Rais Petro poroshenko katikati baada ya kutia sahih mkataba wa ushirikiano na ulaya.
Ukraine, Georgia na Moldova zimetia sahihi mikataba ya ushirikiano na muungano wa ulaya, swala ambalo Urusi inapinga vikali.
Makubaliano hayo ambayo yatayaunganisha pamoja
mataifa hayo na kuyaegemeza Magharibi kiuchumi na kisiasa, haswa ndio
msingi wa mgogoro ulioko Ukraine.
Urusi imesema kuwa hata ingawa kutia saini mkataba huo ni haki ya taifa lolote, kunaweza kuleta madhara mabaya baadaye.
Usitishaji wa vita kati ya vikosi vya serikali na waasi wanaounga mkono Urusi, mashariki mwa Ukraine, unakamilika Ijumaa hii.
Rais wa Ukraine, Petro Poroshenko aliusifu
mkataba huo akisema ni siku ya kihistoria katika taifa la Ukraine baada
ya siku ya Uhuru wa taifa hilo mwaka 1991.
Ameutaja kuwa dalili ya imani na nia isiyoweza kuvunjwa.
Rais Poroshenko akitia sahihi makubaliano ya ushirikiano na ulaya.
Poroshenko pia amesema kuwa ameuona mkataba huo
kama mwanzo wa mchakato wa kujiunga na Umoja wa bara Uropa,''Ukraine
inadhibitisha chaguo lake la kitaifa, kujiunga na EU" alisema.
Kwengineko, rais wa Umoja wa bara Uropa, Herman va Rompuy ametaja kuwa "siku kuu kwa bara Uropa".
''Umoja wa bara Uropa unasimama pamoja nanyi,
leo zaidi ya siku nyingine yoyote awali" aliwaambia viongozi wa nchi
hizo tatu, akiongeza kuwa hakuna chochote katika mikataba hiyo ya
makubaliano kitakachoiletea madhara Urusi kwa njia yoyote ile.
Naibu waziri wa maswala ya nje wa Urusi, Grigory
Karasin ''ameliambia shirika la habari la Interfax kuwa hatua hiyo
huenda ikazua madhara.
Kutiwa sahihi kwa mkataba huu muhimu, kwa hakika ni haki ya taifa lolote lile" alisema.
Ila tu matokeo ya Ukraine na Moldova kutia saini mkataba huu bila shaka yatakuwa mabaya".
Mapema, mshauri mkuu wa Kremlin, Sergei Glazyev
alimtaja Poroshenko kuwa mwanachama wa Nazi na kuwa uchaguzi wake kuwa
rais haukuwa wa haki kwani sehemu kubwa ya Ukraine haikupiga kura katika
uchaguzi wa mwezi Mei.
Alizidi kusema kuwa Poroshenko hana haki kikatiba kutia sahihi mkataba huo, jambo ambalo litadhuru uchumi wa Ukraine