.

Alhamisi, 26 Juni 2014

Gavana wa Kaunti ya Lamu nchini Kenya akamatwa kutokana na mauaji ya Mpeketoni

Issa Timamy Gavana wa Kauti ya Lamu
Issa Timamy Gavana wa Kauti ya Lamu
Daily Nation

Na Victor Melkizedeck Abuso
Polisi nchini Kenya wamemkamata na kumzuia Gavana wa Kauti ya Lamu Issa Timamy kwa tuhma za kuhusishwa na mauaji ya zaidi ya watu 60 katika mji wa Mpeketoni na vitongoji vyake Juma lililopita.

Mkuu wa idaya ya makosa ya Jinai nchini humo Ndegwa Muhoro amethibitisha kukamatwa kwa Gavana huyo siku ya Jumatano na anatarajiwa kufikishwa Mahakamani siku ya Alhamisi.
Haijafahamika vema ni makosa gani Gavana huyo anatuhumiwa kuyafanya.
Juma hili watu wengine 11 waliuliwa na watu wasiojulikana katika Kaunti hiyo ya Lamu, juma moja tu baada ya mauaji ya zaidi ya watu sitini katika eneo la Mpeketoni.
Kundi la kigaidi la Al-Shabab nchini Somalia limekiri kutekeleza mauaji haya yote kutokana na jeshi la Kenya kuwa Somalia lakini serikali ya Kenya imesema mauaji hayo yalipangwa na kuchochewa kisiasa.
Rais Uhuru Kenyatta ameonya kuwa watu wote wanaoshukiwa kupanga na kutekeleza mauaji hayo yaliyolenga jamii ya Kabila moja iliyohamia katika eneo hiyo watachukuliwa hatua za kisheria.

Watu waliopoteza maisha Mpeketoni
Reuters
Upinzani nchini Kenya umekuwa ukiishinikiza wakuu wa usalama nchini humo kujiuzulu kwa kushindwa kuwalinda wakenya na kuwahakikishia usalama wao katika siku za hivi karibuni.
Inspekta wa Polisi David Kimaiyo alinukuliwa juma hili akisema hawezi kujiuzulu kwa kile alichokisema kuwa mauaji hayo yangezuiliwa kama sio kupangwa na kochechewa kisiasa.
Maeneo mengi ya Pwani nchini Kenya yamekuwa yakishuhudia mzozo wa ardhi kutokana na wenyeji wa eneo hilo kudai kuwa ardhi yao imenyakuliwa na wageni.

Benki ya Equity iliyochomwa moto katika mji wa Mpeketoni
REUTERS/Joseph Okanga
Kuzorota kwa usalama Pwani ya Kenya tangu mashambulizi ya kigaidi ya Al Shabab yalipoanza nchini humo umesababisha nchi ya Uingereza kufunga Ubalozi wake mdogo mjini Mombasa na kuwawaomba raia wake kutozuru Pwani ya Kenya.
Mataifa mengine ambayo pia yamewarai raia wake kuwa makini wanapozuru Pwani ya Kenya ni pamoja na Ufaransa na Marekani.

tags: Kenya - Uhuru Kenyatta - Kundi la Wanamgambo la Al Shabab

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni