Alhamisi, 26 Septemba 2013
Jaji Warioba adai kuwa muungano wa CUF, CHADEMA na NCCR Mageuzi ni wa KINAFIKI na hauna manufaa yoyote kwa watanzania
MWENYEKITI wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba ameonya ushirikiano ulioundwa na vyama vya siasa kupinga marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya katiba, lengo lake ni kuwagawa wananchi.
Jaji Wariona alisema ushirikiano ulioundwa na vyama vya NCCR-Mageuzi, Chama Cha Wananchi (CUF), Chama Cha Demokrasia na Maendeleo na baadhi ya vyama vya siasa hauna manufaa kwa Watanzania.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, harakati zinazofanywa na viongozi wa vyama hivyo haziwezi kuwakomboa wananchi badala yake wanafanya hivyo kwa maslahi yao binafasi.
Jaji Warioba alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kueleza hatua iliyofikiwa na tume anayoingoza baada ya kumalizika hatua ya mabaraza ya katiba.
“Kinachofanyika sasa kinaweza kuwagawa Watanzania, viongozi wasite na watafute njia, wakutane na kutafakari muafaka huu wa taifa badala ya kuwagawa.
“Hatuko kwenye mashindano, tunataka katiba itakayokubalika na Watanzania wote badala ya kulumbana kwenye majukwaa, hatutapata katiba kwenye majukwaa wala maandamano isipokuwa majadiliano.
“Lazima tuhakikishe sote tunaungana, tukitaka katiba ya mapambano hatutakuwa na katiba yenye umoja na mshikamano,” alisema Jaji Warioba.
Alisema katika kuyaendesha mabaraza ya katiba changamoto kadhaa zilijitokeza ikiwamo vyama vya siasa kuingilia uhuru wa wajumbe katika kutoa maoni yao kuhusu rasimu ya katiba.
Katika baadhi ya maeneo, wajumbe wa mabaraza walifundishwa maneno ya kusema juu ya rasimu ya katiba na wakati huo huo vyama vya siasa viliendesha mikutano ya hadhara na ya ndani kwa wanachama wao sambamba na mikutano ya mabaraza na kuingilia utulivu wa wajumbe, alisema.
“Walitumia mikutano ya hadhara kuwauliza wananchi kama wanakubaliana nayo wakayachukua kuwa ni maoni ya wananchi, hali iliyosababisha wajumbe ambao ni wanachama wa vyama kutoa maoni yao yanayofanana na miongozo waliyopewa.
“Zaidi ya hayo, baadhi ya viongozi walitoa matamshi ambayo yaliwalenga wajumbe wa tume na kuwafanya baadhi ya wajumbe wa mabaraza kuwajadili wajumbe badala ya rasimu ya katiba iliyotolewa na tume.
“Tume imesikitishwa na matamshi hayo yaliyotolewa na baadhi ya viongozi ambayo yalilenga kubeza na kuwadhalilisha wajumbe wa tume na kuishusha thamani kazi iliyofanywa na tume ya kuandika rasimu ya katiba,” alisema.
Hata hivyo, Jaji Warioba alisema pamoja na changamoto hizo zilizofanya uhusiano wa tume na wananchi kupungua, tume iliendesha mabaraza kwa mafanikio hasa sehemu ambazo wananchi hawakupewa miongozo.
Akizungumzia sheria ya mabadiliko ya katiba ya mwaka 2013, iliyopitishwa na Bunge Agosti mwaka huu, Jaji Warioba alisema ilipitishwa kwa mujibu wa sheria lakini tume haiingiliani na mhimili huo katika kutekeleza majukumu yake.
“Wabunge wana kazi yao na sisi tuna kazi yetu, wamefanya mabadiliko, ni kazi yao.
“Sheria inasema tume itavunjwa baada ya kura za maoni, lakini sasa hivi wakati Bunge la Katiba likikutana, tume itakuwapo kutoa ufafanuzi.
“Muswada huwa unapelekwa bungeni na serikali. Anayepeleka ndiye anatoa ufafanuzi, sasa sheria inasema sisi ndiyo tutakuwapo kutoa ufafanuzi.
“Sisi tulijiuliza sana kuhusu hili linawezekanaje, lakini Bunge limeona ni busara hiyo kazi ifanywe na tume, sisi hatuna ugomvi nao, tutafanya.
“Lakini pia kuna hili jingine kwamba tume italazimika kutoa elimu baada ya mabadiliko… kuna tatizo hapa, tume ikishafungwa tutatoaje elimu, tunawaomba watafakari kisha wafanye mabadiliko,” alisema Jaji Warioba.
Akikanusha taarifa ya baadhi ya wajumbe kutishia kujiuzulu.
Jaji Warioba alisema hakuna mjumbe aliyetishia kujiuzulu isipokuwa walifanya kazi katika mazingira magumu yenye changamoto nyingi, lakini tume inaendelea na kazi zake kama kawaida.
Alisema kazi inayofanywa sasa na tume ni uchambuzi wa maoni yaliyotolewa na mabaraza ya katiba kwa kufuata mwongozo ambao tume imejiwekea kwa kuzingatia uzito wa hoja zilizotolewa na wananchi.
Baada ya uchambuzi huo kukamilika, tume itaandaa ripoti ambayo itajumuisha rasimu ya katiba iliyoboreshwa kutokana na maoni ya mabaraza ya katiba, alisema.
Jaji Warioba alisema ripoti hiyo itawasilishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Zanzibar kama sheria inavyoelekeza.
Alisema mipango ya tume ni kukamilisha kazi hiyo ndani muda uliowekwa na sheria ya mabadiliko ya katiba, sura ya 83, ambako katiba yenyewe itakuwa tayari Aprili 26, mwaka 2014 katika maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano.
-Mtanzania
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni