Wakati
Rais Jakaya Kikwete akikutana na viongozi wa vyama vya siasa
vinavyounda Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) ili kuzungumzia mchakato
wa Katiba, Jukwaa la Wakristo Tanzania (TCF), limesema amani ya nchi
iko mikononi mwa kiongozi huyo mkuu wa nchi.
Kwa
maana hiyo viongozi wa vyama vya siasa hasa vile vinavyounda Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa) wanatarajiwa kusafiri hadi Dodoma kumfuata
Rais Kikwete ambaye leo anaingia katika siku ya tatu ya ziara yake
mkoani hapa, iliyoanza juzi katika Wilaya ya Kongwa.
Baadhi
ya viongozi ambao wanatarajiwa kushiriki mkutano huo ni Katibu Mkuu wa
CCM, Abdulrahman Kinana, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe,
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na Mwenyekiti wa NCCR
Mageuzi, James Mbatia.
Pia katika orodha hiyo wamo Mwenyekiti wa TCD ambaye pia ni Mwenyekiti
wa UDP, John Cheyo, Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema na mwakilishi wa
vyama visivyo na wabunge ndani ya TCD ambaye pia ni Mwenyekiti wa UPDP,
Fahmi Dovutwa. Ukiondoa Kinana, viongozi wengine ni wajumbe wa Bunge
Maalumu.
Habari zilizopatikana juzi na jana Dar es Salaam na Dodoma na
kuthibitishwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu, Salva Rweyemamu
zinasema mkutano huo umepangwa kufanyika leo jioni baada ya Rais Kikwete
kuhitimisha ziara yake katika Wilaya ya Chamwino na unaweza kuendelea
hadi usiku kutokana na jinsi ratiba ilivyokaa.
“Mkutano
utafanyika hapa Dodoma katika muda wa saa 48 kuanzia sasa na Rais
hatakutana na Ukawa kama ambavyo imekuwa ikidaiwa, anakutana na viongozi
wa vyama vya siasa,” alisema Rweyemamu jana mchana.
Mwanzoni mwa wiki hii, Cheyo aliwaambia waandishi wa habari mjini
Dodoma kuwa Rais Kikwete alikuwa amekubali kukutana na viongozi wa vyama
vya siasa wiki hii ili kuzungumzia mustakabali wa Katiba. Hata hivyo,
alipoulizwa jana siku ya mkutano pamoja na mahali utakapofanyika, Cheyo
hakuwa tayari kuzungumza chochote.
Mkutano huo wa Rais na viongozi hao umekuja wakati ambao kamati za
Bunge Maalumu zimekamilisha uchambuzi wa Rasimu ya Katiba, bila kuwapo
kwa wenzao wanaokaribia 120 ambao walisusia mchakato huo tangu Aprili
16, kutokana na kile walichodai kuwa ni kutoridhishwa na mambo
yanavyokwenda.
Mara kadhaa Ukawa wamesisitiza kwamba kamwe hawatarejea bungeni hadi
pale masharti yao yatakapotekelezwa na CCM kikishikilia msimamo wake
kwamba masuala yote yanayohusu Katiba Mpya lazima yatatuliwe ndani ya
Bunge.
Kwa kuzingatia mazingira hayo ni dhahiri kwamba matokeo ya kikao hicho yanasubiriwa kwa shauku kubwa kwani yanaweza kusaidia kukwamua mchakato wa Katiba ambao umekosa uhalali wa kisiasa kutokana na Ukawa kuususia.
Kwa kuzingatia mazingira hayo ni dhahiri kwamba matokeo ya kikao hicho yanasubiriwa kwa shauku kubwa kwani yanaweza kusaidia kukwamua mchakato wa Katiba ambao umekosa uhalali wa kisiasa kutokana na Ukawa kuususia.
Mzigo wa amani
Wakati
hayo yakiendelea Jukwaa la Wakristo Tanzania (TCF) limetoa tamko kali
kuhusu mchakato wa Katiba, na likiweka bayana kwamba ni Rais Kikwete
pekee ambaye anaweza kukwamua suala hilo.
Jukwaa hilo linajumuisha taasisi kubwa za madhehebu ya Kikristo ambazo
ni Baraza la Maaskofu Katoliki nchini (TEC), Jumuiya ya Kikristo
Tanzania (CCT), Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT) na
Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA.)“Tunakuomba Mheshimiwa Rais kwamba amani ya nchi yetu sasa imo mikononi mwako hasa katika kipindi hiki cha kuandikwa kwa Katiba Mpya,” inasomeka sehemu ya tamko hilo lenye kurasa nne na kuongeza: “Tunakuomba uahirishe mchakato unaoendelea ili uepushe ishara za aina mbalimbali za kuanzisha sintofahamu nchini mwetu na hali yoyote inayoweza kuathiri vibaya mshikamano, umoja na amani ya taifa letu.”
Tamko hilo ni matokeo ya mkutano wa siku mbili uliofanyika Agosti 27
na 28, 2014 jijini Dar es Salaam ambako TCF pia walimnyooshea kidole
Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta kwamba amekuwa akiendesha
Bunge hilo kwa ubabe akijivunia wingi wa wajumbe kutoka CCM.
“Maoni
ya wananchi hayawezi kufutwa na kudharauliwa na chama tawala. Hivyo
basi, Bunge Maalumu la Katiba linaloendelea lijadili na kuboresha tu
maoni yaliyomo katika Rasimu ya Katiba na siyo kufanya mabadiliko katika
Katiba ya mwaka 1977,” inasomeka sehemu nyingine ya tamko hilo.
TCF inapendekeza kusimamishwa kwa mchakato wa Katiba ili kupisha
majadiliano, maelewano na maridhiano yatakayowezesha kurekebishwa kwa
Katiba ya sasa kwa lengo la kujenga mazingira bora ya Uchaguzi Mkuu ujao
na ule wa Serikali za Mitaa.
Lilisema
wakati Bunge hilo likiwa limesimamishwa, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba
ifanyiwe marekebisho ili kumbana Rais ajaye kuendelea na mchakato huo
baada ya kuwa maridhiano yamepatikana.
“…Baada
ya Bunge Maalumu la Katiba kuanza shughuli zake tena, Mwenyekiti wa
Bunge hilo afanye kazi kwa mujibu wa kanuni na Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba badala ya kutumia ubabe na kiburi cha wingi wa wajumbe wa CCM
katika Bunge hilo,” inasomeka sehemu nyingine ya tamko.
Tupe maoni yako hapo Chini..!!
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni