.

Alhamisi, 26 Septemba 2013

DAKTARI FEKI WA KCMC APANDISHWA KIZIMBANI LEO...!!

MTU anayetuhumiwa kuwa daktari bandia aliyekamatwa akijiandaa kufanya upasuaji katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC leo atapandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya mjini Moshi kusomewa shitaka kwa mara ya kwanza. Mtuhumiwa huyo, Alex Sumni Massawe, alinaswa Septemba 5, mwaka huu majira ya saa 5 asubuhi katika hospitali akidai kuahidi kumfanyia upasuaji mgonjwa aliyekuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa ngozi. Kabla ya kukamatwa kwa Massawe, mama mzazi wa kijana aliyekuwa akitakiwa kufanyiwa upasuaji, Pamvelina Shirima, alikutana na daktari huyo katika baa maarufu iliyopo eneo la Dar Street na kumtoza sh 200,000 akidai zitatumika kuharakisha mwanae afanyiwe vipimo vya upasuaji. Alex anadaiwa alitaka kumfanyia upasuaji kijana, Makasi Tipesa, mkazi wa Manispaa ya Moshi ambaye amekuwa akisumbuliwa na maradhi ya ngozi kwa muda mrefu sasa. Tukio hilo lililoongeza hali ya wasiwasi kwa wagonjwa wanaopatiwa matibabu katika hospitali hiyo lilifanya uongozi wa KCMC kuimarisha hali ya ulinzi hosptalini hapo huku wagonjwa wakiendelea kupewa tahadhari ya kuwatumia madaktari wasiofahamika. Ofisa Uhusiano wa Hospitali ya KCMC, Gabriel Chisseo, alisema daktari huyo aliwekewa mtego na uongozi wa Hospitali ya KCMC baada ya baadhi ya wagonjwa kuripoti kutapeliwa na mmoja wa madaktari ambaye amekuwa akijinasibu kwamba anafanya huduma hiyo kutokana na wito alionao katika fani hiyo. Alisema mteja wa hosptali hiyo aliyekuwa akitibiwa alitapeliwa na daktari huyo na baadaye alifanikiwa kukamatwa akiwa wodi ya upasuaji baada ya kupokea kiasi cha sh 200,000 kutoka kwa Pamvelina Shirima ambaye alimpeleka mwanae afanyiwe upasuaji wa ngozi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni