Watu
watano wanaosadikiwa kuwa majambazi, wamepigwa kwa mawe hadi kufa
wakijaribu kutoroka nguvu za umma kwa kutumia Mto Mara, wilayani Tarime
huku wakiwa na bunduki mbili zinazotumika vitani aina ya sub machine gun
(SMG).
Tukio hilo lilithibitishwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya, Lazaro Mambosasa.
Kamanda Mambosasa alisema watu waliouawa katika tukio hilo la juzi mchana hawajafahamika kwa majina wala uraia wao.
Hata
hivyo alisema siku ya tukio, majambazi hao wakiwa na silaha za kivita,
walionekana wamejificha vichakani karibu na makazi ya wananchi wa
kitongoji cha Nyabirongo, kijiji cha Gibaso katika Kata ya Nyarukoba,
Tarafa ya Ingwe iliyopo jirani na hifadhi ya Serengeti.
Lakini
baada ya kushitukiwa, walizingirwa na wananchi wenye silaha za jadi
zikiwemo mawe, marungu na mapanga huku wakipiga mayowe ambapo majambazi
hao walijibu kwa kurusha risasi hovyo ili wananchi wasiwakaribie.
Wakati
wakirusha risasi hizo zilimjeruhi mwananchi mmoja, Kagore Paul begani,
na kuwaongezea hasira wananchi walioendelea kuwasakama katika eneo
walilojificha.
Mayowe
waliyopiga yaliwaleta watu wengi zaidi muda ulivyokuwa unakwenda kiasi
cha majambazi hao kuzidiwa na kuamua kukimbia kwa kupitia Mto Mara, ili
waende upande wa pili wa wilaya ya Serengeti.
Kamanda anasema: “Wakazi
wa kijiji hicho na vijiji jirani walijitokeza kwa wingi kwani ilikuwa
mchana na kupambana na watu hao huku wakikimbilia mto Mara kutaka kuvuka
mto huo kwenda wilaya ya Serengeti kuingia mbugani, lakini juhudi zao
za kutaka kuvuka hazikifanikiwa.
“Wananchi
wa vijiji vya upande wa pili Wilaya ya Serengeti nao walijitokeza na
kuziba njia hali iliyowalazimu watuhumiwa kuingia mtoni na kutaka
kuogelea huku wakitupa silaha walizokuwa nazo majini na hapo ndipo
walipopigwa mawe na marungu wakiwa majini na kufa.
“Jeshi
letu la Polisi lilifika na kusaidia kuopoa miili ya watu hao watano
ambapo mmoja alikutwa na risasi 11 mfukoni na mwingine alikutwa na
risasi nne na fedha za Kenya Sh 350 (sawa na fedha za Tanzania sh 7,000)
ambapo inasadikiwa huenda watuhumiwa wakawa raia wa nchi jirani ya
Kenya.”
Kwa
sasa, miili ya watu hao imehifadhiwa katika chumba cha maiti cha
Hospitali ya Wilaya Tarime huku jeshi la polisi likiendelea na uchunguzi
juu ya tukio hilo.
Naye
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya Tarime, Dk Bernard Makonyu
amethibitisha kupokea miili ya watu watano iliyofikishwa hospitali hapo
na gari la polisi huku matumbo ya marehemu yakionekana kuvimba kutokana
na kunywa maji mengi kabla ya kufikwa na mauti.
Hilo
ni tukio la pili katika kipindi cha wiki tatu ambapo Agosti 3 mwaka huu
watu wanne, wakiwemo raia watatu wa Kenya na Mtanzania mmoja waliuawa
kutokana na matukio ya ujambazi katika kijiji cha Mriba.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni