Dar es Salaam,
Shahidi wa
pili katika kesi ya kujipatia Sh29.6 milioni kwa njia ya udanganyifu
inayomkabili mganga wa jadi, Dunia Salumu (37) ‘Manyaunyau’ amedai kuwa
walilazimika kuuza kiwanja na nyumba ya urithi kutafuta fedha za kununua
mabeberu saba na mafuta ya ngamia ili kumpa mganga huyo kama masharti
ya kumfufua ndugu yao aliyefariki dunia.
Manyaunyau alifikishwa kwa mara
ya kwanza katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Desemba mwaka 2013
akikabiliwa na shtaka la kujipatia fedha hizo kutoka kwa Tecla Modest.
Akiongozwa na Mwendesha Mashtaka,
Nassoro Katuda shahidi huyo, Diana Steven (26) alidai kuwa baada ya
kumaliza matanga ya mjomba wake, Saimon Modest aliyefariki mwaka 2008,
wakiwa nyumbani Mchikichini, Dar es Salaam walisikia sauti ya mtu
ikisema kuwa ‘mimi sijafa’.
Wakati Diana akiendelea kutoa
ushahidi huo mrefu, Hakimu Wilberforce Luhwago, alimkatisha akieleza
kuwa ameisikiliza kesi hiyo kwa muda mrefu na kuna nyingine za
kusikiliza, hivyo itaendelea Agosti 13, mwaka huu.
Ushahidi wenyewe
Alisema
siku tatu baada ya mazishi ya mjomba wake, ndugu yao aitwaye Hamisi
akiwa na Manyaunyau walifika nyumbani kutoa pole na walipofika
Manyaunyau alidai kuwa marehemu hajafa, bali ameuawa na kaka yake na
amechukuliwa na Mpemba kwa ajili ya kwenda kuuza duka.
“Mimi na mama zangu wawili
tulishtushwa na kuhoji, mtu aliyekufa anaweza akawa hai?” alisema Diana
katika ushahidi wake uliochukua saa nane.
“Baada ya hapo alituambia siku
iliyofuata twende ofisini kwake (Manyaunyau), Mburahati, tukiwa na
Sh100,000. Mama zangu walisema hawana, lakini ndugu yetu mmoja aitwaye
Bright Steven alikwenda kwenye ATM na kuchukua Sh80,000 na safari
ikafanikiwa,” alidai.
Diana alisema baada ya kupeleka
fedha hizo, Manyaunyau aliwapangia kwenda siku nyingine, akiwataka
kurudi wakiwa na kitambaa cheusi na walipokipeleka alisema alikichukua
na kukifunika kikaanza kutoa sauti ya mtu mzima ikisema: “Karibuni sana
wajukuu zangu na maelezo yote mtapewa na mwenyeji wenu.”
Alisema Manyaunyau pia aliwataka
wapeleke chupa sita za mafuta ya ngamia wakiyakosa wampelekee Sh1.8
milioni. Alisema walimpelekea fedha hizo walizozipata kwa kuuza sehemu
ya kiwanja walichorithi kwa mama yao.
“Siku tuliyopeleka hiyo hela pia
tulipeleka mtama, jogoo mwekundu na tulipelekwa katika pori lililopo
Kibamba na kila tulipokuwa tukienda kule Kibamba tulikuwa tunakodi teksi
kwa Sh40,000,” alidai Diana.
Alidai kuwa kabla ya kufika
katika pori hilo, Manyaunyau aliwaagizia soda wakanywa na baada ya
kumaliza aliwaambia wapige makofi huku wakisema hodi hodi mkubwa!
“Tuliingia katika pori hilo saa
2: 00 usiku, tukaona mwanga kama radi imepiga na tukaona kitu cheupe
kama mtu kafunikwa sanda… ile tuliyoipeleka kwa Manyaunyau siku chache
kabla ya kwenda katika pori hilo.
“Alituambia mtu wenu ndiyo huyo
ila msimfunue kwa sababu ni mchafu, akasema inatakiwa hela ya kununua
mafungu mawili ya dawa ya kumsafishia.
Sisi hatukuelewa, ndipo
alipotuambia siku iliyofuata twende ofisini kwake atufafanulie.
Tulipofika alituambia anataka mbuzi saba madume na Sh2 milioni na kwenda
naye tena Kibamba.
“Tukiwa porini hapo tulisikia
sauti ya babu ikisema marehemu wenu ameshikiliwa na wachawi, wanataka
damu ya mbuzi saba, hivyo tulirudi nyumbani na kwenda kuuza tena kiwanja
kilekile kwa mtu mwingine na kupata Sh4.9 milioni na kuzipeleka kwa
Manyaunyau kununulia mbuzi hao,” shahidi alidai na kuongeza kuwa ‘babu’
alizidi kuongeza madai, mara hii akisema anataka nguo, mkeka na chakula
nyumbani kwa Manyaunyau.
“Baada ya kauli ya babu,
tulipeleka chakula kwa Manyaunyau na hapo alituambia tujiandae kwa
safari ya Majohe na huko tulikwenda mimi na mama zangu wawili na mke wa
Manyaunyau na tulipofika tuliongea tena na ‘babu’ na kutuambia tutafute
Sh2 milioni nyingine kwa ajili ya kumkomboa ndugu yetu.”
Waliporudi kutoka Majohe, alidai
kuwa walikwenda kukopa kwa riba na Manyaunyau alisema fedha hizo
wazifunge katika kitambaa cheusi na kuziweka katika ndoo na kuzipeleka
katika Msitu wa Majohe.

“Tulipofika
Majohe tulipiga makofi na kuziweka zile pesa na siku iliyofuata
Manyaunyau alituambia tutoe Sh3.5 milioni kwa ajili ya kukanyagia na
sisi tulizipelekea hukohuko Majohe.”
Alidai kuwa siku iliyofuata
walikwenda ofisini kwa Manyaunyau na kuambiwa kuwa wapeleke chakula
nyumbani kwake baada ya hapo waende kumwangalia mchawi aliyemchukua
ndugu yao huko Kibamba eneo la makaburi.
“Tulipofika eneo hilo la makaburi
alitokea mtu mrefu sana akiwa ameshikilia mkia na akapiga magoti na
hapo hapo alitokea tena mtu mnene na kusema hamuwezi kumuona ndugu yenu
kwa sasa.”
Diana alidai kuwa baada ya kuambiwa hivyo, ilisikika sauti ya ‘babu’ ikisema watafute Sh5 milioni nyingine.
“Tulivyosikia hiyo sauti ya
‘babu’ akisema tutafute ndugu zangu walisema hawana hiyo hela na sauti
ya babu iliendelea kusema kuwa nyie leteni tu hiyo hela marehemu akija
atailipa,” alieleza.
Tupe maoni yako hapo Chini..!!