Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesisitiza kuwapo kwa
maandamano yasiyo na kikomo yatakayoanza leo katika baadhi ya mikoa
licha ya jeshi la polisi kuzuia.
Chama hicho kimesema maandamano hayo yana lengo la kushinikiza kuahirishwa kwa Bunge la Katiba linaloendelea mjini Dodoma.
Malengo
mengine ni kuitaka Sheria ya Mabadiliko ya Katiba itekelezwe katika
upatikanaji wa Katiba mpya na kupinga uchakachuaji dhidi ya maoni
yaliyotolewa na wananchi kupitia Tume ya Jaji Mstaafu Joseph Warioba.
Akizungumza
na NIPASHE , Mkuu wa Idara ya Mawasiliano wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), Tumaini Makene, alisema tayari mikoa kadhaa na
wenyeviti wa mikoa wa chama hicho, wameshapeleka barua polisi ili
kutekeleza hilo.
Alisema
barua hizo lengo lake ni kupata ushirikiano wa kiulinzi kwa jeshi hilo
na siyo kuomba kibali kama ilivyozoeleka. Alisema mikoa ambayo leo
itaandamana ni Iringa, Arusha na Morogoro huku Tanga, Manyara,
Kilimanjaro, Mbeya, Mwanza na Musoma wanatarajia kuyafanya Jumatatu.
ARUSHA WAJIANDAA NA MAANDAMANO
Chadema mkoa wa Arusha, kimesema maandamano yatakayoanza leo waandamanaji watavaa vitambaa vyeupe kusisitiza amani.
Akizungumza
jana kwa njia ya simu, Mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Arusha, Amani
Golugwa , alisema wamepokea barua ya Polisi ambayo imezuia maandamano
na mkutano wa hadhara waliopanga kufanya leo. Alisema katika barua hiyo
hakuna sababu za msingi zilizotolewa hivyo Chadema na Ukawa wataandamana
kwa lazima na hakuna mtu yeyote atakayeguswa.
Hata
hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatusi Sabasi, alisema
hakuna maandamano yaliyoruhusiwa na atakayeandamana atakabiliana na
mkono wa sheria.
Wakati
hali hiyo ya sintofahamu ikiendelea baadhi ya makada wa chama hicho
wameonekana wakiwa katika harakati za kupamba magari yao kwa maandishi
ya kulaani Bunge la katiba kama maandalizi ya maandamano ya leo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni