambaye anazifahamu siasa za kimataifa
na anayeweza kuungwa mkono na viongozi wengi wa kimataifa. Ni hatari
kutegemea utaweza kufanikisha malengo kama ya taasisi yetu bila mpango
kabambe wa kuungwa mkono na jumuia ya kimataifa. Mpaka hivi sasa hakuna
mpango wowote wala hata mchakato wa maana kuwa connected na jumuia ya
kimataifa. Kiongozi wetu mkuu wa sasa yupo ‘too local’ na hana
mawasiliano yeyote ya maana na viongozi wengine katika kanda na
kimataifa. Ndio maana mkuu huyo na mtendaji wake mkuu wamekuwa
hawaonekani katika matukio makubwa ya kimataifa. Hata katika kutoa maoni
katika mambo makubwa ya kitaifa na kimataifa viongozi hawa hawapo. Kwa
kifupi kwa sababu ya aina ya viongozi tulio nao, nafasi ya taasisi yetu
katika nyanja za kimataifa haipo!
Aina na staili ya uongozi wa
sasa wa taasisi yetu ni kina kwamba nchi hii haipo hadi taasisi yetu
itakapochukua dola. Yaani tunafanya mambo kama kwamba tutaanza upya
kabisa tukichukua dola. Ni kwa sababu tumegombana na kila mtu katika
utawala wan chi, vikiwemo vyombo vya ulinzi na usalama. Ukweli ni kwamba
tutavihitaji vyombo hivi kabla na baada ya kuingia madarakani na ni
ndoto kudhani kwamba tutakabidhiwa nchi kwa kugombana na kila mtu. Ni
kwa sababu ya mtazamo kama huu ndio maana wakuu wetu wa sasa hawaonekani
kabisa katika shughuli za kitaifa kama vile sherehe za uhuru wan chi,
n.k.
Uwezo wa kuwaunganisha wasomi wa kada mbalimbali,
wafanyabiashara wakubwa, watumishi wa umma na sekta binafsi, nk katika
kupata muunganiko wa mawazo na kutoka na sera murua zinazogusa kila
sekta. Hili la kuwashirikisha litaenda sambamba na kutoa elimu kwa wote
waelewe na watuunge mkono. Tunasema hivi kwa kuwa watu wa kada
mbalimbali hawajaelewa sera zetu juu ya mambo yanayowahusu mfano
wafanyabiashara wakubwa, wawekezaji, wakulima, watumishi, wanafunzi,nk
na hivyo hawajawa tayari kutuunga mkono. Kile kinachofanywa wakati wa
uchaguzi kwa njia ya ilani ya uchaguzi na elimu kutolewa kwa njia ya
kampeni majukwaani hakitoshi. Tunahitaji watu wajue tumeunda think tank
kwa ajili hiyo na baadaye wajue nini kimetokana na think tank hiyo ili
wajadili na kutoa maoni na hatimaye tutoke na kitu kinachokubalikwa na
wananchi wote. Na tuna imani hilo tunayempendekeza ana uwezo nalo.
Kubwa
zaidi ni kwamba alishaiangalia taasisi yetu na kuona mambo yanayohitaji
mabadiliko na kujiangalia yeye na kuridhika kwamba ataweza kuleta
mabadiliko tunayoyahitaji na ndipo mwaka 2009 aliamua kujitosa kuutafuta
ukuu wa taasisi yetu kabla ya kuombwa kumwachia aliyepo.
SWOT ANALYSIS:
Kwa
kutumia uchambuzi huu hapa chini wa uimara, udhaifu, fursa na vitisho
ama vikwazo dhidi ya mtu tunayempendekeza, utaweza kutuonyesha kama
tunayempendekeza ataweza kushinda vita iliyo mbele yetu. Kama SWOT
inavyotaka, tutaangalia sifa njema alizonazo tunayemtaka ambao ndio
uimara wake, tutaangalia pia udhaifu wake, tutaangalia fursa alizonazo
na mwisho tutazingatia vitisho ama vikwazo vilivyopo. Ni muhimu
tukaeleza kwamba katika SWOT analysis tunajikita kwa mambo yanayohusika
moja kwa moja na uwezekano wa tunayemtaka, kuchaguliwa. Kwa hiyo kwa
mfano utakuta kwamba katika sehemu hii hatutazungumzia sifa njema
alizonazo tunayemtaka kama kiongozi lakini sifa hizo zikawa hazina
ushawishi wa kuwafanya wajumbe wa kikao cha uchaguzi kumchagua.
Uimara wa tunayemtaka:
Ingawa
si mmoja wa waasisi wa taasisi yetu, lakini ni mwana taasisi mkongwe
akiwa amejiunga na taasisi yetu miaka miwili tu tangu ianzishwe na mwaka
mmoja tangu isajiliwe rasmi na serikali.
Zaidi ya kuwa
mwanataasisi mkongwe, hajawahi kujiunga na taasisi nyingine hapo kabla.
Alijiunga na taasisi hii kabla hata haijajulikana kwa watu na alibaki
kuwa mwana taasisi mwaminifu hata pale taasisi zingine zilipoonekana
kuwa imara na maarufu zaidi ya hii.
Kutokana na vipengele ‘a’ na
‘b’ hapo juu, hakuna mtu hata mmoja anayeweza kusema mtu huyu alikuja
kwenye taasisi yetu kwa ajili ya kutafuta maslahi kama vile uwakilishi
kwenye chombo chetu kikuu cha uwakilishi hapa nchini.
Ni
mvumilivu sana. Katika jitahada za wakuu waliopo kuhakikisha wanaendelea
kukalia viti vyao, wamejitahidi sana kumpaka matope lakini amevumilia.
Mahali ambapo wengine wangeshakata tamaa na kuhama taasisi, yeye alibaki
kuvumilia mpaka imefikia wana taasisi wa ngazi za chini waliokuwa
wanadanganywa kwamba mtu huyu ni msaliti, wameanza sasa kushtuka.
Ana historia nzuri ya utendaji uliotukuka ndani na nje ya chombo cha uwakilishi.
Ana
uwezo mkubwa wa uelewa wa mambo mbalimbali ya uchumi, jamii, utamaduni,
michezo, nk. Uwezo wake unachagizwa si tu na elimu yake ya darasani
bali pia vipaji na akili ya kuzaliwa.
Ni mzalendo wa hali ya juu
anayeipenda nchi yake kwa moyo wa dhati. Amethibitisha hilo kwa namna
anavyolitetea taifa letu katika medani za kimataifa na jinsi
anavyolipigania ndani dhidi ya mafisadi na wasiolitakia mema taifa letu.
Ni mwakilishi pekee aliyekuwa tayari kukosa mishahara ya miezi kadhaa
kwa kuamua kusimamia ukweli kwamba kuna ufisadi ulifanyika mpaka
akasimamishwa uwakilishi wake kwa mikutano kadhaa ya chombo chetu cha
uwakilishi.
Katika kuzidi kuonyesha alivyo mzalendo tunaweza
kusema hapa kwamba ni kiongozi pekee kutoka upande huu ambaye ameonekana
sana kwenye mambo ya kitaifa kwa mfano kulipigania taifa letu katika
mambo ya kimchezo, kutumia gharama zake kwenda nje ya nchi na kujifunza
mambo mbalimbali yanayoweza kulisaidia taifa katika sekta nyeti kama
mafuta, gesi na madini, nk bila kusahau kwamba amekuwa ndiye mwakilishi
pekee aliyeongoza katika kuibua kashfa nyingi na nzito za ubadhirifu
ndani ya serikali hata kufikia mawaziri kadhaa kufukuzwa kazi.
Mambo
hayo tuliyoyataja kwenye vipengele ‘e’, ‘f’, ‘g’ na ‘h’ yamemfanya kuwa
kiongozi wa kwanza kuwa maarufu sana katika taasisi yetu aliyewapiku
hata viongozi wa serikali kwa umaarufu. Hii ya umaarufu ni sifa muhimu
sana linapokuja suala la uchaguzi.
Uwezo wake wa kujieleza kwa
kujenga hoja pale anapopewa nafasi. Hata pale anapokuwa amepakwa sana
matope na wenzake, anapopewa nafasi ya kujieleza huweza kuwashawishi
watu wengi wanaomsikiliza. Hii itamsaidia sana siku ya kujieleza mbele
ya kikao cha uchaguzi ambapo ataweza kupangua hoja zote dhaifu za
kumpaka matope.
Ana uwezo wa kuchangamana na makundi yote ambapo
vijana humwona kama mwenzao, wanawake humwona kama mtetezi wao wakati
wazee humwona kama kijana mwenye busara anayeweza kuelekeza kama
kiongozi.
Ana mahusiano mema na mazuri na viongozi wa ngazi za
chini kutokana na ziara nyingi alizozifanya na kukutana na viongozi wa
ngazi za chini akiwa katika kuijenga taasisi hii. Mahusiano haya mazuri
yanachagizwa na jinsi anavyotumia muda wa kuongea na viongozi wa ngazi
za chini kuzungumza kwa lugha ya upole na kuelekeza viongozi wenzake
bila kuwaonyesha dharau.
Si mtu wa kujipenda nafsi na katika
kupambana umaskini wa watu badala ya umaskini wake, alifikia kuzikataa
posho wanazolipwa wawakilishi wakati wakitekeleza majukumu ambayo kwayo
wanalipwa na kuiomba ofisi ya chombo hicho kuzipeleka posho hizo kwa
watu maskini.
Ana limu nzuri sana aliyoipata katika vyuo vinavyoeleweka kitaifa na kimataifa
Ni kijana na hii ni taswira njema kwa sababu taasisi yetu inaungwa mkono sana na vijana
Udhaifu wa tunayemtaka:
Maneno
yake mara nyingine hayazingatii anayazungumza katika mazingira gani na
hivyo kuwasha masikio ya wanataasisi jambo linalompunguzia kukubalika
kwake taratibu.
Kama ilivyo kwa maneno, kuna matendo pia ambayo
mara nyingine huyafanya bila kuzingatia mazingira na wasikilizaji wake
na hivyo kupunguza imani ya wana taasisi kwake.
Hali ya ndoa ya tunayemtaka kutoeleweka msimamo wake
Kuna
wakati tunayemtaka hu-respondkwa taharuki kubwa dhidi ya mashambulizi
yanayoelekezwa kwake jambo linalomfanya achukue maamuzi yasiyo sahihi
kwa wakati huo. Kwa kifupi kuna wakati tunayemtaka huonekana kufanya
maamuzi kwaemotion zaidi badala ya kutulia kwanza na kutafakari kwa kina
ikiwa ni pamoja na kutafuta ushauri kwa wenzake kabla ya kurespond.
Jambo
lililoelezwa katika ‘d’ hapo juu humfanya tunayemtaka wakati mwingine
kuonekana ana jazba sana kwa sababu akishataharuki na kuchukua maamuzi
akingali kwenye taharuki huwa ni rahisi sana kuonekana anajibu mapigo
kwa jazba sana.
Ustahimilivu: yaliyotajwa katika ‘d’ na ‘e’ hapo juu yanaashiria tunayemtaka si mstahimilivu sana sifa ambayo inahitajika sana kwa kiongozi.
Uwazi: Katika
taasisi zetu hizi ni muhimu sana kuepuka kufanya mambo yote wazi wazi
hata kama ni mema ama ni haki ya mhusika ama si makosa katika jamii
tuliyomo. Kuna mambo ambayo ni haki ya mtu mfano mahusiano binafsi ya
kimapenzi, kuwa na marafiki wa damu kutoka upande mwingine wa utawala,
nk. Lakini mambo hayo ni muhimu wakati mwingine ama kwa kiwango fulani
yakafanywa kwa siri kuepuka mitazamo potofu kwa unaowaongoza.
Fursa alizonazo tunayemtaka:
Utamaduni
wa taasisi yetu wa kubadilisha wakuu wa taasisi kila baada ya vipindi
vifupi ili kuleta maono mapya kwenye taasisi unampendelea tunayemtaka.
Udhaifu
ulioonyeshwa na uongozi uliopo chini ya mpinzani wetu katika kutekeleza
program mbalimbali za taasisi nyingi zikiwa zimebuniwa na wao wenyewe,
pia ni fursa kwa tunayemtaka.
Udhaifu mkubwa ulioonyeshwa na
uongozi uliopo kwenye ugawanyaji wa raslimali za taasisi kama vile fedha
za ruzuku, michango mbalimbali ya wahisani na hata vifaa vya uenezi.
Kujitokeza
kwa tunayemtaka kutaonekana kama fursa kwa wanataasisi kufanya
mabadiliko makubwa na kuua kabisa ile propaganda ya kwamba taasisi yetu
ni ya kabila fulani ama eneo fulani kwa kufanya reference kwa uongozi wa
taasisi.
Hoja ya uongozi uliopo kushindwa kabisa kusoma taarifa
za fedha tokea 2010 ikifahamika kwa wapiga kura inaweza kuwa machinjio
kabisa ya uongozi uliopo na kumpa fursa kubwa tunayemtaka.
Imani
ambayo wana taasisi wengi wanayo kwake. Utafiti mdogo unaonyesha kwamba
bado jina la tunayemtaka linatamkika sana midomoni mwa wanataasisi pale
wanapotajwa viongozi wa juu wa taasisi yetu. Hii inaonyesha bado wana
taasisi wanayo imani kubwa kwake na kwa hiyo atakapopata fursa ya
kupangua matope aliyopakwa atakuwa na nafasi kubwa ya kuchaguliwa.
Mpinzani
wetu hana historia nzuri ya utendaji uliotukuka ndani na nje ya chombo
cha uwakilishi. Hakuonyesha utendaji wowote wa pekee alipokuwepo kwenye
chombo mwaka 2000 -2005 na hata alipopewa uongozi wa upande wetu ndani
ya chombo tokea 2010 hadi leo 2013 hajafanya lolote la kutukuka ndani ya
chombo hicho.
Mpinzani wetu hana uwezo mkubwa wa uelewa wa mambo
mbalimbali ya uchumi, jamii, utamaduni, michezo, nk. Si tuelimu yake ya
darasani ni ya magumashi bali pia vipaji na akili ya kuzaliwa
havijaonekana katika maisha yake.
Uzalendowampinzani wetu unatia
shaka akiwa hajaonyesha lolote la maana katika kulitetea taifa letu
kimataifa. Ingawa ameshapata nafasi lukuki ya kwenda nje ya nchi lakini
mara zote akifika huko ni kuiponda tu nchi yake. Ingawa anayo majukwaa
ya kufanya hivyo akiwa ameshakuwa mwakilishi mara mbili kwenye chombo
chetu lakini hatujawahi kumsikia akiibua kashfa mahsusi ya ufisadi na
kuisimamia zaidi ya yeye mwenyewe wakati fulani fulani kutuhumiwa kwa
ufisadi mfano pale alipokopa kwenye shirika la umma na kugoma kulipa
mkopo.
Katika kuzidi kuonyesha uzalendo hafifu wa mpinzani wetu
tunaweza kuangalia jinsi ambavyo mpinzani haonekani kwenye mambo ya
kitaifa. Hii ni fursa kwa tunayemtaka.
Mpinzani wetu si maarufu
akilinganishwa na tunayemtaka na hivyo kumpa fursa zaidi tunayemtaka
kumshindani mpinzani wetu kwenye uchaguzi.
Uwezo wa mpinzani wetu wa kujieleza kwa kujenga hoja pale anapopewa nafasi ni mdogo sana.
Mpinzani
wetu hajazoea ushindani na changamoto. Ni mtu aliyezaliwa kwenye
utajiri na anadhani pesa ni kila kitu. Ukimnyang’anya pesa ukamwambia
ashindane kwa hoja hawezi na ndo maana anajaribu sana kuhakikisha
anaingia mwenyewe ulingoni bila kupingwa.
Kutokana na
tuliyoyasema hapo juu kwenye ‘m’ ni dhahiri kwambapale mpinzani wetu
anaporushiwa kombora la kashfa anakuwa mzito kujieleza hata kama anapewa
nafasi ya kufanya hivyo na hii ni fursa muhimu kwa tunayemtaka.
Mpinzani
wetu ni mgumu sana katika kuchangamana na makundi yote ambapo vijana
humwona kama si mwenzao kiumri na kifedha, wanawake humwona kama malaya
anayependa kutumia miili yao kujistarehesha wakati wazee humwona kama
mtu anayedhalilisha hata nafasi aliyopewa kwa kufanya uhuni waziwazi
hata kuvunja ndoa si ya kwake tu bali hata za watu wengine.
Mpinzani
wetu hana mahusiano mema na mazuri na viongozi wa ngazi za chini
kutokana na dharau nyingi anazozionyesha pale anapokukutana na viongozi
wa ngazi za chini akiwa katika kuijenga taasisi hii. Hutumia muda mwingi
kuwaponda viongozi wenzake hata kufikia kutamka mara nyingi kwamba kama
kiongozi hawezi kujigharamia nauli na malazi ya kutoka mahali fulani
kwenda mahali fulani kwa siku kadhaa hafai kuwa kiongozi bila kujali
kwamba kuna viongozi wetu wana moyo na taasisi hii na ndo wameifikisha
hapa ilipo lakini hawana uwezo wa kifedha na hivyo kauli kama hizo za
mkuu huyu huona kama anawadharau kwa kuwa yeye ni tajiri. Hii imemfanya
kutopendwa na viongozi wengi wa ngazi ya chini hivi sasa na kutoa fursa
ya pekee kwa tunayemtaka.
Mkuu aliyepo amekuwa na mkakati unaoitwa
kuondoa watu wa zamani. Jambo hili linawaudhi sana viongozi wa ngazi za
chini ambao wanaona kama baada ya kuifikisha taasisi mahali ilipo kwa
sasa wanaonekana hawana maana tena. Wengi wamefikia kuapa kwamba kama
mwendo ni wa kuwaondoa watu wa zamani basi na yeye ni wa zamani lazima
aondoke.
Mpinzani wetu amejionyesha dhahiri kujipenda na kujijali
nafsi bila kujali watu wa hali ya chini. Matukio mawili yanamwacha uchi
katika hili pale alipolitangazia taifa kwamba wawakilishi wetu wote
hawatachukua posho za vikao halafu yeye na wengine wote wanazichukua
hadi leo na kumwacha mtendaji msaidizi peke yake. Na la pili
linalofanana na hilo ni pale alipotangaza kutotumia gari la serikali
ambalo ni la kifahari kisha akalirudia kimya kimya.
Kuwepo
muhtasari wa kikao cha wazee ambacho mwaka 2009 kilimshauri tunayemtaka
ajitoe na kumwachia mkuu aliyepo na kumtaka mkuu aliyepo kumwachia
tunayemtaka katika uchaguzi ujao na wote wakasaini makubaliano hayo,
nayo ni fursa muhimu sana kwa tunayemtaka.
Mkuu aliyepo anaamini
kwamba ameshamsambaratisha tunayemtaka na hivyo kwa sasa amebweteka na
hiyo inatupatia sisi fursa kuendelea kuimarisha mtandao wetu.
Kwa
kuwa ni mwislamu. Hii ni fursa katika kupata kuungwa mkono na wanachama
waislamu ambao wamekuwa na kigugumizi wakidhani waislamu hawatakiwi
katika uongozi wa taasisi yetu.
Elimu ndogo na duni aliyenayo
mpinzani wetu ambaye ndiye mkuu wa taasisi yetu kwa sasa. Kwa sasa ni
kiongozi pekee katika nchi yetu anayeongoza taasisi kubwa asiye na elimu
ya shahada huku taasisi yetu ikiwa inaongoza kwa kuwa na wasomi
waliobobea katika kila nyanja. Hii ni kejeli hasa kwetu sisi ambao
tumekuwa tukiwasema wenzetu kwamba ‘akili ndogo’ inaongoza akili kubwa.
Kimsingi tumekuwa tukijisema kwa kukubali kuongozwa na mtu mwenye akili
ndogo.
Mkuu wa sasa kutokuwa na msimamo thabiti katika mambo ya
msingi. Rejea swala la maandamano ya kumshinikiza Kawambwa ajiuzulu na
kujitoa katika mchakato wa katiba.
Vikwazo dhidi ya tunayemtaka:
Sisi
wenyewe tunaoandaa mkakati huu hatuna uhakika kama tunayemtaka yuko
tayari na yuko serious na business hii, na kwa hiyo huenda tusifanye kwa
nguvu zetu zote ikiwa hatutapata nafasi mapema ya kukutana na mhusika
na akatuhakikishia kwamba yuko serious.
Utayari wa mhusika mkuu
kutekeleza yale tunayokubaliana. Inapotokea baada ya kukubaliana sisi na
yeye akapata ushauri tofauti na ukauona uko more genuine, basi
tuwasiliane kwamba nimeshawishika kufanya hivi badala ya vile
tulivyokubaliana kwa sababu hizi ama zile. Hii haitatukatisha tamaa
tofauti na kama tutakuwa tunapanga hivi halafu yeye anafanya vile bila
maelezo yoyote
Kitendo cha mkuu aliyepo kung’ang’ania kuendelea nayo
ni kikwazo kwa kuwa baada ya kuwa madarakani kwa miaka yote hiyo lazima
amejipatia watu wanaomhusudu ama kumpenda ama kumkubali na kuwepo
wengine wanaoogopa tu kwamba mkuu aliyepo akitoka taasisi itakufa hata
kama hawana sababu yoyote.
Tunatazamia mkuu aliyepo atafanya
vitendo vingi zaidi vya haramu katika kumdhibiti tunayemtaka pale
tunapoelekea kwenye uchaguzi wenyewe.
Raslimali za taasisi
kutumiwa na viongozi waliopo katika kumsaidia mkuu aliyepo wakati wa
kwetu anatumia raslimali zake za mfukoni.
Propaganda chafu zilizokwishapigwa dhidi ya tunayemtaka zimepunguza imani ya wanataasisi kwa tunayemtaka kwa kiasi fulani
Baadhi ya mambo ambayo amekwishayasema ama kuyatenda nayo yameshawapunguzia imani kiasi fulani wanataasisi mbalimbali.
Kutoonekana sana kwenye operations za taasisi yetu pia kumewapa wasiwasi baadhi ya wanataasisi.
Muhtasari
wa SWOT analysis unaonyesha kwamba strength na opportunities za
tunayemtaka ni nyingi sana zikilinganishwa na weaknesses zake na threats
dhidi yake. Aidha ukichambua zaidi utaona kwamba weaknesses za
tunayemtaka nirepairable na vikwazo dhidi yake pia ni rahisi kuvikabili
na kuvisambaratisha. Tukishamaliza maandalizi ya mkakati huu tukaonana
na mhusika mkuu na kumpa ushauri akatulia na kufanya kazi, mkuu aliyepo
hatafua dafu. Tunahitaji kutekeleza mkakati huu kwa siri kubwa ili mkuu
aliyepo aendelee kubweteka na ndiyo maana hata lugha iliyotumika ni
ndani hapa ni ya pekee. Tunahitaji tunayemtaka asionekane kama kuna kitu
anafanya na tunafurahi kwamba kuna wakati alitangaza kwamba hana nia ya
kugombea tena waliopo wanatosha. Ikitokea vyombo vya habari vikamuuliza
tena hiyo ndiyo iwe kauli yake ili kuendelea kumfanya mkuu aliyepo
asihangaike na hivyo kuja kummaliza kirahisi. Aidha katika utekelezaji
wa mkakati kama tutakavyoeleza hapo baadaye, tunayemtaka atajitenga
mbali asionekane hata kuwa karibu na sisi. Vikao vyetu na yeye
vitafanyika mara chache sana na mahali pa faragha kupita kiasi
ikiwezekana hata nchi jirani.
Mkakati huu hautatakiwa kupatikana
kwenye komputa zaidi ya tatu yaani ya mchapaji ambaye ni M3, ya M3 na ya
MK mwenyewe. Hata hivyo email zitakazotumika kusafirisha mkakati huu
kutoka kwa M3 kwenda kwa M1 hadi kwa MK hazitakuwa zile za kawaida za
hao watu bali mpya kabisa zilizofunguliwa kwa makusudi haya tu na kwa
majina fictitious. Aidha kila atakayekuwa na mkakati huu kwenye computer
yake anatakiwa kuliwekea file hilo password ili hata mtu wa karibu naye
anayeweza kufungua computer yake asiweze kulifungua file hilo. Pia
email address hazitatolewa kwa sms bali kwa kupiga na kuambiana spelling
za address.
MTANDAO WA USHINDI:
Mtandao
wa ushindi utakuwa kama ifuatavyo. Kwenye ngazi ya kitaifa tutakuwa na
kamati yenye members watatu tu. M1 ndiye atakayekuwa anawasiliana na
tunayemtaka ambaye ataitwa MM (Mhusika Mkuu). Tumepanga kwamba kusiwe na
mawasiliano mengi kati ya kamati na mhusika mkuu kuepuka tracking ya
wapinzani wetu. M1 ni mtu wa karibu na MM kwa hiyo mawasiliano yao
hayataweza kutiliwa shaka na mtu yeyote hata wangewasiliana mara nyingi
kiasi gani. Hata hivyo, linapokuja suala la mkakati huu tunasihi
mawasiliano yawe kwa kuonana uso kwa uso ama kwa simu na si sms. M1
ndiye atakayewasilisha mambo yote yanayotoka kwenye kamati ya kitaifa na
endapo kuna haja ya MM kukutana na kamati ya kitaifa, mipango yote ya
kikao itafanywa na M1 kwa usiri mkubwa. M2 ni mtu ambaye yuko kwenye
ofisi kuu za taasisi yetu wakati M3 ndiye mchapaji wa mkakati huu.
Kamati
hii imefanywa kuwa na members wachache sana wenye uelewa mpana wa mambo
na wenye elimu nzuri ili kuhakikisha kazi inafanyika kitaalam na kwa
uhakika sana. Kamati ya kitaifa itapeleka mapendekezo yake kwaMM na yeye
pia ataleta ushauri wake kwa kamati kama mishale inavyoonyesha. Chini
ya kamati ya kitaifa kutakuwepo waratibu wa kanda zote kumi
watakaojulikana kama MK1 – MK10. Hawa watatafutwa na kusimikwa na kamati
ya kitaifa kwa kushauriana na MM kwa utaratibu utakaokubalika na pande
zote yaani MM na kamati ya kitaifa. Chini ya waratibu wa kanda
kutakuwapo waratibu wa mikoa yote 30 (MMK1 – MMK30) ambao watapatikana
kwa utaratibu ule ule wa kuwapata waratibu wa kanda. Isipokuwa pale
ambapo inakuwa ngumu, itabidi kamati ya taifa isaidiane na waratibu wa
kanda kuwapata waratibu wa mikoa lakini kamati itashauriana na MM kabla
ya kuwasimika rasmi hao waratibu wa mikoa.Mtandao utakuwa kama
inavyoonyeshwa kwenye mchoro ufuatao:
NAMNA YA KUFANIKISHA MKAKATI:
Kazi itagawanywa katika awamu tatu:
Awamu
ya kwanza ni kuanzia sasa mpaka uchaguzi wa ngazi ya matawi
utakapoanza. Katika awamu hii kazi ni kuhakikisha kwamba mtandao mzima
umekamilika mpaka kwenye ngazi ya mkoa. Kazi nyingine itakayofanyika ni
kwa waratibu wa mikoa kuendelea kuspot makada kwenye wilaya na mikoa
ambao tayari wana mtazamo tulio nao ama ambao wanaweza kuingiziwa
kirahisi mbegu hii ya mabadiliko na wakawa tayari na wana uwezo na sifa
za kushinda uongozi kwenye wilaya na mikoa yao bila kusahau sifa ya kuwa
waaminifu wenye uwezo wa kutunza siri. Kulingana na muda hii ni kazi
inayotakiwa kufanyika sasa lakini kwa uangalifu mkubwa. Ni muhimu
kukumbushana hapa kwamba katika awamu hii hakuna anayetakiwa kujua
mpango mzima zaidi ya kamati ya kitaifa na MMili kuhakikisha uwezekano
wa mkakati wetu mapema kwa wapinzani wetu unakuwa minimized to almost
zero.
Awamu ya pili ni kipindi kuanzia uchaguzi wa matawi mpaka
uchaguzi wa mikoa unapokamilika. Katika awamu hii tutasaidiana na
waratibu wa kanda na mikoa kuhakikisha makada tuliowaspot kwenye wilaya
wanapanga safu zao kwenye kata ili kuhakikisha watakaochaguliwa kwenye
kata ni watu wao ili waje wawachague kwenye wilaya.Vivyo hivyo kwa
makada tuliowaspot kwenye mikoa wahakikishe wanaochaguliwa kwenye wilaya
ni wale makada wetu ili nao waje wawachague kwenye mikoa yao. Hapa
ndipo kwenye kazi kubwa ya mkakati wetu na hapa ndipo tutakapohitaji
kuingia gharama zaidi kwa ajili ya kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa
kwa asilimia angalau 80.
Awamu ya tatu ni kuanzia baada ya
kukamilika kwa uchaguzi wa mikoa hadi uchaguzi wa kitaifa
utakapoitishwa. Katika kipindi hiki kwa ustadi mkubwa tutakuwa
tukiwaandaa makada wetu waliochaguliwa tayari kuja kufanya mabadiliko
makubwa kitaifa. Ni wakati huu ambapo tutawaingizia mkakati taratibu
lakini kwa ustadi mkubwa tukijikita hasa kwenye kuonyesha kwa nini
tunahitaji mabadiliko. Ni katika kipindi hiki ambapo kwa ustadi mkubwa
tunaweza kuwaspot wale waliochaguliwa ambao hatukuwaandaa na kuwaingizia
pia mbegu ya mabadiliko ili kuwawin na kuwarecruit kwenye mkakati.
Aidha
katika awamu zote tatu kazi ya kuianalyze ofisi kuu itakuwa non stop
kwa kuzingatia kwamba mabadiliko ya wakurugenzi na maofisa yatakuwa
yanatokea na watu nao watakuwa wanabadilika kimtazamo. Analysis ya ofisi
kuu ni kuhakikisha tunajua nani na nani wako na sisi na nani na nani
wako against na pia nani na nani wanaweza kupandikiziwa mbegu kwa ustadi
na wakaungana nasi.
MAHITAJI YA KUFANIKISHA MKAKATI:
Raslimali
watu. Tunahitaji watu waaminifu watatu kwenye ngazi ya kitaifa ambao
tayari wapo. Tunahitaji watu waaminifu kumi kwenye kanda ambao
tutawatafuta na pia waaminifu wengine 30 kwenye mikoa yote thelathini.
Fedha.
Tunahitaji fedha kwa ajili ya mawasiliano kati ya wanakamati na wale wa
ngazi ya chini. Aidha tunahitaji fedha kwa ajili ya gharama za usafiri
pale tutakapohitaji kwenda kwenye kanda na mikoa husika kwa ajili ya
kusimika watu hao tunaowahitaji.
MAPENDEKEZO MAHSUSI NA HITIMISHO:
Katika kuhitimisha tunapendekeza mambo mahsusi yafuatayo:
Kuhusu Bajeti:
Tunapendekeza
kwamba bajeti ya mkakati huu isipangwe hivi sasa. Ni muhimu tu sote
kuelewa kwamba wakati wenzetu wanatumia raslimali za taasisi kujijenga
na kutekeleza mkakati wao wa ushindi, sisi tunapaswa kuingia mifukoni.
Kwa kila kila mmoja wetu atakuwa budget conscious ili kuepuka matumizi
makubwa ya pesa. Hata hivyo, kwa kuzingatia kwamba lazima pesa
inahitajika ni muhimu M1 na MM kujaribu kuangalia namna ya kuraise pesa
na kushauri. Otherwise, tutakapokuwa tunahitaji kufanya hatua yoyote ama
jambo lolote tutakuwa ndo tunapiga hesabu za funds tunazohitaji kwa
jambo husika na kuingia katika utekelezaji.
Kuhusu mwenendo wa MM kuanzia sasa:
Ni
maoni yetu pia kwamba kuanzia sasa MM aenende katika mwenendo ambao
utarahisisha ushindi. Mfano tunapendekeza afanye yafuatayo kuanzia sasa:
Apunguze ukaribu na viongozi wa serikali na wa chama tawala na awe crical zaidi na utendaji wa serikali nje na ndani ya bunge.
Ashiriki kikamilifu katika shughuli za taasisi yetu zikiwamo vikao vyote vinavyomhusu, operesheni mbalimbali, chaguzi ndogo, nk.
Aendelee
kushusha ‘nondo’ ndani ya chombo chetu cha uwakilishi na kuendelea kuwa
juu ya wawakilishi wengine katika hoja mbalimbali zenye maslahi ya
kitaifa.
Ajitahidi kudhibiti jazba hata pale anapokuwa
amebambikiziwa tuhuma nzito namna gani. Atulie, ashauriane na wazee ili
kuona namna nzuri ya kujibu tuhuma zinazomkera. Tukumbuke kwamba wakati
mwingine kukaa kimya ni jibu zuri zaidi kuliko hoja nzito.
Sambamba
na ‘iv’ hapo juu, adhibiti sana emotion ili kuhakikisha kila kitu
kinachofanywa ama kuzungumzwa kinachomgusa asikimbilie kuongea na vyombo
vya habari ama kwenye mitandao ya kijamii bali afuate kile
tulichokizungumza kwenye kipengele cha ‘iv’ hapo juu.
Kuhusu mapambano ya kuchafuana kwenye mitandao ya kijamii:
Katika hili sisi hatukuona haja ya kufanya hivyo kwa sababu mbili:
Imani
yetu kwamba taasisi yetu ni kubwa kuliko watu kwa hiyo ni muhimu
kuzingatia kwamba hatuiui taasisi katika mapambano haya. Tukiendekeza
mashambulizi kwa njia ya mitandao ya kijamii hatutakuwa na ngao ya
kuwakinga watu wa kawaida (wanataasisi na wasio wanataasisi) dhidi ya
kujikuta wakiamini kwamba taasisi hii nayo haina jipya ni sawa tu na ile
tunayotaka kuitoa.
Tutakuwa tumeiua taasisi na mkakati huu
hautakuwa na maana sana kama lengo ni kufanya mabadiliko ya uongozi wa
taasisi tu lakini malengo ya taasisi ya mwaka 2015 yasitimie!
Kujikita
kwenye mashambulizi kupitia mitandao ni kuzidi kuwashtua wakuu waliopo
kwamba bado tuko serious na mkakati wa kuwatoa na kuwafanya wafanye kazi
zaidi huku wakiendelea kumpaka matope MM kwamba ndiye anayerusha
makombora hayo kwenye mitandao kwa kusudi la kuhujumu taasisi maana hiyo
ndo lugha yao. Hatukatai kwamba wakuu wanajua kabisa kwamba bado MM ana
nia ya kumvaa mkuu aliyepo lakini tunajua kwamba kwa sasa wanaamini
wamemdhoofisha na hana madhara tena. Ndiyo maana tunataka kutekeleza
mkakati wetu kwa siri sana ili wafikiri MM amekata tamaa kumbe ndo
anakuja na mkakati mzito zaidi.
Hata hivyo, ni muhimu
kukumbushana kwamba wenzetu hawatanyamaza kwa sababu eti sisi tumeacha
kuwashambulia kwenye mitandao ya kijamii. Lazima wataendelea!
Wataendelea kumchafua MM kwa kupitia wapuuzi kama yule kichaa wa ‘ars’
na kundi lake. Nini tutakuwa tunakifanya sasa? Tutahakikisha tuko busy
kupost mambo mema na mazuri yatakayokuwa yakifanywa na MM kila wakati na
kuzidi kusambaza sifa zake njema kila inapotokea nafasi. Atakayefanya
kazi hiyo ni sisi wengine wala si yeye! Pia tutahakikisha kila post ya
kumchafua inapatiwa majibu bila kutumia ID yake inayojulikana. Ni vema
aidha akatupatia majibu na sisi kuyapost ama afungue ID mpya kabisa
ambazo hazijawahi kuwepo kwenye mitandao halafu ndo awe anazitumia
kujibu lakini kwa kuzingatia tuliyokwishayazungumza hapo juu yaani
kutofanya kwa emotion na kuepuka jazba lakini pia kushauriana na watu wa
karibu kabla ya kutoa majibu kwa jambo lolote linalomhusu.
Kuhusu kamati ya kitaifa (hususan M2 & M3):
Tulikubaliana
kwa kauli moja kwamba katika kutekeleza mkakati huu tunahitaji members
hawa wawe wametulia kimaisha. Inakuwa vigumu kwa mfano kumtaka member
aende mahali fulani kwa makusudi ya mkakati huu wakati hajui familia
yake nyumbani anaiacha inakula nini. Tuliona kwamba M3 tayari hana kazi
kwa sasa tena kwa kufanyiziwa na wakuu waliopo. Ni katika mwendelezo huo
huo tunamwona M2 naye akiwa ukingoni kupigwa nje na kuachwa mtupu na
wakuu waliopo katika kile wanachokiita wao reshuffle ya ofisi kuu. Kwa
sababu hiyo tukapendekeza kwamba MM kwa kushirikiana na M1 kwa hatua ya
kwanza wanaweza kutafuta kiasi cha sh. 2m kila mmoja tukijua kwamba kama
members hawa wawili wakisaidiwa milioni mbili mbili wanaweza kuanzisha
projects ambazo zitawasustain hata kama hawana ajira. Kwa hatua ya
baadaye tutasaidiana kuona kama hawa members wanaweza kusecure good
employments mahali, provided hazitawazuia kufanya siasa.