.

Alhamisi, 10 Julai 2014

Obama: Marekani kumaliza mgogoro Gaza



Rais Barack Obama
Rais wa Marekani Barak Obama amesema nchi yake inajiandaa kusaidia kumaliza mgogoro katika Gaza kati ya Israel na Hamas.
Katika mazungumzo ya simu na Waziri Mkuu Benjamini Netanyahu, Rais Obama amesisitiza umuhimu wa pande zote mbili kuepuka mashambulizi zaidi ili kurudisha utulivu. Hapo awali, Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki Moon, ameliambia baraza la usalama la umoja wa mataifa lililoitishwa kwa dharura kuwa matumizi makubwa ya nguvu hayavumiliki na wanaoumia ni wananchi.
Naye Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anasema mashambulizi katika Gaza yataongezeka. Maafisa wa afya wanasema zaidi ya watu 80 wameshapoteza maisha tangu kuanza kwa mashambulizi ya Israeli katika eneo hilo la gaza.
" Mpaka sasa mapambano yanaendelea kama yalivyopangwa lakini tunaweza kutegemea mengine siku za usoni. Mpaka sasa tumeshaipiga Hamas na mashirika ya kigaidi na tutaendelea kuongeza nguvu dhidi yao kadri mapambano yanavyoendelea" Alisema Netanyau
Kwa upande wa rais wa Palestina Mahmoud Abbas anasema anayo taarifa kuwa Israel wanampango wa kuendesha oparesheni ya ardhini katika eneo la Gaza saa chache zijazo.
"serikali ya Israel imesema itafanya oparesheni ya ardhini katika ukanda wa Gaza, ambayo itaanza muda mchache ujao. Asubuhi hii tumetaarifiwa kuwa wakazi wa mpakani katika eneo la Gaza, Beit Hanoun na Beit Lahiya pamoja na vijiji na miji mikubwa walitakiwa kuondoka kuelekea katika maeneo ya katikati" Alisema Rais Mahamamod Abas

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni